1Mshukuruni Yahwe, liitieni jina lake; myafanye matendo yake yajulikane kati ya mataifa.
2Mwimbieni yeye, mwimbieni sifa yeye; semeni matendo yake yote ya ajau.
3Mjivune katika utakatifu wa jina lake; moyo wao wamtafutao Yahwe ufurahi.
4Mtafuteni Yahwe na nguvu zake; utafuteni uwepo wake siku zote.
5Kumbukeni mambo ya ajabu aliyoyatenda,
6miujiza yake na amri zitokazo kinywani mwake, enyi kizazi cha Ibrahimu mtumishi wake, enyi watu wa Yakobo, wachaguliwa wake.
7Yeye ni Yahwe, Mungu wetu. Amri zake ziko juu ya nchi yote.
8Naye hulikumbuka agano lake milele, neno alilo amuru kwa ajili ya vizazi elfu.
9Hulikumbuka agano alilolifanya na Ibrahimu na kiapo alicho mwapia Isaka.
10Hiki ndicho alicho mthibitishia Yakobo kama agano na kama agano la milele kwa Israeli.
11Alisema, “Nitakupa wewe ardhi ya Kanaani kama sehemu yako ya urithi.”
12Alisema hili wakati tu walipokuwa wachache katika hesabu, yaani wachahe sana, nao walikuwa wageni katika nchi.
13Walienda taifa hadi taifa na kutoka ufalme moja kwenda mwingine.
14Hakuruhusu yeyote kuwaonea; aliwakemea wafalme kwa ajili yao.
15Alisema, “Msiwaguze wapakwa mafuta wangu, na msiwadhuru manabii wangu.”
16Aliita njaa katika nchi; akaondoa upatikanaji wa mkate wote.
17Akatuma mtu mbele yao; Yusufu aliuzwa kama mtumishi.
18Miguu yake ilifungwa kwa pingu; alivishwa mnyororo wa chuma shingoni mwake,
19mpaka wakati wa maneno yake ulipotimia, nalo neno la Yahwe lilimjaribu.
20Mfalme alituma watumishi kumfungua; mtawala wa watu alimuweka huru.
21Alimuweka kuwa msimamizi wa nyumba yake kama mtawala wa mali zake zote
22kuwaelekeza wakuu kama alivyopenda na kuwafundisha viongozi wake hekima.
23Kisha Israeli iliingia Misri, na Yakobo aliishi kwa muda katika nchi ya Hamu.
24Yahwe aliwajalia watu wake wazae sana, na aliwafanya wenye nguvu kuliko adui zao.
25Alisababisha adui zao wawachukie watu wake, na kuwatendea visivyo watumishi wake.
26Alimtuma Musa, mtumishi wake, na Haruni, ambaye alikwisha mchagua.
27Walifanya ishara zake kati ya Wamisri na maajabu yake katika ya nchi ya Hamu.
28Alituma giza na likaifanya nchi hiyo kuwa giza, lakini watu wake hawakutii amri zake.
29Aligeuza maji kuwa damu na aliua samaki wao.
30Nchi yao ilijaa vyura, hata katika vyumba vya watawala wao.
31Alisema, na makundi ya inzi na chawa wakaja mjini mwote.
32Aliigeuza mvua yao kuwa mvua ya mawe, pamoja na miali ya moto juu ya ardhi yao.
33Aliiharibu mizabibu yao na mitini yao; akaivunja miti ya mji wao.
34Alisema, na nzige wakaja, nzige wengi sana.
35Nzige walikula mboga zao zote za majani katika nchi yao. Walikula mazao yote ardhini.
36Aliua kila mzaliwa wa kwanza katika nchi yao, malimbuko ya nguvu zao.
37Aliwatoa nje Waisraeli wakiwa na fedha na dhahabu; hakuna mmoja wa kabila lake aliyejikwaa njiani.
38Misri ilifurahi walipoondoka, maana Wamisri waliwaogopa.
39Alitandaza wingu liwafunike na alifanya moto uwaangazie wakati wa usiku.
40Waisraeli waliomba chakula, naye aliwaletea kware na aliwatosheleza kwa mkate kutoka mbiguni.
41Aliugawa mwamba, maji yalimwagika kutoka humo; yalitiririka katika jangwa kama mto.
42Kwa maana alikumbuka ahadi yake takatifu aliyoifanya kwa Ibrahimu mtumishi wake.
43Aliwaongoza watu wake kwa furaha, wateule wake kwa kelele za ushindi.
44Aliwapa nchi za mataifa; walichukua milki ya mali za watu
45ili waweze kushika amri zake na kutii sheria zake. Msifuni Yahwe.