Text copied!
CopyCompare
Biblia ya Kiswahili - 2 Samweli

2 Samweli 20

Help us?
Click on verse(s) to share them!
1Ikatukia pia kuwa katika eneo lilelile kulikuwa mfanya fujo jina lake Sheba mwana wa Bikri Mbenjamini. Akapiga tarumbeta na kusema, “Sisi hatuna sehemu katika Daudi, wala hatuna urithi katika mwana wa Yese. Haya kila mtu na aende nyumbani kwake, Israeli.”
2Hivyo watu wote wa Israeli wakamwacha Daudi na kumfuata Sheba mwana wa Bikri. Lakini watu wa Yuda wakamfuata mfalme wao kwa karibu sana, kutoka Yordani njia yote hadi Yerusalemu.
3Daudi alipofika katika kasri lake huko Yerusalemu, akawachukua masuria aliokuwa amewaacha kulitunza kasri, na akawaweka katika nyumba chini ya uangalizi. Aliwaandalia mahitaji yao lakini hakulala nao tena. Hivyo walikuwa wametengwa hadi siku ya kufa kwao, waliishi kama wajane.
4Kisha mfalme akamwambia Amasa, “Uwaite watu wa Yuda ndani ya siku hizi tatu; wewe pia uwepo hapa.”
5Hivyo Amasa akaenda kuwaalika watu wote wa Yuda kwa pamoja, lakini akatumia muda mrefu kulika mfalme alivyokuwa amemwamuru.
6Hivyo Daudi akamwambia Abishai, “Sasa Sheba mwana wa Bikri atatufanyia madhara zaidi ya Absalomu. Chukua watumishi wa bwana wako, askari wangu, na umfuatie asije akaingia katika mji wenye ngome na kututoroka.”
7Ndipo watu wa Yoabu wakamfuatia, pamoja na Wakerethi na Wapelethi na mashujaa wote. Wakatoka Yerusalemu ili kumfuatia Sheba mwana wa Bikri.
8Walipokuwa katika jiwe kubwa lililoko Gibeoni, Amasa akaja kuwalaki. Yoabu alikuwa amevaa silaha ya vita aliyokuwa ameivaa, alikuwa pia na upanga uliokuwa umefungwa na mkanda katika kiuno chake. Kadili alivyoendelea mbele upanga ukadondoka.
9Hivyo Yoabu akamwambia Amasa, “Haujambo binamu yangu?” Kwa utaratibu Yoabu akakishika kidevu cha Amasa kwa mkono wake wa kulia ili ambusu.
10Amasa hakutambua kwamba kulikuwa na jambia katika mkono wa kushoto wa Yoabu. Yoabu akamchoma Amasa tumboni na matumbo yake yakadondoka chini. Wala Yoabu hakumpiga tena, na Amasa akafa. Hivyo Yoabu na Abishai nduguye wakamfuatia Sheba mwana wa Bikri.
11Kisha mmoja wa watu wa Yoabu akasimama kando ya Amasa naye akasema, “Aliye upande wa Yoabu na aliyeupande wa Daudi na amfuate Yoabu.”
12Amasa akawa anagalagala katika damu yake katikati ya njia. Mtu yule alipoona kwamba watu wote wamesimama, akambeba Amasa na kumweka shambani kando ya njia. Akatupa vazi juu yake kwa maana aliona kila mmoja aliyekuja alisimamaa pale.
13Baada ya Amasa kuondolewa njiani watu wote wakamfuata Yoabu katika kumfuatia Sheba mwana wa Bikri.
14Sheba akazipita kabila zote za Israeli mpaka Abeli wa Beth Maaka, na katika nchi yote ya Berite ambao pia walijikusanya pamoja pia na kumfuatia Sheba.
15Walimpata na kumzingira huko Abeli wa Bethi Maaka. Wakajenga buruji ya kuhusuru mji nyuma ya ukuta. Jeshi lote lilokuwa pamoja na Yoabu likaugongagonga ukuta ili uanguke.
16Ndipo mwanamke mwerevu akapiga kelele kutoka ndani ya mji, “Sikiliza, Yoabu, tafadhari sikiliza! Sogea karibu nami ili niongee nawe.”
17Hivyo Yoabu akakaribia, mwanamke akamwambia, “Je wewe ni Yoabu? Akajibu, “ni mimi.” mwanamke akamwambia, “Sikiliza maneno ya mtumishi wako.” Akajibu, “Nasikiliza.”
18Ndipo aliposema, “Hapo zamani ilisemwa, 'Bila shaka tafuteni ushauri huko Abeli,' na kwamba ushauri huo utakata maneno.

19Sisi ni mji ulio miongoni mwa miji yenye nguvu na aminifu sana katika Israeli. Mnataka kuharibu mji ambao ni mama katika Israeli. Kwa nini unataka kuumeza urithi wa Yahwe?”
20Ndipo Yoabu alipojibu na kusema, “Iwe mbali, iwe mbali nami, hata nikameze au kuharibu.
21Hiyo si kweli. Lakini mtu kutoka katika nchi ya milima ya Efraimu, aitwaye Sheba mwana wa Bikri, ameinua mkono wake kinyume cha mfalme, kinyume cha Daudi. Mtoeni yeye nami nitauacha mji.” Mwanamke akamwambia Yoabu, “Utarushiwa kichwa chake kutoka juu ya ukuta.”
22Kisha mwanamke akawaendea watu wote wa mji kwa hekima yake. Wakakiondoa kichwa cha Sheba mwana wa Bikri na kumrushia Yoabu. Ndipo alipopiga tarumbeta na watu wa Yoabu wakauacha mji kila mtu nyumbani kwake. Na Yoabu akarejea Yerusalemu kwa mfalme.
23Yoabu alikuwa juu ya jeshi lote la Israeli na Benaya mwana wa Yehoiada alikuwa juu ya Wakerethi na Wapelethi.
24Adoramu alikuwa juu ya watu waliofanya kazi ya shokoa na Yehoshafati mwana wa Ahiludi alikuwa mkumbushaji.
25Sheva alikuwa mwandishi, na Sadoki na Abiathari walikuwa makuhani.
26Ira wa Yairi alikuwa mhudumu mkuu wa Daudi.