Text copied!
CopyCompare
Biblia ya Kiswahili - Mithali

Mithali 4

Help us?
Click on verse(s) to share them!
1Wanangu, sikilizeni, fundisho la baba, na zingatieni ili mjue maana ya ufahamu.
2Mimi ninawapa mafundisho mazuri; msiyaache mafundisho yangu.
3Mimi nilikuwa mwana kwa baba yangu, mpole na mtoto pekee kwa mama yangu,
4baba alinifundisha akiniambia, “Moyo wako uzingatie sana maneno yangu; shika amri zangu nawe uishi.
5Jipatie hekima na ufahamu; usisahau na kuyakataa maneno ya kinywa changu;
6usiiache hekima nayo itakulinda; ipenda nayo itakuhifadhi salama.
7Hekima ni kitu cha muhimu sana, hivyo jipatie hekima na tumia namna zote kuweza kupata ufahamu.
8Tunza hekima nayo itakutukuza; ikumbatie nayo itakuheshimu.
9Hekima itaweka kilemba cha heshima juu ya kichwa chako; itakupa taji zuri.
10Mwanangu, sikiliza, na kuzingatia maneno yangu, nawe utapata miaka mingi ya maisha yako.
11Ninakuelekeza katika njia ya hekima, nimekuongoza katika mapito yaliyonyooka.
12Unapotembea, hakuna atakayesimama katika njia yako na kama ukikimbia hutajikwaa.
13Shika mwongozo wala usiuache, utakuongoza, maana ni uzima wako.
14Usifuate njia ya waovu wala usiende katika njia ya watendao uovu.
15Jiepushe nayo, usipite katika njia hiyo; geuka na upite njia nyingine.
16Maana hawawezi kulala mpaka wafanye ubaya na hupotewa na usingizi hadi wasababishe mtu kujikwaa.
17Maana wao hula mkate wa uovu na hunywa divai ya vurugu.
18Bali njia ya mwenye kutenda haki ni kama mwanga ung'aao, huangaza zaidi na zaidi hadi mchana inapowasili kwa ukamilifu.

19Njia ya waovu ni kama giza - hawajui ni kitu gani huwa wanajikwaa juu yake.
20Mwanangu, zingatia maneno yangu; sikiliza kauli zangu.
21Usiziache zikaondoka machoni pako; uzitunze katika moyo wako.
22Maana maneno yangu ni uzima kwa wenye kuyapata na afya katika mwili wao.
23Ulinde salama moyo wako na uukinge kwa bidii zote; kwa kuwa katika moyo hububujika chemichemi za uzima.
24Jiepushe na kauli za udanganyifu na ujiepushe na mazungumzo ya ufisadi.
25Macho yako yatazame mbele kwa unyoofu na kwa uthabiti tazama mbele sawasawa.
26Usawazishe pito la mguu wako; na njia zako zote zitakuwa salama.
27Usigeuke upande wa kulia au kushoto; ondoa mguu wako mbali na uovu.