Text copied!
CopyCompare
Biblia ya Kiswahili - Zaburi

Zaburi 48

Help us?
Click on verse(s) to share them!
1Yahwe ndiye aliye mkuu na mwenyekusifiwa sana, katika mji wa Mungu wetu kwenye mlima wake mtakatifu.
2Ni mzuri katika mwinuko wake, furaha ya nchi yote, ni mlima Sayuni, kwenye upande wa kaskazini, mji wa Mfalme mkuu.
3Mungu amejifunua mwenyewe katika jumba lake la kifahari kama kimbilio la usalama.
4Maana, tazama, wafalme walikusanyika wenyewe; wote pamoja walipita.
5Nao waliuona, wakashangaa; walifadhaika, na wakaharakisha kuondoka.
6Pale pale tetemeko liliwashikilia, maumivu makali kama mwanamke anaye zaa.
7Kwa upepo wa mashariki wewe huivunja meli ya Tarshishi.
8Kama tulivyo sikia, vivyo hivyo tumeona katika mji wa Yahwe wa majeshi, katika mji wa Mungu wetu; Mungu atautunza milele. Selah
9Tumeutafakari uaminifu wa agano lako, Mungu, katikati ya hekalu lako.
10Kama lilivyo jina lako, Mungu, hivyo ndivyo zilivyo sifa zako mpaka miisho ya dunia; mkono wako wa kuume umejaa haki.
11Milma Sayuni na ufurahi, nao wana wa Yuda washangilie kwa sababu ya amri ya haki yako.
12Tembeeni katika Mlima Sayuni, muuzungukie mji,
13mzitazame kwa makini nguzo zake, na mtazame majumba yake ya kifahari ili kwamba muweze kuwasimulia kizazi kijacho.
14Kwa kuwa huyu Mungu ni Mungu wetu milele na milele; naye atakuwa kiongozi wetu mpaka kufa.