1Hautakiwi kumtazama ng’ombe au kondoo wa Muisraeli mwenzako akikosea njia na ukajificha kwao; hakika unapaswa kuwarejesha kwake.
2Iwapo Muisraeli mwenzako hayupo karibu nawe, au kama haumfahamu, basi unapaswa kumleta mnyama huyo nyumbani kwako, na lazima uwe naye mpaka pale mwenyewe atakapomtafuta, na kisha lazima umrejeshee mwenyewe.
3Unapaswa kufanya vivyo hivyo kwa punda wake; unapaswa kufanya vivyo hivyo na vazi lake; unapaswa kufanya vivyo hivyo kwa kila kitu alichopoteza Muisraeli mwenzako, kitu chochote alichopoteza na ukakipata; hautakiwi kujificha.
4Haupaswi kumwona punda wa Muisraeli mwenzako au ng’ombe wake kaanguka chini barabarani na kujificha dhidi yao; hakika unapaswa kumsaidia kumwinua tena.
5Mwanamke hatakiwi kuvaa kinachokusudiwa kwa mwanamume, vilevile mwanamume hapaswi kuvaa mavazi ya mwanamke; kwa maana yeyote afanyaye vitu hivi ni chukizo kwa Yahwe Mungu wako.
6Iwapo kiota cha ndege kikaonekana barabarani mbele yako, kwenye mti wowote au juu ya ardhi, kikiwa na makinda ya ndege au mayai ndani mwake, na mama yao akiwa juu yao au juu ya mayai, haupaswi kumchukua mama pamoja na makinda au mayai yake.
7Hakika unapaswa kumuacha mama aende zake, ila makinda yake unaweza kuyachukua. Tii amri hii ili uenende vyema, na siku zako ziweze kurefushwa.
8Ujengapo nyumba mpya, basi unapaswa kujenga kitalu kwa ajili ya paa yako ili usilete damu juu ya nyumba yako mtu akianguka kutoka pale.
9Haupaswi kupanda shamba lako la mizabibu kwa mbegu mbili, ili kwamba mavuno yote yasichukuliwe na sehemu takatifu, mbegu uliyoipanda pamoja na matunda ya mzabibu.
10Haupaswi kulimia ng’ombe na punda kwa pamoja.
11Haupaswi kuvaa kitambaa kilichotengenezwa kwa sufu na kitani kwa pamoja.
12Unapaswa kutengeneza pindo katika pembe nne za nguo unayoivaa.
13Iwapo mwanamume kachukua mke, kisha kalala naye, na baadae kumchukia,
14na kisha kumtuhumu kwa vitu vya aibu na kumharibia sifa yake kwa kusema, “Nilimchukua huyu mwanamke, lakini nilipomkaribia sikukuta ushahidi waubikra kwake”.
15Kisha baba na mama mzazi wa binti wanatakiwa kupeleka ushahidi wa ubikra wake kwa wazee mlangoni mwa mji.
16Baba wa binti anapaswa kuwaambia wazee, “nilimpatia binti yangu kwa mwanamume huyu awe mkewe, naye anamchukia.
17Tazama, amemtuhumu na vitu vya aibu na kusema, “Sikukuta ushahidi wa ubikra kwa binti yako”. Lakini ushahidi huu hapa wa ubikra wa binti yangu”. Kisha watatandaza shuka mbele ya wazee wa mji.
18Wazee wa mji wanapaswa kumchukua mwanamume huyo na kumuadhibu;
19nao wanapaswa kumtoza faini ya shekeli mia moja ya fedha, na kumpatia baba wa binti, kwa sababu mwanamume kasababisha sifa mbaya kwa bikra wa Israeli. Binti huyu anapaswa kuwa mke wake; mwanamume huyu hatakiwi kumfukuza katika siku zake zote.
20Ila kama jambo hili ni la kweli, kwamba ushahidi wa bikra ya binti haukupatikana,
21basi wanapaswa kumpeleka binti mlangoni kwa baba yake, na kisha wanamume wa mji wake wanatakiwa kumpiga kwa mawe hadi afe, kwa sababu amefanya jambo la aibu katika Israeli, kwa kutenda kama kahaba chini ya nyumba ya baba yake, nanyi mtakuwa mmeondoa uovu miongoni mwenu.
22Iwapo mwanamume kakutwa analala na mwanamke ambaye ni mke wa mtu, basi wote wanapaswa kufa, mwanamume aliyelala na mwanamke pamoja na mwanamke mwenyewe; nanyi mtakuwa mmeondoa uovu miongoni mwenu.
23Iwapo kuna msichana bikra, ambaye amechumbiwa na mwanamume, kisha mwanamume mwingine kamkuta mjini na kulala naye,
24wachukueni wote wawili malangoni mwa mji, na kuwapiga mawe. Unapaswa kumpiga msichana mawe, kwa sababu hakupaza sauti kuomba msaada, ingawa alikuwa ndani ya mji. Unapaswa kumpiga mwanamume mawe, kwa sababu amemwingilia mke wa jirani yake; nanyi mtakuwa mmeondoa uovu miongoni mwenu
25Lakini kama mwanamume amemkuta msichana aliyechumbiwa shambani, na kama akamkamata na kulala naye, basi mwanamume pekee aliyelala naye ndiye lazima afe.
26Lakini kwake msichana msifanye chochote; hakuna dhambi inayostahili kifo kwake msichana. Kwa maana suala hili ni kama mwanamume amshambuliapo jirani yake na kumuua.
27Kwa maana alimkuta shambani; msichana huyu aliyechumbiwa alipaza sauti, lakini hapakuwa na mtu wa kumuokoa.
28Iwapo mwanamume amemkuta msichana ambaye ni bikra lakini hajachumbiwa, na kama akamkamata na kulala naye, na kama wakagundulika,
29basi mwanamume aliyelala naye lazima atoe shekeli hamsini za fedha kwa baba wa msichana, naye lazima awe mke wake, kwa sababu amemdhalilisha. Hatakiwi kumfukuza katika siku zake zote.
30Mwanamume hapaswi kumchukua mke wa baba yake kama wake; hatakiwi kuchukua haki za ndoa za baba yake.