Text copied!
CopyCompare
Biblia ya Kiswahili - 2 Samweli

2 Samweli 22

Help us?
Click on verse(s) to share them!
1Daudi akamwimbia Yahwe maneno ya wimbo huu siku ile Yahwe alipomwokoa katika mkono wa adui zake wote na katika mkono wa Sauli.
2Akaomba hivi, “Yahwe ni mwamba wangu, ngome yangu, aliyeniokoa.
3Mungu ni mwamba wangu. Yeye ni kimbilio langu. Ngao yangu, pembe ya wokovu wangu, ngome yangu na kimbilio langu, aniokoaye na mabaya yote.
4Nitamwita Yahwe, astahiliye kutukuzwa, nami nitaokolewa kutoka kwa adui zangu.
5Maana mawimbi ya mauti yalinizunguka, mafuriko ya maji ya uharibifu yakanishinda.
6Vifungo vya kuzimu vilinizunguka; kamba za mauti zikaninasa.
7Katika shida yangu nalimwita Yahwe; nilimwita Mungu wangu; akaisikia sauti yangu katika hekalu lake, na kilio changu cha msaada kikafika masikioni mwake.
8Ndipo nchi ilipotikisika na kutetemeka. Misingi ya mbingu ikatetemeka na kutikiswa, kwa kuwa Mungu alikasirika.
9Moshi ukatoka katika pua yake, na miale ya moto ikatoka katika kinywa chake. Makaa yakawashwa nayo.
10Alizifungua mbingu akashuka, na giza totoro lilikuwa chini ya miguu yake.
11Alipanda juu ya kerubi na kuruka. Alionekana katika mawingu ya upepo.
12Naye akalifanya giza kuwa hema kumzunguka, akakusanya mawingu makubwa ya mvua angani.
13Makaa ya moto yalidondoka mbele zake kutoka katika radi.
14Yahwe alishuka kutoka katika mbingu. Aliyejuu alipiga kelele.
15Alipiga mishale na kuwatawanya adui zake—miale ya radi na kuwasambaratisha.
16Kisha njia za maji zikaonekana; misingi ya dunia ikawa wazi katika kilio cha vita ya Yahweh, katika sauti za pumzi ya pua zake.
17Kutoka juu alifika chini; akanishikilia! Aliniondoa katika vilindi vya maji.
18Aliniokoa kutoka kwa adui zangu wenye nguvu, kwao walionichukia, kwa maana walikuwa na nguvu sana kwangu.

19Walikuja kinyume changu siku ya shida yangu, lakini Yahwe alikuwa msaada wangu.
20Pia aliniweka mahali panapo nafasi. Aliniokoa kwa kuwa alipendezwa nami.
21Yahwe amenituza kwa kipimo cha haki yangu; amenirejesha kwa kiwango cha usafi wa mikono yangu.
22Kwa maana nimezishika njia za Yahwe na sijafanya uovu kwa kugeuka kutoka kwa Mungu.
23Kwa kuwa maagizo yake yote ya haki yamekuwa mbele yangu; kwa kuwa sheria zake, sikujiepusha nazo.
24Nimekuwa bila hatia mbele zake pia, na nimejiepusha na dhambi.
25Kwa hiyo Yahwe amenirejesha kwa kiasi cha uadilifu wangu, kwa kipimo cha usafi wangu mbele zake.
26Kwa mwaminifu, unajionesha kuwa mwaminifu; kwake asiye na hatia; unajionesha kuwa hauna hatia.
27Kwa usafi unajionesha kuwa msafi, lakini kwa wakaidi unajionesha kuwa mkaidi.
28Unaokoa walioteswa, lakini macho yako ni kinyume cha wenye kiburi, unawashusha chini.
29Kwa maana wewe ni taa yangu, Yahwe. Yahwe huangaza katika giza langu.
30Maana kwa ajili yake ninaweza kupita vipingamizi; kwa msaada wa Mungu wangu naweza kuruka juu ya ukuta.
31Maana njia za Mungu ni kamilifu. Neno la Yahwe ni safi. Yeye ni ngao yao wanaomkimbilia.
32Maana ni nani aliye Mungu isipokuwa Yahwe? Na ni nani aliyemwamba isipokuwa Mungu?
33Mungu ni kimbilio langu, na umwongoza katika njia yake mtu asiye na hatia.
34Huifanya myepesi miguu yangu kama kurungu na kuniweka katika vilima virefu.
35Huifundisha mikono yangu kwa vita, na viganja vyangu kupinda upinde wa shaba.
36Umenipa ngao ya wokovu wako, na matakwa yako yamenifanya mkuu.

37Umeitengenezea miguu yangu nafasi chini yangu, hivyo miguu yangu haikujikwaa.
38Niliwafuatia adui zangu na kuwaangamiza. Sikurudi nyuma hadi walipoangamizwa.
39Niliwararua na kuwasambaratisha; hawawezi kuinuka. Wameanguka chini ya miguu yangu.
40Unaweka nguvu ndani yangu kama mkanda kwa vita; unawaweka chini yangu wanaoinuka kinyume changu.
41Ulinipa migongo ya shingo za adui zangu; niliwaangamiza kabisa wale wanaonichukia.
42Walilia kwa msaada, lakini hakuna aliyewaokoa; walimlilia Yahwe, lakini hakuwajibu.
43Niliwaponda katika vipande kama mavumbi juu ya ardhi, niliwakanyaga kama matope mitaani.
44Umeniokoa pia kutoka katika mashutumu ya watu wangu. Umeniweka kama kichwa cha mataifa. Watu nisiowajua wananitumikia.
45Wageni walishurutishwa kuniinamia. Mara waliposikia kuhusu mimi, walinitii.
46Wageni walikuja wakitetemeka kutoka katika ngome zao.
47Yahwe anaishi! Mwamba wangu atukuzwe. Mungu na ainuliwe, mwamba wa wokovu wangu.
48Huyu ndiye Mungu anilipiaye kisasi, awawekaye watu chini yangu.
49Uniweka huru mbali na adui zangu. Hakika, uliniinua juu yao walioinuka kinyume changu. Uliniokoa kutoka kwa watu wenye ghasia.
50Kwa hiyo nitakushukuru, Yahwe, kati ya mataifa; nitaliimbia sifa jina lako.
51Mungu hutoa ushindi mkuu kwa mfalme wake, na uonesha uaminifu wake wa kiagano kwa mtiwa mafuta wake, kwa Daudi na uzao wake daima.”