Text copied!
CopyCompare
Biblia Takatifu - Luka - Luka 3

Luka 3:3-19

Help us?
Click on verse(s) to share them!
3Basi, Yohane akaenda katika sehemu zote zilizopakana na mto Yordani, akihubiri watu watubu na kubatizwa ili Mungu awaondolee dhambi.
4Ndivyo ilivyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya: “Sauti ya mtu imesikika jangwani: Mtayarishieni Bwana njia yake; nyosheni mapito yake.
5Kila bonde litafukiwa, kila mlima na kilima vitasawazishwa; palipopindika patanyooshwa, njia mbaya zitatengenezwa.
6Na, watu wote watauona wokovu utokao kwa Mungu.”
7Basi, Yohane akawa anawaambia watu wengi waliofika ili awabatize: “Enyi kizazi cha nyoka! Ni nani aliyewadokezea kwamba mngeweza kuiepuka ghadhabu inayokuja?
8Basi, onyesheni kwa matendo kwamba mmetubu. Msianze sasa kusema: Sisi ni watoto wa Abrahamu. Nawaambieni hakika, Mungu anaweza kuyageuza mawe haya yawe watoto wa Abrahamu!
9Lakini, sasa hivi shoka limewekwa tayari kukata mizizi ya miti. Kila mti usiozaa matunda mazuri utakatwa na kutupwa motoni.”
10Umati wa watu ukamwuliza, “Tufanye nini basi?”
11Akawajibu, “Aliye na nguo mbili amgawie yule asiye na nguo; aliye na chakula afanye vivyo hivyo.”
12Nao watoza ushuru wakaja pia ili wabatizwe, wakamwuliza, “Mwalimu, tufanye nini?”
13Naye akawaambia, “Msitoze ushuru zaidi ya kima kilichowekwa.”
14Nao askari wakamwuliza, “Na sisi tufanye nini?” Naye akawajibu, “Msichukue vitu vya mtu yeyote kwa nguvu wala kumshtaki yeyote kwa uongo. Toshekeni na mishahara yenu.”
15Wote walikuwa wanatazamia kitu fulani; basi, wakaanza kujiuliza mioyoni mwao kuhusu Yohane: kuwa labda yeye ndiye Kristo.
16Hapo Yohane akawaambia wote, “Mimi ninawabatiza kwa maji, lakini anakuja mwenye uwezo zaidi kuliko mimi ambaye sistahili hata kumfungulia kamba za viatu vyake. Yeye atawabatizeni kwa Roho Mtakatifu na kwa moto.
17Yeye ni kama mtu anayeshika mikononi mwake chombo cha kupuria nafaka, aipure nafaka yake, akusanye ngano ghalani mwake, na makapi ayachome kwa moto usiozimika.”
18Hivyo, pamoja na mawaidha mengine mengi, Yohane aliwahimiza watu akiwahubiria Habari Njema.
19Lakini Yohane alimgombeza Herode, mkuu wa mkoa, kwa sababu alikuwa amemchukua Herodia, mke wa ndugu yake, na kumfanya mke wake; na pia kwa ajili ya mabaya yote aliyokuwa amefanya.

Read Luka 3Luka 3
Compare Luka 3:3-19Luka 3:3-19