Text copied!
CopyCompare
Biblia Takatifu - Luka - Luka 22

Luka 22:35-64

Help us?
Click on verse(s) to share them!
35Kisha, Yesu akawauliza wanafunzi wake, “Wakati nilipowatuma bila mfuko wa fedha wala mkoba wala viatu, mlitindikiwa chochote?” Wakajibu, “La.”
36Naye akawaambia, “Lakini sasa, yule aliye na mfuko wa fedha auchukue; na aliye na mkoba, hali kadhalika. Na yeyote asiye na upanga, auze koti lake anunue mmoja.
37Maana nawaambieni, haya maneno ya Maandiko Matakatifu: Aliwekwa kundi moja na wahalifu, ni lazima yatimie. Naam, yale yanayonihusu yanafikia ukamilifu wake.”
38Nao wakasema, “Bwana, tazama; hapa kuna panga mbili.” Naye akasema, “Basi!”
39Yesu akatoka, na kama ilivyokuwa desturi yake, akaenda katika mlima wa Mizeituni; wanafunzi wake wakamfuata.
40Alipofika huko akawaambia, “Salini, msije mkaingia katika kishawishi.”
41Kisha akawaacha, akaenda umbali wa mtu kuweza kutupa jiwe, akapiga magoti, akasali:
42“Baba, kama wapenda, ukiondoe kwangu kikombe hiki; hata hivyo, mapenzi yako yatimizwe, wala siyo yangu.”
43Hapo, malaika kutoka mbinguni, akamtokea ili kumtia moyo.
44Akiwa katika uchungu mkubwa, alisali kwa bidii zaidi; na jasho likamtoka, kama matone ya damu, likatiririka mpaka chini.
45Baada ya kusali, aliwarudia wanafunzi wake, akawakuta wamelala, kwani walikuwa na huzuni.
46Akawaambia, “Mbona mnalala? Amkeni msali, msije mkaingia katika kishawishi.”
47Alipokuwa bado anaongea, kundi la watu likaja likiongozwa na yule aliyeitwa Yuda, mmoja wa wale mitume kumi na wawili. Yuda akaenda kumsalimu Yesu kwa kumbusu.
48Lakini Yesu akamwambia, “Yuda! Je, unamsaliti Mwana wa Mtu kwa kumbusu?”
49Wale wanafunzi wake walipoona hayo wakasema, “Bwana, tutumie panga zetu?”
50Na mmoja wao akampiga upanga mtumishi wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio lake la kulia.
51Hapo, Yesu akasema, “Acha! Hii inatosha.” Akaligusa sikio la mtu huyo akaliponya.
52Kisha Yesu akawaambia makuhani wakuu, wakubwa wa walinzi wa Hekalu na wazee waliokuja kumkamata: “Je, mmekuja na mapanga na marungu kunikamata kana kwamba mimi ni mnyang'anyi?
53Nilipokuwa pamoja nanyi kila siku Hekaluni hamkunitia nguvuni. Lakini, huu ndio wakati wenu hasa, ndio wakati wa utawala wa giza.”
54Basi, wakamkamata, wakamchukua na kwenda naye nyumbani kwa Kuhani Mkuu. Petro akawa anamfuata nyuma kwa mbali.
55Moto ulikuwa umewashwa katikati ya ua, nao wakawa wameketi pamoja Petro akiwa miongoni mwao.
56Mjakazi mmoja alipomwona Petro ameketi karibu na moto, akamkodolea macho, akasema, “Mtu huyu alikuwa pia pamoja na Yesu.”
57Lakini Petro akakana akisema, “Wee! simjui mimi.”
58Baadaye kidogo, mtu mwingine akamwona Petro, akasema, “Wewe ni mmoja wao.” Lakini Petro akajibu “Bwana we; si mimi!”
59Kama saa moja baadaye, mtu mwingine akasisitiza, “Hakika huyu alikuwa pamoja naye; ametoka Galilaya ati.”
60Lakini Petro akasema, “Bwana wee; sijui hata unachosema!” Na papo hapo, akiwa bado anaongea, jogoo akawika.
61Bwana akageuka na kumtazama Petro, naye Petro akakumbuka yale aliyokuwa ameambiwa na Bwana: “Leo kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu.”
62Hapo akatoka nje, akalia sana.
63Wale watu waliokuwa wanamchunga Yesu, walimpiga na kumdhihaki.
64Walimfunga kitambaa usoni, wakawa wanamwuliza, “Ni nani aliyekupiga? Hebu bashiri tuone!”

Read Luka 22Luka 22
Compare Luka 22:35-64Luka 22:35-64