1Ni kwa sababu Kristo alitupa uhuru ili tuwe huru. Hivyo, simameni imara wala msinaswe tena katika kongwa la utumwa.
2Tazama, Mimi Paulo, ninawaambia kwamba ikiwa mtatahiriwa, Kristo hatawafaidia kwa njia yoyote ile.
3Tena, namshuhudia kila mwanaume aliyetahiriwa kwamba anapaswa kuwajibika kwa sheria yote.
4Mmetengwa mbali na Kristo, wale wote “mnaohesabiwa haki” kwa sheria. Mmeanguka mbali na neema.
5Maana kwa njia ya Roho, kwa imani tunasubiri ujasiri wa haki.
6Katika Kristo Yesu kutahiriwa au kutokutahiriwa hakuna maana yoyote. Ni imani pekee inayofanya kazi kupitia upendo ndiyo humaanisha kitu.
7Mlikuwa mnapiga mbio vizuri. Nani aliwazuia kutokuitii kweli?
8Ushawishi wa kufanya hivyo hautoki kwake yeye anayewaita ninyi.
9Chachu kidogo huathiri donge zima.
10Nina matumaini na ninyi katika Bwana kwamba hamtafikiri kwa njia nyingine yoyote. Yeyote yule atakayewapotosha atabeba hukumu yake yeye mwenyewe, yeyote yule.
11Ndugu, kama naendelea kutangaza tohara, kwanini bado ninateswa? Kwa suala hilo kile ambacho ni kizuizi cha msalaba kitaweza kuharibiwa.
12Ni matakwa yangu kuwa wale wanaowaongoza vibaya watajihasi wenyewe.
13Mungu amewaiteni ninyi, ndugu, kwenye uhuru. Ila msiutumie uhuru wenu kama fursa kwa mwili. Badala yake kwa upendo mhudumiane ninyi kwa ninyi.
14Kwa kuwa sheria yote imekamilika katika amri moja; nayo ni “Ni lazima umpende jirani yako kama wewe mwenyewe.”
15Lakini kama mkiumana na kulana, jiangalieni kwamba msijiharibu ninyi kwa ninyi.
16Nasema, tembeeni kwa roho, na wala hamtazitimiza tamaa za mwili.
17Kwa kuwa mwili una tamaa kubwa dhidi ya Roho, na Roho ina tamaa kubwa dhidi ya mwili. Hizi zinapingana kila moja na nyingine. Matokeo ni kwamba hamfanyi vitu mnavyotamani kuvifanya.
18Lakini kama Roho anawaongoza ninyi, hamko chini ya sheria.
19Sasa matendo ya mwili yanaonekana. Nayo ni uasherati, uchafu, ufisadi,
20ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, husuda, kuwaka hasira, ushindani, faraka, mgawanyiko wa madhehebu,
21wivu, ulevi, ulafi na mambo mengine kama haya. Nawaonya ninyi, kama nilivyowaonya mwanzoni, kwamba wale wanaofanya mambo kama hayo hawataurithi ufalme wa Mungu.
22Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, ukarimu, utu wema, imani,
23upole, na kiasi. Hakuna sheria dhidi ya mambo kama hayo.
24Wale walio wa Kristo Yesu wameusulubisha mwili pamoja na shauku na tamaa zao mbaya.
25Kama tukiishi kwa Roho, pia tutembee kwa Roho.
26Tusiwe wa kujivuna, tusichokozane kila mmoja na mwenzake, wala tusioneane wivu.