Text copied!
CopyCompare
Biblia ya Kiswahili - Ayubu

Ayubu 21

Help us?
Click on verse(s) to share them!
1Kisha Ayubu akajibu na kusema,
2“Sikilizeni hotuba yangu kwa makini, hii na iwe faraja yenu.
3Nimeteswa, lakini pia nitasema; nikisha kusema, endeleeni kudhihaki.
4Lakini kwangu mimi, malalamikio yangu ni kwa mtu? Kwa nini nisiwe mwenye subira?
5Nitazameni na mshangae, nanyi wekeni mkono wenu midomoni mwenu.
6Ninapoyafikiria mateso yangu, ninaumizwa, mwili wangu unaogopa.
7Kwa nini waovu wanaendelea kuishi, wanazeeka, na kuwa na uwezo katika madaraka?
8Wazao wao wanathibitishwa mbele zao, na uzao wao unaimarika machoni pao.
9Nyumba zao ziko salama mbali na hofu; wala fimbo ya Mungu haiko juu yao.
10Dume lao la ng'ombe linazalisha; halishindwi kufanya hivyo; ng'ombe wao anazaa na hafishi ndama wake akiwa mchanga.
11Wanawapeleka wadogo wao kama kundi la kondoo, na watoto wao hucheza.
12Wanaimba kwa tari na vinubi na hufurahi kwa muziki na zomari.
13Wanatumia siku zao katika mafanikio, na wanashuka kuzimu kwa utulivu.
14Wanamwambia Mungu, 'Ondoka kwetu kwani hatutaki ufahamu wowote juu ya njia zako.
15Mwenye enzi ni nani, hata tumwabudu? Tutafaidika na nini tukimwabudu? Tutapata faida gani ikiwa tutamwomba?
16Tazama, je mafanikio yao hayamo katika mikono yao wenyewe? Sina cha kufanya na ushauri wa waovu.
17Mara ngapi taa za waovu huzimwa, au kwamba majanga huja juu yao? Mara ngapi inatokea kwamba Mungu husambaza huzuni kwao kwa hasira?
18Ni mara ngapi inatokea kwamba wanakuwa kama mabua mbele ya upepo au kama makapi yanayopeperushwa na dhoruba?

19Mnasema, 'Mungu huweka hatia ya mtu kwa watoto wake kuilipa.' Na alipe yeye mwenyewe, ili kwamba aweze kujua hatia yake mwenyewe.
20Acha macho yake yaone uangamivu wake mwenyewe, na acha anywe gadhabu ya Mwenyezi.
21Kwani anaangaliaje familia yake mbele yake idadi ya miezi yake inapokwisha.
22Je kuna mtu anaweza kumfundisha Mungu maarifa kwa kuwa yeye huwaukumu hata walio juu?
23Mtu mmoja ufa katika nguvu zake kamili, akiwa na utulivu kabisa na kwa amani.
24Mwili wake hauna uhitaji, na kiini cha mifupa yake ina unyevu na afya njema.
25Mtu mwingine ufa kwa uchungu wa nafsi, bila kujifurahisha kwa jambo lolote jema.
26Wanazikwa kaburini wote kwa pamoja, funza wanawafunika wote.
27Tazama, nayajua mawazo yenu, na jinsi mnavyotaka kunikosesha.
28Kwa kuwa mwasema, 'Iko wapi sasa nyumba ya mwana wa mfalme? Liko wapi kao alipokaa mwovu?'
29Je hamjawauliza wasafiri? Hamfahamu wanavyoweza kusema,
30kwamba mwovu anaepushwa na siku ya shida, na kwamba anawekwa mbali na siku ya gadhabu?
31Ni nani atakaye ituhumu siku ya mwovu mbele yake? Ni nani atakayemwadhibu kwa alichokifanya?
32Hata hivyo atapelekwa kaburini; watu wataliona kaburi lake.
33Udongo wa bondeni utakuwa mtamu kwake; watu wote watamfuata, hata kuwe na watu wengi mbele yake.
34Ni jinsi gani basi mtanifariji bila kufikiri, kwa kuwa majibu yenu hayana lolote ila uongo?”