Text copied!
CopyCompare
Biblia ya Kiswahili - Mithali

Mithali 21

Help us?
Click on verse(s) to share them!
1Moyo wa mfalme ni mfereji wa maji katika mkono wa Yehova; anaugeuza popote anakopenda.
2Kila njia ya mtu ni sawa katika macho yake mwenyewe, lakini ni Yehova anayeipima mioyo.
3Kutenda haki na adili hukubaliwa zaidi na Yehova kuliko sadaka.
4Macho ya kiburi na moyo wa majivuno- taa ya waovu- ni dhambi.
5Mipango ya mwenye juhudi huelekea kwenye mafanikio tu, bali kila mtu anayetenda kwa haraka huelekea umasikini.
6Kujipatia utajiri kwa ulimi wa uongo ni mvuke unaopita upesi na mtego ambao unafisha.
7Vurugu ya waovu itawaburuta mbali, maana wanakataa kutenda haki.
8Njia ya mwenye hatia ni ukatiri, bali mwenye usafi hutenda yaliyo ya haki.
9Bora kuishi kwenye kona ya juu darini kuliko katika nyumba pamoja na mke mgonvi.
10Hamu ya mwovu ni uchu wa mabaya; jirani yake haoni ukarimu katika macho yake.
11Mwenye dhihaka anapoadhibiwa mjinga hupata busara, na mtu mwenye busara anapofundishwa, anaongeza maarifa.
12Atendaye haki huilinda nyumba ya mwovu; huwashusha waovu kwenye uharibifu.
13Anayeziba masikio yake kwenye kilio cha masikini, pia atalia, lakini hatajibiwa.
14Zawadi ya siri hutuliza hasira na zawadi ya kificho hutuliza ghadhabu kuu.
15Haki ikitendeka, huleta furaha kwa mwenye kutenda wema, lakini huleta hofu kubwa kwa watenda mabaya.
16Yule anayezurura kutoka kwenye njia ya ufahamu, atapumzika kwenye kusanyiko la wafu.
17Anayependa raha atakuwa masikini; anayependa divai na mafuta hawezi kuwa tajiri.
18Mtu mbaya ni fidia kwa yule atendaye haki, na mdanganyifu ni fidia kwa waaminifu.

19Bora kuishi jangwani kuliko kuishi pamoja na mwanamke ambaye huchochea sana ugomvi na malalamiko.
20Hazina yenye thamani na mafuta vipo nyumbani kwa mwenye busara, bali mtu mpumbavu huviharibu.
21Mtu atendaye haki na mwema -huyu mtu hupata uzima, haki na heshima.
22Mtu mwenye busara huupima mji wa mashujaa, na huiangusha ngome wanayoitumaini.
23Anayelinda kinywa chake na ulimi wake hujilinda mwenyewe na taabu.
24Mtu mwenye kiburi na maringo- “Dhihaka” ndilo jina lake - hutenda kwa majivuno na kujidai.
25Shauku ya mtu mvivu itamuua, maana mikono yake hukataa kufanya kazi.
26Kwa siku nzima hupatwa na uchu na uchu zaidi, lakini atendaye haki hutoa na wala hazuii.
27Sadaka ya mwovu ni chukizo; huwa ni chukizo zaidi anapoileta kwa nia mbaya.
28Shahidi wa uongo ataangamia, bali anayesikiliza ataongea kwa muda wote.
29Mtu mwovu huufanya uso wake kuwa mgumu, bali mtu mwadilifu ni thabiti juu ya njia zake.
30Hakuna hekima, hakuna ufahamu, na hakuna shauri linaloweza kusimama kinyume na Yehova.
31Farasi hutayarishwa kwa siku ya mapigano, lakini ushindi hupatikana kwa Yehova.