Text copied!
CopyCompare
Biblia ya Kiswahili - Ayubu

Ayubu 30

Help us?
Click on verse(s) to share them!
1Sasa vijana wananidhihaki - vijana ambao baba zao wasingeweza hata kuwahudumia mbwa wa kundi langu.
2Kwa kweli, nguvu za mikono ya baba zao, zingenisaidia nini - watu ambao hawakuwa na nguvu wakati wa kukua kwao?
3Walidhoofishwa na umasikini na njaa; walisaga nchi kavu mafichoni.
4Walichuma mche chumvi na majani ya vichaka; mizizi ya mti wa ufagio ilikuwa ndiyo chakula chao.
5Waliondolewa miongoni mwa watu waliopiga kelele nyuma yao kama ambavyo mtu angempigia kelele mwizi.
6Hivyo walipaswa kuishi katika mabonde ya mto, katika mashimo ya ardhi na miamba.
7Walilia kwa uchungu porini kama punda; chini ya vichaka walikutana.
8Walikuwa uzao wa wapumbavu, hakika, wa watu wasiofaa; waliondolewa duniani kama waarifu.
9Lakini sasa, nimekua sababu ya wimbo wa dhihaka kwa wana wao; hakika, nimekuwa mzaa kwao.
10Wananichukia na kusimama mbali nami; hawaachi kunitemea usoni.
11Kwa maana Mungu ameondoa kamba katika upinde wangu na amenipiga, na hivyo watu hawa wanashindwa kujizuia mbele yangu.
12Kundi la vijana wabaya wanashambulia nguvu zangu; wananiondolea mbali na kukusanya kinyume changu rundo la kuhusuru.
13Wanaharibu maisha yangu; wanapeleka mbele maangamizi yangu, watu wasio na wakuwazuia.
14Wanakuja kinyume changu kama jeshi katika tundu pana katika ukuta wa mji; katikati ya maangamizi wanajizungusha juu yangu.
15Hofu zimeniandama; heshima yangu imeondolewa mbali nami kama kwa upepo; mafanikio yangu yameondolewa kama wingu.
16Sasa uhai wangu umeondolewa ndani yangu; siku nyingi za maumivu zimenipita.
17Mifupa inauma ndani yangu wakati wa usiku; maumivu yanayonisaga hayaishi.
18Nguvu kuu ya Mungu imeshika mavazi yangu; yananizunguka kama kala ya vazi langu.

19Amenitupa matopeni; nimekuwa kama vumbi na majivu.
20Nakulilia wewe, Mungu, lakini haunijibu; ninasimama, nawe unaniangalia tu.
21Umegeuka na kuwa mkali kwangu; kwa nguvu za mkono wako umenitesa.
22Unaniinua katika upepo na kuufanya unikokote; unanirusha huku na kule katika dhoruba.
23Kwa maana najua ya kwamba utanipeleka mautini, nyumba ya hatima kwa viumbe vyote.
24Lakini, je hakuna ainuaye mkono wake kuomba msaada aangukapo? Je hakuna aombaye msaada akiwa tabuni?
25Je sikulia kwa ajili yake aliyekuwa tabuni? Je sijahuzunika kwa ajili ya mwitaji?
26Nilipotazamia mema, ndipo yalipokuja mabaya; niliposubiri nuru, giza lilikuja badala yake.
27Moyo wangu umetaabika na hautulii; siku za mateso zimenipata.
28Nimekuwa na ngozi nyeusi lakini si kwa sababu ya jua; nasimama katika kusanyiko na kulilia msaada.
29Nimekuwa ndugu kwa mbwea, mshirika wa mbuni.
30Ngozi yangu imekuwa nyeusi na inapukutika; mifupa yangu imeunguzwa na joto.
31Kwa hiyo kinubi changu kimefunguliwa kwa nyimbo za maombolezo, zomari yangu kwa kuimba kwao waombolezao.