1Utakaposikiliza kwa makini sauti ya Yahwe Mungu wako ili kwamba ushikilie amri zake zote ambazo nakuamuru leo, Yahwe Mungu wako atakuweka juu ya mataifa yote ya ulimwengu.
2Baraka hizi zote zitakuja kwako na kukupita, kama utasikiliza sauti ya Yahwe Mungu wako.
3Utabarikiwa ndani ya mji, na utabarikiwa shambani.
4Matunda ya mwili wako yatabarikiwa, na matunda ya ardhi yako, na matunda ya wanyama wako, ongezeko la ng’ombe wako, na wachanga wa mifugo wako.
5Kitabarikiwa kikapu chako na chombo cha kukandia.
6Utabarikiwa utakaporudi ndani, na utabarikiwa utakapotoka nje.
7Yahwe atasababisha maadui zako wanaoinuka dhidi yako kupigwa chini mbele yako; watajitokeza dhidi yako kwa njia moja lakini watakimbia mbele zako kwa njia saba.
8Yahwe ataamuru baraka kuja kwako katika maghala yako na katika kila unapoweka mkono wako; atakubariki katika nchi anayokupatia.
9Yahwe atawaimarisha kama watu waliotengwa kwa ajili yake, kama alivyoapa kwenu, iwapo mtashikilia amri za Yahwe Mungu wenu, na kutembea katika njia zake.
10Watu wote wa ulimwengu wataona ya kwamba mmeitwa kwa jina la Yahwe, nao watawaogopa.
11Yahwe atakufanya kuwa na mafanikio sana katika matunda ya mwili wako, katika matunda ya ng’ombe zako, katika matunda ya ardhi yako, katika nchi aliyoapa kwa mababu zako kuwapatia.
12Yahwe atafungua kwako ghala lake la mbingu kuruhusu mvua juu ya ardhi katika muda sahihi, na kubariki kazi zote za mikono yako; utakopesha kwa mataifa mengi, lakini wewe hautakopa.
13Yahwe atakufanya kuwa kichwa, na sio mkia; utakuwa juu tu, na hautakuwa chini, iwapo utaisikiliza amri za Yahwe Mungu wako ambazo ninakuamuru leo, ili kuzishikilia na kuzitenda,
14na usipogeuka kinyume na maneno yoyote ninayokuamuru leo, kulia kwako wala kushoto kwako, na kufuata miungu mingine na kuwatumikia.
15Lakini usiposikiliza sauti ya Yahwe Mungu wako, na kushikilia amri zake zote na sheria zake ninazokuamuru leo, basi laana hizi zote zitakuja kwako na kukupita.
16Utalaaniwa utakapokuwa mjini, na utalaaniwa utakapokuwa shambani.
17Kitalaaniwa kikapu chako na chombo chako cha kukandia.
18Litalaaniwa tunda la mwili wako, tunda la ardhi yako, ongezeko la ng’ombe wako, na wachanga wa mifugo.
19Utalaaniwa utakaporudi, na utalaaniwa utokapo.
20Yahwe atatuma laana juu yako, kuchanganyikiwa, na shutuma katika kila jambo uwekalo mikono yako, hadi utakapoangamizwa, na hadi utakapotoweka haraka kwa sababu ya matendo yako maovu ambayo utakuwa umenitelekeza mimi.
21Yahwe atafanya pigo likung’ang’anie mpaka kukuangamiza kutoka katika nchi utakayoenda kumiliki.
22Yahwe atakushambulia kwa magonjwa ya kuambukiza, kwa homa, kwa uvimbe, na kwa kiangazi na jua kali, na kwa upepo mkali na ukungu. Hivi vitakufukuza hadi uangamie.
23Mbingu zilizo juu ya vichwa vyenu zitakuwa shaba, na ardhi chini yenu itakuwa chuma.
24Yahwe atafanya mvua ya ardhi yako kuwa unga na vumbi, kutoka mbinguni vitashuka kwako, hadi utakapoangamizwa.
25Yahwe atakusababishia upigwe mbele ya maadui zako; utawafuata kwa njia moja dhidi yao lakini utakimbia mbele zao kwa njia saba. Utapelekwa huku na kule miongoni mwa falme za nchi.
