Text copied!
CopyCompare
Biblia ya Kiswahili - Mithali

Mithali 18

Help us?
Click on verse(s) to share them!
1Yule ambaye hujitenga hutafuta matakwa yake mwenyewe na hupingana na hukumu zote za kweli.
2Mpumbavu hapati raha katika ufahamu, lakini hufunua kile kilichopo katika moyo wake.
3Mtu mwovu anapokuja, dharau huja pamoja naye- sambamba na aibu na shutuma.
4Maneno ya kinywa cha mtu ni maji yenye kina kirefu; chemchemi ya hekima ni mkondo unaotiririka.
5Si vema kuwa na upendeleo kwa mwovu, wala haifai kukana haki kwa wale watendao mema.
6Midomo ya mpumbavu huletea mafarakano na kinywa chake hukaribisha mapigo.
7Kinywa cha mpumbavu ni uharibifu wake na hujinasa mwenye kwa midomo yake.
8Maneno ya mmbea ni kama chembe tamu na hushuka katika sehema za ndani sana kwenye mwili.
9Basi, ambaye ni mzembe katika kazi yake ni ndugu yake anayeharibu wengi.
10Jina la Yehova ni mnara imara; atendaye haki hukimbilia na kuwa salama.
11Mali ya tajiri ni mji wake imara na katika fikira zake ni kama ukuta mrefu.
12Moyo wa mtu huwa na kiburi kabla ya anguko lake, bali unyenyekevu hutangulia kabla ya heshima.
13Anayejibu kabla ya kusikiliza- ni upuuzi na aibu yake.
14Roho ya mtu itajinusuru na madhara, bali roho iliyopondeka nani anaweza kuivumilia?
15Moyo wa mwenye akili hujipatia maarifa na usikivu wa mwenye busara huitafuta.
16Zawadi ya mtu inaweza kufungua njia na kumleta mbele ya mtu muhimu.
17Wa kwanza kujitetea katika shitaka lake huonekana kuwa na haki hadi mpinzani wake aje na kumuuliza maswali.
18Kupiga kura kunamaliza mabishano na kuwatawanya wapinzani imara.

19Ndugu aliyechukizwa ni mgumu kushawishiwa kuliko mji wenye nguvu, na kugombana ni kama makomeo ya ngome.
20Tumbo la mtu litashiba kutoka kwenye tunda la kinywa chake; atatoshelezwa kwa mavuno ya midomo yake.
21Uzima na kifo hutawaliwa kwa ulimi, na wale wenye kuupenda ulimi watakula tunda lake.
22Yeye apataye mke anapata kitu chema na kupokea fadhila kutoka kwa Yehova.
23Mtu masikini huomba rehema, lakini mtu tajiri hujibu kwa ukali.
24Anayejidai kwa marafiki wengi watamleta katika uharibifu, bali yupo rafiki ambaye huwa karibu kuliko ndugu.