36Uelekeze moyo wangu kuzielekea amari za agano lako na uniweke mbali na matendo yasiyo haki tena.
37Uyageuze macho yangu dhidi ya kutazama mambo yasiyofaa; unihuishe katika njia zako.
38Umtendee mtumishi wako ahadi ambayo uliifanya kwa wale wanaokuheshimu wewe.
39Uniondolee shutumu niiogopayo, maana hukumu zako za haki ni njema.
40Tazama, nimeyatamani maagizo yako; unihuishe katika haki yako. VAV.
41Ee Yahwe, unipe upendo wako usiokwisha na wokovu wako kulingana na ahadi yako;
42ndipo nitakuwa na jibu kwa ajili ya yule anayenidhihaki.
43Usiliondoe neno la kweli mdomoni mwangu, maana nimesubiri kwa ajili ya amri zako za haki.
44Nitazitii sheria zako siku zote, milele na milele.
45Nitaenenda salama, maana ninayatafuta maagizo yako.
46Nitazinena amri zako thabiti mbele ya wafalme nami sitaaibika.
47Ninafurahia katika amri zako, nizipendazo sana.
48Nitaziinulia mikono yangu amri zako, nizipendazo; nitazitafakari sheria zako. ZAYIN.
49Kumbuka ahadi yako kwa mtumishi wako kwa sababu umenipa tumaini.
50Hii ni faraja yangu katika mateso: kuwa ahadi yako imeniweka hai.
51Wenye kiburi wamenicheka, lakini sijaiacha sheria yako.
52Nimezitafakari amri zako za haki tangu zamani, Yahwe, nami ninajifariji mwenyewe.
53Hasira kali imenishikilia kwa sababu ya waovu wanaoikataa sheria yako.
54Sheria zako zimekuwa nyimbo zangu katika nyumba ninayoishi kwa muda.
55Ninalifikiria jina lako wakati wa usiku, Yahwe, na kuzishika sheria zako.
56Hili limekuwa zoezi langu kwa sababu nimeyatii maagizo yako. HETH.
57Yahwe ni sehemu yangu; nimeamua kuyatii maneno yake.
58Kwa bidii ninaomba neema yako kwa moyo wangu wote; unihurumie, kama neno lako lilivyo ahidi.
59Nilizichunguza njia zangu na kugeuzia miguu yangu kwenye amri za agano lako.
60Naharakisha na sichelewi kuzishika amri zako.
61Kamba za waovu zimenifunga; nami sijaisahau sheria yako.
62Katikati ya usiku ninaamka kukushukuru wewe kwa sababu ya amri za haki yako.
63Ninaurafiki na wale wanao kuabudu wewe, wale wote watiio maagizo yako.
64Yahwe, nchi, imejaa uaminifu wa agano lako; unifundishe sheria zako. TETH.
65Wewe umemtendea mema mtumishi wako, Yahwe, sawasawa na neno lako.
66Unifundishe utambuzi sahihi na uelewa, kwa kuwa nimeamini katika amri zako.
67Kabla sijateswa nilipotea, lakini sasa nimelitii neno lako.
68Wewe ni mwema, na ndiye yule utendaye mema; unifundishe sheria zako.
69Wenye kiburi wamenichafua kwa uongo, lakini niliyashika maagizo yako kwa moyo wangu wote.
70Mioyo yao ni migumu, lakini ninafurahia katika sheria yako.
71Ni vizuri kwangu kuwa nimeteseka ili niweze kujifunza sheria zako.
72Maagizo yatokayo kinywani mwako ni ya thamani zaidi kwangu kuliko maelfu ya vipande vya dhahabu na fedha. YOD.
73Mikono yako imeniumba na kunitengeneza; unipe uelewa ili niweze kujifunza amri zako.
74Wale wanao kucha wewe watafurahi wanionapo kwa sababu ninapata tumaini katika neno lako.
75Ninajua, Yahwe, kuwa amri zako ni za haki, na kuwa katika uaminifu ulinitesa.
76Agano lako aminifu na linifariji, kama ulivyomwahidi mtumishi wako.
77Unihurumie ili niweze kuishi, kwa maana sheria yako ni furaha yangu.
78Wenye kiburi na waaibishwe, maana wamenitukana; bali mimi nitayatafakari maagizo yako.