1Walipokuwa wanakaribia Yerusalemu walifika Bethfage na Bethania, karibu na mlima wa Mizeituni. Hapo aliwatuma wawili wa wanafunzi wake,
2akawaambia, “Nendeni katika kijiji kilicho mbele yenu. Mtakapokuwa mnaingia humo, mtakuta mwana punda amefungwa ambaye bado hajatumiwa na mtu. Mfungueni mkamlete.
3Kama mtu akiwauliza, Mbona mnafanya hivyo? Mwambieni, Bwana anamhitaji na atamrudisha hapa mara.”
4Basi, wakaenda, wakamkuta mwana punda barabarani amefungwa mlangoni. Walipokuwa wakimfungua,
5baadhi ya watu waliokuwa wamesimama hapo wakawauliza “Kwa nini mnamfungua huyo mwana punda?”
6Wanafunzi wakajibu kama Yesu alivyokuwa amewaambia; nao wakawaacha waende zao.
7Wakampelekea Yesu huyo mwana punda. Wakatandika mavazi yao juu ya huyo mwana punda, na Yesu akaketi juu yake.
8Watu wengi wakatandaza mavazi yao barabarani; wengine wakatandaza matawi ya miti waliyoyakata mashambani.
9Watu wote waliotangulia na wale waliofuata wakapaaza sauti zao wakisema, “Hosana! Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Bwana!
10Ubarikiwe Ufalme ujao wa baba yetu Daudi. Hosana juu mbinguni!”
11Yesu aliingia mjini Yerusalemu akaenda moja kwa moja mpaka Hekaluni, akatazama kila kitu kwa makini. Lakini kwa vile ilikwisha kuwa jioni, akaenda Bethania pamoja na wale kumi na wawili.
12Kesho yake, walipokuwa wanatoka Bethania, Yesu aliona njaa.
13Basi, akaona kwa mbali mtini wenye majani mengi. Akauendea ili aone kama ulikuwa na tunda lolote. Alipoufikia, aliukuta bila tunda lolote ila majani matupu, kwa vile hayakuwa majira ya mtini kuzaa matunda.
14Hapo akauambia mtini, “Tangu leo hata milele mtu yeyote asile matunda kwako.” Nao wanafunzi wake walisikia maneno hayo.
15Basi, wakafika Yerusalemu. Yesu akaingia Hekaluni, akaanza kuwafukuza nje watu waliokuwa wanauza na kununua vitu humo ndani. Akazipindua meza za wale waliokuwa wakibadilishana fedha na viti vya wale waliokuwa wakiuza njiwa.
16Hakumruhusu mtu yeyote kupitia Hekaluni akichukua kitu.
17Kisha akawafundisha, “Imeandikwa: Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa ajili ya mataifa yote! Lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang'anyi!”
18Makuhani wakuu na walimu wa Sheria waliposikia hayo, walianza kutafuta njia ya kumwangamiza. Lakini walimwogopa kwa sababu umati wa watu ulishangazwa na mafundisho yake.
19Ilipokuwa jioni, Yesu na wanafunzi wake waliondoka mjini.
20Asubuhi na mapema, walipokuwa wanapita, waliuona ule mtini umenyauka wote, hata mizizi.
21Petro aliukumbuka, akamwambia Yesu, “Mwalimu, tazama! Ule mtini ulioulaani, umenyauka!”
22Yesu akawaambia, “Mwaminini Mungu.
23Nawaambieni kweli, mtu akiuambia mlima huu: Ng'oka ukajitose baharini bila kuona shaka moyoni mwake, ila akaamini kwamba mambo yote anayosema yanafanyika, atafanyiwa jambo hilo.
24Kwa hiyo nawaambieni, mnaposali na kuomba kitu, aminini kwamba mmekipokea, nanyi mtapewa.
25Mnaposimama kusali, sameheni kila mtu aliyewakosea chochote, ili Baba yenu aliye mbinguni awasamehe ninyi makosa yenu.
26Lakini msipowasamehe wengine, hata Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu.”
27Basi, wakafika tena Yerusalemu. Yesu alipokuwa akitembea Hekaluni, makuhani wakuu, walimu wa Sheria na wazee walimwendea,
28wakamwuliza, “Unafanya mambo haya kwa mamlaka gani? Nani aliyekupa mamlaka ya kufanya mambo haya?”
29Lakini Yesu akawaambia, “Nitawaulizeni swali moja; mkinijibu, na pia nitawaambieni ni kwa mamlaka gani ninafanya mambo haya.
30Je, mamlaka ya Yohane ya kubatiza yalitoka mbinguni ama kwa watu? Nijibuni.”
31Wakaanza kujadiliana, “Tukisema, Yalitoka mbinguni, atatuuliza, Basi, mbona hamkumsadiki?
32Na tukisema, Yalitoka kwa watu...” (Waliogopa umati wa watu maana wote waliamini kwamba Yohane alikuwa kweli nabii.)
33Basi, wakamjibu Yesu, “Sisi hatujui.” Naye Yesu akawaambia, “Nami pia sitawaambieni ninafanya mambo haya kwa mamlaka gani.”