26Mzoga wako utakuwa chakula kwa ndege wote wa angani na kwa wanyama wa ulimwengu; hakutakuwa na mtu wa kuwatisha.
27Yahwe atawashambulia na majipu ya Misri na vidonda, kiseyeye na mwasho ambazo hautapona.
28Yahwe atakushambulia kwa ukichaa, kwa upofu, pamoja na kuchanganyikiwa kwa akili.
29Utapapasa papasa mchana kama kipofu apapasavyo usiku, na hautafanikiwa katika njia zako; daima utakandamizwa na kuporwa, na hakutakuwa na mtu wa kukuokoa.
30Utamchumbia mwanamke, lakini mwanamume mwingine atamkamata na kumbaka. Utajenga nyumba lakini hautaishi ndani mwake; utapanda shamba la mizabibu lakini hautafurahia matunda yake.
31Ng’ombe wako atachinjwa mbele ya macho yako, lakini hautakula nyama yake; punda wako atachukuliwa kwa nguvu mbele yako na hatarejeshwa kwako. Kondoo wako watapewa maadui zako, na hautakuwa na mtu wa kukusaidia.
32Watoto wa kiume na mabinti zako watapewa kwa watu wengine; macho yako yatawatafuta siku nzima, lakini yatashindwa kwa shauku juu yao. Hakutakuwa na nguvu mikononi mwako.
33Mavuno ya ardhi yako na ya kazi yako yote – taifa usilolijua litayatafuna; daima utaonewa na kugandamizwa,
34ili upatwe na wazimu kwa yale utakayoona yakitendeka.
35Yahwe atakushambulia kwenye magoti na miguu kwa majibu makali ambayo hutaweza kupona, kutoka chini ya miguu yako mpaka juu ya kichwa chako.
36Yahwe atawachukua pamoja na mfalme ambaye mtakuwa mmemuweka juu yenu kwa taifa ambalo hamjalijua, wala nyie au mababu zenu; kule mtaabudu miungu mingine ya mbao na mawe.
37Nawe utakuwa chanzo cha kitisho, mithali, na uvumi, miongoni mwa watu wote ambako Yahwe atakupeleka.
38Utaweka mbegu nyingi shambani, lakini utakusanya mbegu chache, kwa maana nzige itaziangamiza.
39Utapanda mashamba ya mizabibu na kuyapalilia, lakini hautakunywa divai yoyote, wala hautakusanya matunda yoyote, kwa maana funza watayala.
40Utakuwa na miti ya mizeituni katika eneo lako, lakini hautajipaka mafuta yoyote juu yako, kwa maana mti wako wa mzeituni utaangusha matunda yake.
41Utakuwa na wana wa kiume na mabinti, lakini hawatabaki kuwa wako, kwani watachukuliwa mateka.
42Miti yako yote na matunda ya ardhi yako – nzige watajitwalia.
43Mgeni aliye miongoni mwako atainuka juu zaidi yako juu na juu; wewe mwenyewe utashuka chini na chini.
44Atakukopesha, lakini hautamkopesha; atakuwa kichwa, nawe utakuwa mkia.
45Laana hizi zote zitakujia juu yako na kukuandama na kukupita hadi utakapoangamizwa. Hii itatokea kwa sababu haukuisikia sauti ya Yahwe Mungu wako, ili kushikilia amri na maagizo yake aliyokuamuru.
46Laana hizi zitakuwa juu yako kama ishara na miujiza, na juu ya uzao wako milele.
47Kwa sababu hukumuabudu Yahwe Mungu wako kwa shangwe na furaha moyoni mwako ulipokuwa na mafanikio,
48kwa hiyo utatumikia maadui ambao Yahwe atatuma dhidi yako; utawatumikia katika njaa, katika kiu, katika uchi, na katika umaskini. Ataweka mzigo wa chuma juu ya shingo yako hadi akuangamize.
49Yahwe ataleta taifa dhidi yako kutoka mbali, kutoka mwisho wa ulimwengu, kama tai arukaye kwa mhanga wake, taifa ambalo lugha yake hauelewi;
50taifa lenye sura katili ambalo haliheshimu wazee na halionyeshi fadhila kwa wadogo.
