1Samweli akamwambia Sauli, “BWANA alinituma nikutie mafuta uwe mfalme wa watu wake Israeli. Basi sikiliza maneno ya BWANA.
2Hivi ndivyo BWANA wa majeshi asemavyo, 'Nilichunguza jinsi Amaleki alivyomfanyia Israeli kwa kuwapinga njiani, walipopanda kutoka Misri.
3Sasa nenda umshambulie Amaleki na ukaangamize kabisa vitu vyote walivyo navyo. Usiwaache, ua wote mwanamme na mwanamke, mtoto na mtoto mchanga, ng'ombe na kondoo, ngamia na punda.”'
4Sauli akwaita watu na kuwahesabu katika mji wa Talemu: watu mia mbili elfu waendao kwa miguu, na watu elfu kumi kutoka Yuda.
5Kisha Sauli akaja hadi mji wa Amaleki akangoja huko bondeni.
6Ndipo Sauli akawaambia Wakeni, “Nendeni, muondoke, mkajitenge na Waamaleki, nisije kuwaangamiza pamoja nao. Kwa maana ulionesha wema kwa watu wote wa Israeli, walipotoka Misri.” Kwa hiyo Wakeni wakajitenga na Waamaleki.
7Kisha sauli akawashambulia Waamaleki, kutoka Havila hadi kufika Shuri, ulio mashariki mwa Misri.
8Basi akamchukua Agagi mfalme wa Waamaleki akiwa hai; aliwaangamiza kabisa watu wote kwa ncha ya upanga.
9Lakini Sauli na watu wake wakamwacha Agagi akiwa hai, pamoja na kondoo wazuri, ng'ombe, ndama wanono, na wanakondoo. Kila kitu kilichokuwa kizuri, hawakukiangamiza. Bali waliangamiza kabisa chochote kilichodharaulika na kisicho na thamani.
10Baadaye neno la BWANA likamjia Samweli, kusema,
11“Inanihuzunisha kwamba nimemchagua Samweli awe mfalme, kwa maana aligeuka nyuma asinifuate na hakutekeleza maagizo yangu.” Samweli alikasirika; akamlilia BWANA usiku kucha.
12Samweli aliamka mapema akutane na Sauli wakati wa asubuhi. Samweli aliambiwa, “Sauli alifika Karmeli na amejijengea ukumbusho kwa ajili yake, kisha aligeuka na kuendelea chini hadi Gilgali.” Ndipo
13Samweli akamwendea Sauli, na Sauli akamwambia, “Umebarikiwa na BWANA! Nami nimetekeleza amri ya BWANA.”
14Samweli akasema, “Hicho kilio cha kondoo ni cha nini basi masikioni mwangu, na hiyo milio ya ng'ombe ninayosikia?
15Sauli akamjibu, “Wao wamewaleta kutoka kwa Waamaleki. Kwa sababu watu waliwaacha hai kondoo wazuri na ng'ombe, kwa ajili ya sadaka kwa BWANA Mungu wako. Zilizobaki tuliziangamiza kabisa.”
16Ndipo Samweli akamwambia Sauli, “Subiri nitakumbia kile ambacho BWANA amekisema kwangu usiku.” Sauli akamwambia, “Sema!”
17Samweli akasema, “Ingawa wewe ni mdogo machoni pako mwenyewe, je, hukufanywa mkuu wa kabila za Israeli? Na BWANA akakutia mafuta uwe mfalme juu ya Israeli;
18BWANA alikutuma katika safari yako akisema, 'nenda na uangamize kabisa wenye dhambi, Waamaleki, na upigane dhidi yao hadi wameangamizwa.'
19Kwa nini basi haukuitii sauti ya BWANA, bali badala yake ulishikilia nyara na ukafanya uovu machoni pa BWANA?”
20Ndipo Sauli akamwambia Samweli, “Kweli kabisa niliitii sauti ya BWANA, Na nimeifuata njia ambayo BWANA alinituma. Nimemteka Agagi, mfalme wa Waamaleki, na kuwaangamiza kabisa Waamaleki.
21Lakini watu walichukua baadhi ya nyara-kondoo na ng'ombe, na vitu vizuri vilivyokusudiwa kuangamizwa, ili wavitoe dhabihu kwa BWANA, Mungu wako, huko Gilgali.”
22Samweli akajibu, “Je, BWANA hufurahia sadaka za kuteketezwa na dhabihu kama ilivyo kuitii sauti yake? Utii ni bora kuliko dhabihu, na kusikia ni bora kuliko mafuta ya beberu.
23Kwa maana uasi ni sawa na dhambi ya uchawi, na ukaidi ni sawa na uovu na udhalimu. Kwa kuwa umelikataa neno la BWANA, naye pia amekukataa usiwe mfalme.”
24Ndipo Sauli akamwambia Samweli, “Nimetenda dhambi; kwa maana nimevunja amri ya BWANA na maneno yako, kwa sababu niliwaogopa watu na kuitii sauti yao.
25Sasa, tafadhali nisamehe dhambi yangu, na urudi nami ili nipate kumcha BWANA.”
26Samweli akamwambia Sauli, “Sitarudi pamoja na wewe; kwa sababu umekataa neno la BWANA, naye BWANA amekukataa usiwe mfalme juu ya Israeli.”
27Samweli alipogeuka kuondoka, Sauli akashika pindo la kanzu yake, na likachanika.
28Samweli akamwambia, “BWANA ameuchana ufalme wa Israeli kutoka kwako leo na amempa ufalme huo jirani yako, aliye bora kuliko wewe.
29Pia, yeye ni Uwezo wa Israeli hatasema uongo wala kubadili nia yake; kwa sababu si mwanadamu, kwamba abadili nia yake.”
30Kisha Sauli akasema, “Nimetenda dhambi. Lakini tafadhali nipe heshima wakati huu mbele ya wakuu wa watu wangu na mbele ya Israeli. Urudi tena pamoja nami, kusudi niweze kumcha BWANA, Mungu wako.”
31Hivyo Samweli akamrudia tena Sauli, na Sauli akamcha BWANA.
32Kisha Samweli akasema, “Mmlete hapa kwangu Agagi mfalme wa Waamaleki.” Agagi akafika kwake akiwa amefungwa minyororo na kusema, “Hakika uchungu wa kifo umepita.”
33Naye Samweli akamjibu, “Jinsi upanga wako ulivyofanya wanawake wapoteze watoto, vivyo hivyo mama yako naye hatakuwa na mtoto miongoni mwa wanawake.” Kisha Samweli akamkata Agagi vipande vipande mbele za BWANA huko Gilgali.
34Samweli akaenda Rama, na Sauli akapanda kwenda nyumbani kwake Gibea ya Sauli.
35Samweli hakumuona tena Sauli hadi siku ya kifo chake, lakini alimwombolezea Sauli. Na BWANA alijuta kwa kumfanya Sauli awe mfalme juu ya Israeli.