Text copied!
CopyCompare
Biblia ya Kiswahili - 2 Samweli

2 Samweli 24

Help us?
Click on verse(s) to share them!
1Kisha hasira ya Yahwe ikawaka dhidi ya Israeli, naye akamchochea Daudi kinyume chao kusema, “Nenda, ukawahesabu Israeli na Yuda.”
2Mfalme akamwambia Yoabu, jemedari wa jeshi, aliyekuwa pamoja naye, “Nenda upite katika kabila zote za Israeli, toka Dani mpaka Beersheba, uwahesabu watu wote, ili niweze kujua idadi kamili ya watu wanaofaa kwa vita.”
3Yoabu akamwambia mfalme, “Yahwe Mungu wako na aizidishe hesabu ya watu mara mia, na macho ya bwana wangu mfalme yaone ikifanyika. Lakini kwa nini bwana wangu mfalme analitaka jambo hili?
4Walakini neno la mfalme lilikuwa la mwisho dhidi ya Yoabu na dhidhi ya majemedari wa jeshi. Hivyo Yoabu na majemedari wakatoka mbele ya mfalme kuwahesabu watu wa Israeli.
5Wakavuka Yordani na kupiga kambi karibu na Aroeri, kusini mwa mji bondeni. Kisha wakasafiri kupitia Gadi mpaka Yazeri.
6Wakaja Gileadi na nchi ya Tahtimu Hodshi, kisha Dani, Jaani na karibu kuelekea Sidoni.
7Wakafika ngome ya Tiro na miji yote ya Wahivi na Wakanaani. Kisha wakaenda Negebu katika Yuda huko Beersheba.
8Walipokuwa wamepita katika nchi yote, wakarejea Yerusalemu mwishoni mwa miezi tisa na siku ishirini.
9Ndipo Yoabu alipotoa taarifa ya hesabu kamili kwa mfalme kuhusu watu wawezao kupigana vita. Katika Israeli kulikuwa na watu 800, 000 jasiri wawezao kutoa upanga, na wale wa Yuda walikuwa watu 500, 000.
10Ndipo moyo wa Daudi ukamchoma alipokuwa amewahesabu watu. Hivyo akamwambia Yahwe, “Kwa kufanya hivi nimetenda dhambi sana. Sasa, Yahwe, uiondoe hatia ya mtumishi wako, kwani nimetenda kwa upumbavu.”
11Daudi alipoinuka asubuhi, neno la Yahwe likamjia nabii Gadi, mwonaji wa Daudi, kusema,
12Nenda umwambie Daudi; 'Hivi ndivyo asemavyo Yahwe: “Ninakupa mambo matatu. Uchague mojawapo.”
13Hivyo Gadi akaenda kwa Daudi na kumwambia, “Je miaka mitatu ya njaa ije katika nchi yako? au miezi mitatu ukimbie kutoka kwa adui zako huku wakikufuatia? au kuwe na tauni ya siku tatu katika nchi yako? Amua sasa jibu gani nimrudishie aliyenituma.”
14Ndipo Daudi alipomwambia Gadi, “Nipo katika shida kubwa. Haya na tuanguke katika mikono ya Yahwe kuliko kuanguka katika mikono ya mwanadamu, kwani matendo yake ya rehema ni makuu sana.”
15Hivyo akatuma tauni juu ya Israeli kuanzia asubuhi kwa muda ulioamriwa, na watu sabini na tano elfu kutoka Dani mpaka Beersheba wakafa.
16Malaika aliponyosha mkono wake kuelekea Yerusalemu ili kuuharibu, Yahwe akabadili nia yake kuhusu madhara, na akamwambia malaika aliyekuwa tiyari kuwaangamiza watu, “Yatosha! Rudisha mkono wako sasa.” Wakati huo malaika wa Yahwe alikuwa amesimama katika kiwanja cha kupuria cha Arauna Myebusi.
17Daudi alipomwona malaika aliyekuwa amewapiga watu, akamwambia Yahwe kusema, “Nimetenda dhambi, na nimetenda kwa upumbavu. Lakini kondoo hawa, wamefanya nini? Tafadhari, mkono wako na uniadhibu mimi na familia ya baba yangu!”
18Kisha Gadi akaja siku hiyo kwa Daudi na kumwambia, “Kwea na ujenge madhabahu kwa ajili ya Yahwe katika kiwanja cha kupuria cha Arauna Myebusi.”

19Hivyo Daudi akakwea kama Gadi alivyomwelekeza kufanya, kama Yahwe alivyokuwa ameagiza.
20Arauna akatazama na kumwona mfalme na watumishi wake wakikaribia. Ndipo Arauna akaondoka na kumsujudia mfalme uso wake mpaka juu ya ardhi.
21Kisha Arauna akasema, “Kwa nini bwana wangu mfalme amekuja kwangu, mtumishi wake? Daudi akajibu, “Kununua uwanja wako wa kupuria, ili nimjengee Yahwe madhabahu, ili kwamba tauni iondolewe kwa watu.”
22Arauna akamwambia Daudi, “Chukua liwe lako, bwana wangu mfalme. Ulifanyie lolote lolote lililojema machoni pako. Tazama, ng'ombe kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa na miganda ya kupuria na nira kwa kuni.
23Haya yote bwana wangu mfalme, mimi Arauna nakupa.” Kisha akamwambia mfalme, “Yahwe Mungu wako na awe nawe.”
24Mfalme akamwambia Arauna, “Hapana, nahimiza kukinunua kwa thamani yake. Sitatoa kama sadaka ya kuteketezwa kwa Yahwe chochote nisichokigharimia.” Hivyo Daudi akakinunua kiwanja cha kupuria na ng'ombe kwa shekeli hamsini za fedha.
25Daudi akajenga madhabahu kwa Yahwe pale na kutoa juu yake sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani. Hivyo wakamsihi Yahwe kwa niaba ya nchi, hivyo akaizuia tauni katika katika Israeli yote.