51Watakula wachanga wa ng’ombe wako na matunda ya ardhi yako hadi utakapoangamizwa. Hawatawaachia nafaka, divai mpya, au mafuta, wachanga wa ng’ombe au mifugo yako, hadi watakaposababisha kutoweka kwako.
52Watawazingira katika malango ya miji yenu, hadi kuta zenu ndefu na imara zitakaposhuka chini ardhini, kuta ambazo mliziamini. Watawazingira ndani ya malango ya miji yenu kotekote katika nchi ambayo Yahwe Mungu wenu amewapatia.
53Utakula tunda la mwili wako mwenyewe, nyama ya watoto wa kiume na binti zako, ambao Yahwe Mungu wako aliwapatia, katika uvamizi na katika dhiki ambayo adui zako wataweka juu yako.
54Mwanamume laini na mlegevu miongoni mwenu – atakuwa na wivu kwa kaka yake na kwa mkewe, na kwa watoto wowote waliosalia.
55Kwa hiyo hatawapatia kati yao nyama ya watoto wake ambayo ataenda kuila, kwa sababu hatabakiwa na chochote katika uvamizi na dhiki ambayo adui yako ataiweka juu yako ndani ya malango yote ya mji wako.
56Mwanamke laini na mlegevu miongoni mwenu, ambaye hatadiriki kuweka tako la mguu wake ardhini kwa sababu ya ulaini na maringo yake – atakuwa na wivu kwa mume kipenzi wake mwenyewe, kwa mtoto wake wa kiume, na kwa binti yake,
57na kwa mtoto wake mchanga atakayetoka katikati ya miguu yake, na kwa watoto atakayewazaa. Atawala kwa siri kwa kukosa kitu kingine, katika uvamizi na dhiki ambayo adui yako ataweka juu yako ndani ya malango ya mji wako.
58Iwapo hautashika maneno yote ya sheria yaliyoandikwa katika kitabu hiki, ili kuheshimu jina hili tukufu na la kutisha, Yahwe Mungu wako,
59basi Yahwe atafanya mapigo yako kuwa ya kutisha, na yale ya wazao wako; yatakuwa mapigo makuu, ya muda mrefu, na magonjwa makali, ya muda mrefu.
60Ataleta juu yako mara nyingine magonjwa yote ya Misri ambayo ulikuwa unayaogopa; yatakung’ang’ania.
61Pia kila gonjwa na pigo ambalo halijaandikwa katika kitabu cha sheria hii, hayo pia Yahwe atayaleta juu yako hadi utakapoangamizwa.
62Utabaki wachache kwa idadi, ingawa ulikuwa kama nyota wa mbinguni kwa idadi, kwa sababu haukuisikiliza sauti ya Yawhe Mungu wako.
63Kama vile hapo awali Yawhe alivyofurahia juu yako na kutenda mema, na kuwazidisha, basi atafurahia juu yako kwa kufanya upotee na kwa kukuangamiza. Utang’olewa katika nchi utakayoenda kuimiliki.
64Yahwe atakusambaza miongoni mwa watu wote kutoka mwisho mmoja wa dunia hadi mwisho mwingine wa dunia; huko utaabudu miungu mingine ambayo hujawajua, wewe wala mababu zako, miungu ya mbao na jiwe.
65Miongoni mwa mataifa haya hautapata utulivu, na hakutakuwa na pumziko chini ya miguu yako; badala yake, Yahwe atakupatia huko moyo wa kutetemeka, macho yanayofeli na nafsi inayoomboleza.
66Maisha yako yataning’inia kwa mashaka mbele yako; utaogopa kila usiku na mchana na hutakuwa na uhakika kabisa maishani mwako.
67Asubuhi utasema, “Natamani ingekuwa jioni!” na jioni utasema, “Natamani ingekuwa asubuhi!” kwa sababu ya hofu mioyoni mwenu na vitu ambavyo macho yako italazimu kuona.
68Yahwe atakuleta Misri mara nyingine kwa meli, kwa njia ambayo nilikuambia, “Hutaiona Misri tena”. Kule utajitoa kuuzwa kwa maadui zako kama watumwa wa kiume na kike, lakini hakutakuwa na mtu wa kuwanunua.