1Musa aliondoka kutoka nyanda za Moabu mpaka mlima wa Nebo, hadi kilele cha Pisga, kilicho mkabala na Yericho. Huko Yahwe alimwonyesha nchi yote ya Gileadi kutoka umbali wa Dani,
2na Naftali yote, na nchi ya Efraimu na Manase, na nchi yote ya Yuda, mpaka bahari ya magharibi,
3na Negevi, na uwanda wa bonde la Yericho, mji wa mitende, mpaka umbali wa Soari.
4Yahwe alimwambia, “Hii ni nchi niliyoapa kwa Abrahamu, kwa Isaka, na kwa Yakobo, na kusema, “Nitawapatia uzao wako.” Nimekuruhusu uitazame kwa macho yako, lakini hautakwenda kule.”
5Basi Musa mtumishi wa Yahwe, alikufa pale katika nchi ya Moabu, kama neno la Yahwe lilivyoahidi.
6Yahwe alimzika katika bonde katika nchi ya Moabu mkabala na Beth-peori, lakini hakuna ajuaye kaburi lake lilipo hadi leo hii.
7Musa alikuwa na umri wa miaka mia moja na ishirini alipokufa; macho yake hayakufifia, wala nguvu asili zake hazikupungua.
8Watu wa Israeli walimuomboleza Musa katika nyanda za Moabu kwa siku thelathini, hapo ndipo siku za maombolezo ya Musa zilipotimia.
9Yoshua mwana wa Nuni alikuwa amejawa na roho ya hekima, kwa maana Musa alimwekea mkono juu yake. Watu wa Israeli walimsikiliza na kufanya yale ambayo Yahwe alimuamuru Musa.
10Tangu hapo hakujatokea nabii katika Israeli kama Musa, ambaye Yahwe alimjua uso kwa uso.
11Hakujawahi kuwa na nabii yeyote kama yeye kwa ishara na miujiza ambayo Yahwe alimtuma kufanya katika nchi ya Misri, kwa Farao, na kwa watumishi wake, na kwa nchi yake yote.
12Hakujawahi kuwa na nabii yeyote kama yeye kwa mambo yote makubwa, ya kutisha ambayo Musa aliyafanya machoni pa Israeli yote.