Text copied!
CopyCompare
Biblia ya Kiswahili - Mithali

Mithali 24

Help us?
Click on verse(s) to share them!
1Usiwe na husuda kwa wenye ubaya, wala usitamani kuambatana nao,
2kwa sababu mioyo yao inapanga njama za vurugu na midomo ya huongea juu ya madhara.
3Kwa hekima nyumba hujengwa na kwa ufahamu huimarishwa.
4Kwa maarifa vyumba hujazwa vitu vyote vya thamani na utajiri wa kupendeza.
5Shujaa wa hekima ni imara, na mtu wa maarifa huongeza nguvu zake;
6maana kwa uongozi wa busara unaweza kufanya vita na kwa washauri wengi kuna ushindi.
7Hekima ipo juu sana kwa mpumbavu; hafumbui kinywa chake kwenye mlango.
8Kuna yule mwenye kupanga kufanya mabaya- watu wanamwita bwana wa njama.
9Mipango ya mpumbavu ni dhambi na watu humchukia mwenye dhihaka.
10Kama utakuwa dhaifu na mwenye kuogopa siku ya taabu, basi nguvu zako ni haba.
11Waokoe wanaochukuliwa kwenda kwenye mauti na uwashikilie wale wanaopepesuka kwenda kwa mchinjaji.
12Kama utasema, “Tazama, hatujui chochote juu ya hili,” je yule anayepima mioyo hajui unachosema? Na yule anayelinda maisha yako, je hajui? Je Mungu hatampa kila mmoja kile anachostahili?
13Mwanangu, kula asali kwa kuwa ni nzuri, kwa sababu matone ya sega la asali ni matamu unapoonja.
14Hekima ndiyo ilivyo katika nafsi yako - kama utaitafuta, tumaini lako halitabatilika na kutakuwa na tumaini.
15Usisubiri kwa kuvizia kama waovu ambao hushambulia nyumba ya mwenye haki. Usiiharibu nyumba yake!
16Maana mwenye haki huanguka mara saba na kuinuka tena, lakini waovu huangushwa kwa maafa.
17Usisherekee wakati adui yako anapoanguka na wala moyo wako usifurahi anapojikwaa,
18au Yehova ataona na kutoridhika na kuondoa ghadhabu juu yake.

19Usifadhaike kwa sababu ya watenda mabaya, na wala usiwahusudu watu waovu,
20maana mtu mbaya hana matumaini na taa ya watu waovu itazimika.
21Mwanangu; mche Yehova, na umwogope mfalme, usishirikiane na watu wenye kuasi dhidi yao,
22maana kwa ghafula msiba wao utakuja na ni nani ajuaye ukubwa wa uharibifu utakao kuja kutoka kwa hao wote?
23Haya ni maneno ya wenye busara pia. Upendeleo katika kuhukumu kesi kwa sheria si vizuri.
24Anayemwambia mwenye hatia, “Wewe upo sawa,” atalaaniwa na watu na mataifa yatamchukia.
25Bali wenye kuwakemea waovu watakuwa na furaha na zawadi za wema zitakuja kwao.
26Anayetoa jibu la kweli hutoa busu kwenye midomo.
27Andaa kazi yako ya nje, na tayarisha kila kitu kwa ajili yako mwenyewe shambani; baada ya hapo, jenga nyumba yako.
28Usitoe ushahidi dhidi ya jirani yako bila sababu na usidanganye kwa midomo yako.
29Usiseme, “Mimi nitamtendea kile alichonitendea; nitalipiza kwa kile alichofanya.”
30Nilikwenda jirani na shamba la mtu mvivu, nikapita kwenye shamba la mzabibu la mtu asiye na akili.
31Miiba imeota kila sehemu, ardhi ilikuwa imefunikwa kwa upupu, na ukuta wake wa mawe ulikuwa umebomoka.
32Kisha nikaliona na kufikiria juu yake; nikatazama na kupokea mafundisho.
33Kulala kidogo, kusinzia kidogo, kupumzika kwa kukunja mikono kidogo-
34na umasikini huja kwa kutembea juu yako, na mahitaji yako kama askari mwenye silaha.