Text copied!
CopyCompare
Biblia ya Kiswahili - Torati

Torati 21

Help us?
Click on verse(s) to share them!
1Iwapo mtu amekutwa kauwawa ndani ya nchi ambayo Yahwe Mungu wako anawapatia kumiliki, kalala shambani, na haijulikani aliyemshambulia;
2basi wazee wenu pamoja na waamuzi wenu wanapaswa kutoka nje, na kupima katika miji ambayo inamzunguka yule aliyeuawa.
3Kisha wazee wa mji ulio karibu na mwili wa marehemu wanapaswa kuchukua mtamba kutoka kwenye kundi la mifugo, ambaye hajawahi kutumikishwa, wala kubebeshwa nira.
4Kisha wanapaswa kumuongoza mtamba huyo mpaka chini ya bonde litiririkalo maji, bonde ambalo halijawahi kulimwa wala kupandwa, na mle bondeni wanapaswa kuvunja shingo ya mtamba huyo.
5Makuhani, uzao wa Lawi, wanapaswa kuja mbele, kwa maana Yahwe Mungu wako amewachagua wamtumikie yeye na kutoa baraka katika jina la Yahwe na kuamua kila mtafaruku na ugomvi kwa neno lao.
6Wazee wote wa mji ulio karibu na mtu aliyeuawa wanapaswa kunawa mikono yao juu ya mtamba aliyevunjwa shingo bondeni;
7na wanapaswa kutoa suhulisho juu ya jambo hilo na kusema, ‘Mikono yetu haijamwaga damu hii, wala macho yetu hayajaona suala hili.
8Tusamehe watu wako Israeli, Yahwe, ambao umewakomboa, na usiweke hatia juu ya umwagaji damu usio na kosa miongoni mwa watu wako Israeli.’ Kisha umwagaji damu utasamehewa kwao.
9Kwa njia hii utaweka mbali umwagaji damu usio na hatia miongoni mwenu, mtakapofanya yaliyo mema machoni pa YAHWE.
10Utakapokwenda kupigana vita dhidi ya maadui zako na Yahwe Mungu wako atakapokupa ushindi na kuwaweka chini ya mamlaka yako, na ukawachukua mbali kuwa mateka,
11kama kati ya mateka ukamwona mwanamke mzuri, nawe ukamtamani na kutaka kujitwalia awe mke wako,
12basi utamleta nyumbani kwako; atanyoa nywele zake na kukata kucha zake.
13Kisha atazivua nguo alizokuwa amezivaa wakati alipochukuliwa mateka na atabaki nyumbani kwako na kuwaomboleza baba yake na mama yake kwa mwezi mzima. Baada ya hapo unaweza kulala naye na kuwa mume wake, naye atakuwa mke wako.
14Lakini usipofurahishwa naye, basi unatakiwa kumruhusu aondoke apendaye yeye. Lakini haupaswi kamwe kumuuza kwa fedha, pia haupaswi kumfanya kama mtumwa, kwa sababu umemdhalilisha.
15Iwapo mwanamume ana wake wawili na mmoja wao ampenda na mwingine kumchukia, na wote wamekwisha mzalia watoto –wote mwanamke mpendwa na mwanamke achukiwae –
16basi katika siku ambayo mwanamume atakapowarithisha mali zake wanawe, hapaswi kumfanya mwana wa mke ampendaye kuwa mzawa wa kwanza kabla ya mwana wa mke amchukiaye, ambaye ndiye mwana wa kwanza.
17Badala yake, anapaswa kumtambua mwana wa kwanza, mwana wa mke asiyempenda, kwa kumpatia mara mbili ya mali zake; kwa maana huyo mwana ni mwanzo wa nguvu zake; haki za mzawa wa kwanza ni zake.
18Iwapo mwanamume ana mwana mkaidi na muasi ambaye hatatii sauti ya baba yake au sauti ya mama yake, ambaye, hata baada ya kurekebishwa, hatawasikia;

19basi baba yake na mama yake wanapaswa kumshika na kumleta mbele ya wazee wa mji na kwenye malango ya mji.
20Wanapaswa kuwaambia wazee wa mji, “Huyu mwanetu ni mkaidi na muasi; hataki kusikia sauti zetu; ni mwasherati na pia ni mlevi’.
21Kisha wanaume wote wa mji wanapaswa kumpiga kwa mawe hadi kufa; nanyi mtaondoa uovu miongoni mwenu. Israeli yote itasikia juu ya hili na kuogopa.
22Iwapo mwanamume kafanya dhambi inayostahili kifo na kisha akauwawa, kwa kunyongwa juu ya mti,
23basi mwili wake haupaswi kubaki usiku kucha juu ya mti. Badala yake, unapaswa kuhakikisha unamzika siku hiyo; kwa maana yeyote anyongwaye amekwisha laaniwa na Mungu. Tii amri hii ili kwamba usitie najisi nchi ambayo Yahwe Mungu wako anawapatia kama urithi.