Text copied!
CopyCompare
Biblia Takatifu - Yohana - Yohana 11

Yohana 11:6-40

Help us?
Click on verse(s) to share them!
6Alipopata habari kwamba Lazaro ni mgonjwa, Yesu aliendelea kukaa mahali hapo alipokuwa kwa siku mbili zaidi.
7Kisha akawaambia wanafunzi wake, “Twendeni tena Yudea!”
8Wanafunzi wakamwambia, “Mwalimu! Muda mfupi tu umepita tangu Wayahudi walipotaka kukuua kwa mawe, nawe unataka kwenda huko tena?”
9Yesu akajibu, “Je, saa za mchana si kumi na mbili? Basi, mtu akitembea mchana hawezi kujikwaa kwa kuwa anauona mwanga wa ulimwengu huu.
10Lakini mtu akitembea usiku atajikwaa kwa maana mwanga haumo ndani yake.”
11Yesu alipomaliza kusema maneno hayo, akawaambia, “Rafiki yetu Lazaro amelala, lakini mimi nitakwenda kumwamsha.”
12Wanafunzi wake wakamwambia, “Bwana, ikiwa amelala, basi atapona.”
13Wao walidhani kwamba alikuwa amesema juu ya kulala usingizi, kumbe alikuwa amesema juu ya kifo cha Lazaro.
14Basi, Yesu akawaambia waziwazi, “Lazaro amekufa;
15Lakini nafurahi kwa ajili yenu kwamba sikuwako huko, ili mpate kuamini. Haya, twendeni kwake.”
16Thoma (aitwaye Pacha) akawaambia wanafunzi wenzake, “Twendeni nasi tukafe pamoja naye!”
17Yesu alipofika huko alikuta Lazaro amekwisha kaa kaburini kwa siku nne.
18Kijiji cha Bethania kilikuwa karibu na Yerusalemu umbali upatao kilomita tatu.
19Wayahudi wengi walikuwa wamefika kwa Martha na Maria kuwafariji kwa kifo cha kaka yao.
20Basi, Martha aliposikia kwamba Yesu alikuwa anakuja, akaenda kumlaki; lakini Maria alibaki nyumbani.
21Martha akamwambia Yesu, “Bwana, kama ungalikuwa hapa, kaka yangu hangalikufa!
22Lakini najua kwamba hata sasa chochote utakachomwomba Mungu, atakupa.”
23Yesu akamwambia, “Kaka yako atafufuka.”
24Martha akamjibu, “Najua kwamba atafufuka wakati wa ufufuo, siku ya mwisho.”
25Yesu akamwambia, “Mimi ndimi ufufuo na uzima. Anayeniamini mimi hata kama anakufa, ataishi:
26na kila anayeishi na kuniamini, hatakufa kamwe. Je, waamini hayo?”
27Martha akamwambia, “Ndiyo Bwana! Naamini kwamba wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu, yule ajaye ulimwenguni.”
28Baada ya kusema hayo, Martha alikwenda kumwita Maria, dada yake, akamwabia faraghani, “Mwalimu yuko hapa, anakuita.”
29Naye aliposikia hivyo, akainuka mara, akamwendea Yesu.
30Yesu alikuwa hajaingia kijijini, ila alikuwa bado mahali palepale Martha alipomlaki.
31Basi, Wayahudi waliokuwa nyumbani pamoja na Maria wakimfariji walipomwona ameinuka na kutoka nje ghafla, walimfuata. Walidhani alikuwa anakwenda kaburini kuomboleza.
32Basi, Maria alipofika mahali pale Yesu alipokuwa na kumwona, alipiga magoti, akamwabia, “Bwana, kama ungalikuwa hapa, kaka yangu hangalikufa!”
33Yesu alipomwona analia, na wale Wayahudi waliokuja pamoja naye wanalia pia, alijawa na huzuni na kufadhaika moyoni.
34Kisha akawauliza, “Mlimweka wapi?” Wakamwambia, “Bwana, njoo uone.”
35Yesu akalia machozi.
36Basi, Wayahudi wakasema, “Tazameni jinsi alivyompenda!”
37Lakini baadhi yao wakasema, “Je, huyu aliyemfumbua macho yule kipofu, hakuweza kumfanya Lazaro asife?”
38Basi, Yesu akiwa amehuzunika tena moyoni, akafika kaburini. Kaburi lenyewe lilikuwa pango, na lilikuwa limefunikwa kwa jiwe.
39Yesu akasema, “Ondoeni hilo jiwe!” Martha, dada yake huyo aliyekufa, akamwambia, “Bwana, amekwishaanza kunuka; amekaa kaburini siku nne!”
40Yesu akamwambia, “Je, sikukwambia kwamba ukiamini utaona utukufu wa Mungu?”

Read Yohana 11Yohana 11
Compare Yohana 11:6-40Yohana 11:6-40