1Watu wangu, sikieni mafundisho yangu, sikilizeni maneno ya kinywa changu.
2Nitafungua kinywa changu katika mifano; nitaimba kuhusu mambo yaliyofichika yahusuyo yaliyopita.
3Haya ni mambo ambayo tumeyasikia na kujifunza mambo ambayo mababu zetu wametuambia sisi. Hatutawaficha uzao wao.
4Tutawaambia kizazi kijacho kuhusu sifa anazostahili Yahwe kwa matendo yake, nguvu zake, na maajabu ambayo ameyafanya.
5Kwa kuwa yeye alianzisha agano la amri katika Yakobo na sheria maalumu katika Israeli. Yeye aliamuru mababu zetu kuwa walipaswa kuzifundisha kwa watoto wao.
6Aliamuru hivi ili kwamba kizazi kijacho kiweze kuzijua amri zake, ili wawafundishe wana ambao bado hawajazaliwa.
7Kisha wangeweka tumaini lao katika Mungu na kutokusahau matendo yake bali wazishike amri zake.
8Ndipo wasingekuwa kama mababu zao, ambao walikuwa wakaidi na wenye uasi, kizazi ambacho mioyo yao haikuwa kamilifu, na ambao roho zao hazikuwa na nia thabiti na aminifu kwa Mungu.
9Waefraimu walikuwa na silaha na upinde, lakini walikimbia siku ya vita.
10Hawakutunza agano na Mungu, na walikataa kutii sheria yake.
11Walisahau matendo yake, mambo ya ajabu ambayo yeye amewaonesha wao.
12Walisahau mambo ya ajabu aliyofayafanya machoni pa mababu zao katika nchi ya Misri, katika ardhi ya Soani.
13Aliigawa bahari na akawaongoza katikati ya bahari; aliyafanya maji yasimame kama kuta.
14Wakati wa mchana aliwaongoza kwa wingu na usiku wote kwa nuru ya moto.
15Alipasua miamba jangwani, na aliwapa maji mengi, ya kutosha kujaza vina virefu vya bahari.
16Alifanya maporomoko ya maji kutiririka tokea mwambani na aliyafanya maji yatiririke kama mito.
17Lakini bado waliendelea kutenda dhambi dhidi yake, wakiasi dhidi ya Aliye Juu katika jangwa.
18Walimjaribu Mungu mioyoni mwao kwa kuomba chakula cha kuwatosheleza hamu zao.
19Waliongea dhidi ya Mungu; walisema, “Kweli Mungu anaweza kuweka meza ya chakula kwa ajili yetu jangwani?
20Tazama, wakati alipoupiga mwamba, maji yalibubujika, mito ikafurika. Lakini anaweza kutoa mkate tena? Ataweza kuleta nyama kwa watu wake?”
21Yahwe aliposikia haya, alikasirika; moto wake uliwaka dhidi ya Yakobo, hasira yake ikamshambulia Israeli,
22kwa sababu hawakumwamini Mungu na hawakuamini katika wokovu wake.
23Lakini yeye bado aliziamuru mbingu juu na kufungua milango ya mbingu.
24Aliwanyeshea mana ili wale, na aliwapa nafaka kutoka mbinguni.
25Watu walikula mikate ya malaika. Aliwatumia chakula kingi.
26Alisababisha upepo wa mashariki kupiga mawinguni, na kwa uweza wake aliuongoza upepo wa kusini.
27Aliwanyeshea nyama kama mavumbi, na ndege kama wingi wa mchanga wa baharini.
28Walianguka katikati ya kambi yao, na maeneo yote karibu na hema zao.
29Hivyo walikula na walishiba. Maana aliwapa kile walichokitamani sana.
30Lakini walikuwa bado hawajatosheka; chakula chao kilikuwa bado kinywani mwao.
31Ndipo hasira ya Mungu iliwashambulia na kuwaua wenye nguvu kati yao. Aliwaangusha chini vijana wa Israeli.
32Licha ya hili, waliendelea kutenda dhambi na hawakuyaamini matendo yake ya ajabu.