Text copied!
CopyCompare
Biblia ya Kiswahili - Zaburi

Zaburi 104

Help us?
Click on verse(s) to share them!
1Nitamsifu Yahwe maisha yangu yote, Ewe Yahwe Mungu wangu, wewe ni mkubwa sana; umevikwa kwa utukufu na enzi.
2Unajifunika mwenyewe kwa nuru kama kwa mavazi; umetandaza mbingu kama pazia za hema.
3Umeweka mawinguni mihimili ya vyumba vyako; huyafanya mawingu gari lako; hutembea juu ya mbawa za upepo.
4Yeye huufanya upepo kuwa wajumbe wake, miale ya moto kuwa watumishi wake.
5Aliiweka misingi ya nchi, nayo haitahamishwa kamwe.
6Wewe uliifunika nchi kwa maji kama kwa mavazi; maji yalifunika milima.
7Kukemea kwako kulifanya maji kupungua; kwa sauti ya radi yako yakaondoka kasi.
8Milima iliinuka, na mabonde yakaenea mahali ambapo wewe ulikwisha pachagua kwa ajili yao.
9Umeweka mipaka kwa ajili yao ambao hayawezi kuupita; hayawezi kuifunika nchi tena.
10Yeye alifanya chemchemi kutiririsha maji mabondeni; mito kutiririka katikati ya milima.
11Inasambaza maji kwa ajili ya wanyama wote wa shambani; punda wa porini hukata kiu yao.
12Kandokando ya mito ndege hujenga viota vyao; huimba kati ya matawi.
13Humwagilia milima kutoka katika chumba chake cha maji mawinguni. Nchi imejazwa kwa matunda ya kazi yake.
14Huzifanya nyasi kukua kwa ajili ya mifugo na mimea kwa ajili ya binadamu kulima ili kwamba mwanadamu aweze kuzalisha chakula toka nchini.
15Hutengeneza mvinyo kumfurahisha mwanadamu, mafuta yakumfanya uso wake ung'ae, na chakula kwa ajili ya kuimarisha uhai wake.
16Miti ya Yahwe hupata mvua nyingi; Mierezi ya Lebanoni aliyoipanda.
17Hapo ndege hutengeneza viota vyao. Na korongo, misunobari ni nyuma yake.
18Mbuzi mwitu huishi kwenye milima mrefu; na urefu wa milima ni kimilio la wibari.

19Aliuchagua mwezi kuweka alama ya majira; jua latambua kuchwa kwake.
20Wewe hufanya giza la usiku ambapo wanyama wote wa msituni hutoka nje.
21Wana simba huunguruma kwa ajili ya mawindo na hutafuta chakula chao kutoka kwa Mungu.
22Jua linapochomoza, huenda zao na kujilaza mapangoni mwao.
23Wakati huo huo, watu hutoka nje kuelekea kazi zao na utumishi wake mpaka jioni.
24Yahwe, ni jinsi gani kazi zako zilivyo nyingi na za aina mbalimbali! Kwa hekima ulizifanya zote; nchi inafurika kwa kazi zako.
25Kule kuna bahari, yenye kina kirefu na pana, ikiwa na viume vingi visivyo hesabika, vyote vidogo na vikubwa.
26Meli husafili humo, na ndimo alimo Lewiathani uliye muumba acheze baharini.
27Hawa wote hukutazama wewe uwape chakula kwa wakati.
28Unapowapa chakula, hukusanyika; ufunguapo mkono wako, wanatosheka.
29Unapouficha uso wako, wanateseka; ukiiondoa pumzi yao, wanakufa na kurudi mavumbini.
30Unapotuma Roho yako, wanaumbwa, nawe unaifanya upya nchi.
31Utukufu wa Yahwe na udumu milele; Yahwe na aufurahie uumbaji wake.
32Yeye hutazama nchi, nayo hutikisika; huigusa milima, nayo hutoa moshi.
33Nitamwimbia Yahwe maisha yangu yote; nitamwimbia sifa Mungu wangu nigali ninaishi.
34Mawazo yangu na yawe matamu kwake; nitafurahia katika Yahwe.
35Wenye dhambi na waondoshwe katika nchi, na waovu wasiwepo tena. Ninamsifu Yahwe maisha yangu yote. Msifuni Yahwe.