Text copied!
CopyCompare
Biblia ya Kiswahili - 2 Samweli

2 Samweli 17

Help us?
Click on verse(s) to share them!
1Kisha Ahithofeli akamwambia Absalomu, “Niruhusu sasa nichague watu elfu kumi na mbili nami nitaondoka na kumfuatia Daudi usiku huu.
2Nitampata kwa ghafla wakati amechoka na dhaifu nami nitamstukiza kwa hofu. Watu waliopamoja naye watakimbia nami nitamshambulia mfalme peke yake.
3Nitawarejesha watu wote kwako kama bibi harusi ajavyo kwa bwana wake, na watu wote watakuwa katika amani chini yako.”
4Alichokisema Ahithofeli kikampendeza mfalme na wazee wote wa Israeli.
5Kisha Absalomu akasema, “Sasa mwiteni pia Hushai Mwarki ili tusikie yeye pia anasemavyo.”
6Hushai alipofika kwa Absalomu, Absalomu akamweleza kile ambacho Ahithofeli alikuwa amesema na kisha akamwuliza Hushai, “Je tufanye alivyosema Ahithofeli? Ikiwa hapana, tueleze kile unachoshauri.”
7Hivyo Hushai akamwambia Absalomu, “Ushauri aliotoa Ahithofeli siyo mzuri kwa wakati huu.”
8Hushai akaongeza, “Unamjua baba yako na kwamba watu wake ni mashujaa na kwa sasa wanauchungu, ni kama dubu aliyenyang'anywa watoto wake mwituni. Baba yako ni mtu wa vita; hatalala na jeshi usiku huu.
9Tazama, kwa wakati huu pengine amejificha katika shimo fulani au mahali pengine. Itakuwa kwamba baadhi ya watu wako watakapokuwa wameuawa mwanzoni mwa shambulio hata kila mtu atakayesikia atasema, mauaji yamefanyika kwa askari wanaomfuata Absalomu.'
10Kisha hata askari jasiri zaidi ambao moyo wao ni kama moyo wa simba, wataogopa kwa kuwa Israeli yote inajua kwamba baba yako ni mtu mwenye nguvu na kwamba watu alionao ni wenye nguvu sana.
11Hivyo ninashauri kwamba Israeli wote wakutanike kwako pamoja kutoka Dani hadi Beersheba, wengi kama mchanga ufuoni mwa bahari na kwamba wewe mwenyewe uende vitani.
12Kisha tutampata popote atakapokuwa nasi tutamfunika kama umande uangukavyo juu ya nchi. Hatutamwachia hata mmoja aliye hai kati ya watu wake wala yeye mwenyewe.
13Ikiwa ataingia ndani ya mji kisha Israeli wote tutaleta kamba juu ya mji huo na kuukokotea mtoni, hata kusionekane hata jiwe moja dogo lililosalia.”
14Kisha Absalomu na watu wa Israeli wakasema, “Shauri la Hushai Mwarki ni jema kuliko lile la Ahithofeli. Yahwe aliwafanya wakatae shauri jema la Ahithofeli ili kumwangamiza Absalomu.
15Kisha Hushai akawambia Sadoki na Abiathari makuhani, “Ahithofeli alimshauri Absalomu na wazee wa Israeli hivi na hivi, lakini mimi nimeshauri vinginevyo.
16Sasa basi, nendeni haraka na mmtaarifu Daudi kusema, 'Usipige kambi usiku huu katika vivuko vya Araba, lakini kwa namna yoyote vukeni, tofauti na hapo mfalme atamezwa pamoja na watu wote walio pamoja naye.”
17Yonathani na Ahimaasi walikuwako katika chemichemi za En Rogeli. Hivyo kijakazi mmoja alikuwa akienda na kuwapasha habari waliyopaswa kuifahamu, ili kwamba wasihatarishe maisha yao kwa kuonwa wakiingia mjini. Ujumbe ulipofika ndipo huenda na kumtaarifu mfalme Daudi.
18Lakini kijana mmoja akawaoni mara akamwambia Absalomu. Hivyo Yonathani na Ahimaasi wakaenda kwa haraka na wakaingia katika nyumba ya mtu mmoja huko Bahurimu, aliyekuwa na kisima katika ua wake wakaingia humo.

19Mke wa mtu huyo akachukua kifuniko na kukikufunika kwenye mlango wa kisima kisha akaanika nafaka juu yake, hivyo hakuna aliyejua kwamba Yonathani na Ahimaasi walikuwa kisimani.
20Watu wa Absalomu wakaja kwa mwanamke na kumwuliza, “Ahimaasi na Yonathani wako wapi?” Mwanamke akawaambia, “Wamevuka mto.” Hivyo baada ya kuwatafuta bila kuwaona kurejea Yerusalemu.
21Ikawa baada yao kuondoka Yonathani na Ahimaasi wakatoka ndani ya kisima. Wakaenda kumtaarifu mfalme Daudi; wakamwambia, “Inuka na uvuke maji haraka kwa maana Ahithofeli ametoa mashauri haya na haya juu yako.”
22Kisha Daudi akainuka pamoja na watu wote walikuwa pamoja naye, nao wakauvuka Yordani. Hata ilipofika alfajiri hakuna hata mmoja aliyesalia kwa kutouvuka Yordani.
23Ikawa Ahithofeli alipoona kwamba ushauri wake haukufuatwa, akapanda punda wake na kuondoka. Akaenda nyumbani katika mji wake mwenyewe, akaweka mambo yake katika utaratibu na kisha akajinyonga. Kwa hiyo akafa na kuzikwa katika kaburi la baba yake.
24Ndipo Daudi akaja Mahanaimu. Lakini Absalomu yeye akavuka Yordani yeye pamoja na watu wote wa Israeli waliokuwa pamoja naye.
25Absalomu alikuwa amemweka Amasa juu ya jeshi badala ya Yoabu. Naye huyo Amasa alikuwa mwana wa Yetheri Mwishmaeli, aliyekuwa amelala na Abigaili, aliyekuwa binti Nahashi na dada wa Seruya, mamaye Yoabu.
26Kisha Israeli na Absalomu wakapiga kambi katika nchi ya Gileadi.
27Ikawa wakati Daudi alipokuwa amekuja Mahanaimu, huyo Shobi mwana wa Nahashi kutoka Raba ya Waamoni na Makiri mwana wa Amieli wa kutoka Lo Debari, na Berzilai Mgileadi wa Rogelimu,
28wakaleta magodoro na mabulangeti, mabakuri na vyungu, na ngano, unga wa shayiri, nafaka zilizokaangwa, maharage, dengu,
29asali, siagi, kondoo na samli, ili kwamba Daudi na watu waliokuwa pamoja naye waweze kula. Kwani walisema, “Watu wana njaa, wamechoka na wana kiu huko nyikani.”