1Msifuni Yahwe. Mshukuruni Yahwe, kwa kuwa ni mwema, kwa maana uaminifu wa agano lake wadumu milele.
2Ni nani awezaye kuyahesabu mataendo makuu ya yahwe au kutangaza katika ukamilifu sifa zote za matendo yake ya kuaminika.
3Wamebarikiwa wale watendao yaliyo mema na matendo yao yaliyo haki siku zote.
4Ukumbuke, Ee Yahwe, unapowaonesha watu wako neema; unisaidie unapowaokoa.
5Ndipo nitaona mafanikio ya wateule wako, wakifurahia katika furaha ya taifa lako, na utukufu pamoja na urithi wako.
6Tumefanya dhambi kama babu zetu, tumekosea, na kufanya uovu.
7Baba zetu hawakuyatambua matendo yako ya ajabu katika Misri; walipuuzia matendo yako mengi ya uaminifu wa agano; waliasi penye bahari, bahari ya Shamu.
8Hata hivyo, yeye aliwaokoa kwa ajili ya jina lake ili kwamba aweze kuzifunua nguvu zake.
9Aliikemea Bahari ya Shamu, nayo ikakauka. Kisha akawaongoza vilindini, kana kwamba ni jangwani.
10Aliwaokoa kutoka mkononi mwa wale waliowachukia, na aliwaokoa kutoka mkononi mwa adui.
11Lakini maji yaliwafunika washindani wao; hakuna hata mmoja aliye okolewa.
12Ndipo waliyaamini maneno yake, nao waliimba sifa zake.
13Lakini walisahau haraka kile alichofanya; hawakuyasubiri maelekezo yake.
14Walikuwa na tamaa isiyotoshelezwa jangwani, wakamjaribu Mungu nyikani.
15Aliwapa ombi lao, lakini alituma gonjwa ambalo lilishambulia miili yao.
16Katika kambi wakawa na wivu juu Musa na Haruni, kuhani mtakatifu wa Yahwe.
17Nchi ilifunguka na ilimmeza Dathani na iliwafunika wafuasi wa Abiramu.
18Moto uliwaka kati yao; moto uliwaangamiza waovu.
19Walitengeneza ndama huko Horebu na kuabudu sanamu ya kuyeyuka.
20Wakaubadili utukufu wa Mungu kuwa mfano wa ng'ombe alaye majani.
21Walimsahau Mungu wokozi wao, aliyefanya mambo makuu katika Misri.
22Alifanya matendo ya ajabu katika nchi ya Hamu na matendo makuu penye Bahari ya Shamu.
23Mungu angetangaza uharibifu wao, kama sio Musa, mteule wake, aliingilia kati kugeuza hasira yake dhidi ya kuwaangamiza.
24Kisha waliidharau nchi yenye matunda; hawakuiamini ahadi yake,
25bali walilalamiaka katika mahema yao, na hawakumtii Yahwe.
26Kwa hiyo aliinua mkono wake na kuapa kwao kuwa atawaacha wafe jangwani,
27akitawanya uzao wao kati ya mataifa, na kuwatawanya katika nchi za kigeni.
28Waliabudu Baal ya Poeri na walizila dhabihu zilizotolewa kwa wafu.
29Walimkasirisha kwa matendo yao, na pigo la gonjwa baya liliwashambulia kati yao.
30Ndipo Finehasi aliinuka kuingilia kati, na pigo likakoma.
31Ilihesabika kwake kama tendo la haki kwa vizazi vyote hata milele.
32Pia walimkasirisha Yahwe penye maji ya Meriba, na Musa aliteseka kwa ajili yao.
33Walimghadhabisha Musa naye akaongea haraka.
34Hawakuyaharibu mataifa kama Yahwe alivyowaamuru,
35bali walichangamana na mataifa na walijifunza njia zao
36nao waliabudu sanamu, nazo zikawa mtego kwao.
37Waliwatoa wana wao na binti zao kwa mapepo.
38Walimwaga damu isiyo na hatia, damu ya wana na binti zao, ambao waliwatoa kama dhabihu kwa sanamu za Kanaani, waliinajisi nchi kwa damu.
39Walinajisiwa kwa matendo yao; katika matendo yao walikuwa kama malaya.
40Hivyo Yahwe aliwakasilikia watu wake, akawadharau watu wake mwenyewe.
41Akawaruhusu mataifa, na wale walio wachukia wakawatawala.
42Maadui zao wakawaonea, wakatiishwa chini ya mamlaka yao.
43Mara nyingi alienda kuwasaidia, lakini waliendelea kuasi nao walishushwa chini kwa dhambi zao wenyewe.
44Hata hivyo, aliiangalia dhiki yao aliposikia kilio chao kwa ajili ya msaada.
45Alikumbuka agano lake pamoja nao na alijirudi kwa sababu ya upendo wake thabiti.
46Aliwafanya wote waliowateka wawahurumie.
47Utuokoe, Ee Yahwe, Mungu wetu. Utukusanye kutoka kati ya mataifa ili kwamba tuweze kulishukuru jina lako takatifu na utukufu katika sifa zako. Yahwe,
48Mungu wa Israeli, na asifiwe toka milele na milele. watu wote walisema, “Amen.” Msifuni Yahwe. Kitabu cha tano.