1Mwanangu, zingatia hekima yangu; sikiliza kwa makini ufahamu wangu,
2ili ujifunze busara na midomo yako iweze kuhifadhi maarifa.
3Maana midomo ya malaya hutiririsha asali na kinywa chake ni laini kuliko mafuta,
4lakini mwishoni anakuwa mchungu kama mnyoo, hukata kama upunga mkali.
5Miguu yake huelekea mauti; hatua zake huelekea njia yote ya kuzimu.
6Hafikirii njia ya uzima. Hatua za miguu yake hupotea, maana hajui anakwenda wapi.
7Sasa, wanangu, nisikilizeni; wala msiache kusikiliza maneno ya kinywa changu.
8Lindeni njia yenu mbali naye wala msiende karibu na mlango wa nyumba yake.
9Kwa njia hiyo hamtawapa wengine heshima yenu au miaka ya uzima wenu kwa mtu mkatiri;
10wageni usije kufanya karamu kwa utajiri wenu; kazi mliyoifanya haitaenda katika nyumba ya wageni.
11Mwishoni mwa maisha yenu mtajuta ambapo nyama na mwili wenu vitaangamia.
12Nanyi mtasema, “Namna gani nilichukia fundisho na moyo wangu ulidharau sahihisho!
13Sikuweza kuwatii walimu wangu au kuwasikiliza walionielekeza.
14Nilikuwa nimeharibika kabisa katikati ya kusanyiko, miongoni mwa makutano ya watu.”
15Munywe maji kutoka kwenye birika lenu mwenyewe na munywe maji yanatiririka kutoka kwenye kisima chenu.
16Je inapaswa chemichemi yenu ifurike popote na mifereji yenu ya maji itiririke katika njia kuu?
17Yawe yenu wenyewe peke yenu wala si kwa wageni.
18Chemichemi yako ibarikiwe na umfurahie mke wa ujana wako.
19Maana ni ayala apendezaye na kulungu mwenye uzuri. Matiti yake na yakujaze furaha muda wote; daima na utekwe na upendo wake.
20Mwanangu, kwa nini uwe mateka wa malaya, kwa nini uyakumbatie matiti ya mwanamke mgeni?
21Yehova huona kila kitu afanyacho mtu na huangalia mapito yake yote.
22Mtu mwovu atatekwa na makosa yake mwenyewe; kamba za dhambi yake zitamnasa kwa nguvu.
23Atakufa kwa kukosa maonyo; atapotelea mbali kwa upumbavu wake wingi.