Text copied!
CopyCompare
Biblia ya Kiswahili - Wagalatia

Wagalatia 4

Help us?
Click on verse(s) to share them!
1Ninasema kwamba maadamu mrithi ni mtoto, hana tofauti na mtumwa, hata ingawa ni mmiliki wa mali yote.
2Badala yake, yuko chini ya waangalizi na wadhamini mpaka wakati uliowekwa na baba yake.
3Kadhalika pia na sisi, tulipokuwa watoto, tulishikiliwa katika utumwa wa kanuni za kwanza za ulimwengu.
4Lakini wakati sahihi ulipofika, Mungu alimtuma mwanawe, mzaliwa wa mwanamke, mzaliwa chini ya sheria.
5Alifanya hivi ili kuwakomboa wale waliokuwa chini ya sheria, ili kwamba tupokee hali ya kuwa kama wana.
6Kwa sababu ninyi ni wana, Mungu alimtuma Roho wa mwanawe ndani ya mioyo yetu, Roho aitaye, “Abba, Baba.”
7Kwa sababu hii wewe si mtumwa tena bali mwana. Kama ni mwana, basi wewe pia ni mrithi kupitia Mungu.
8Hata kabla, wakati hamkumjua Mungu, mlikuwa watumwa kwa wale ambao kwa asili si miungu kabisa.
9Lakini sasa kwamba mnamjua Mungu, au kwamba mnajulikana na Mungu, kwa nini mnarudi tena kwenye kanuni dhaifu za kwanza na zisizo za thamani? Je mnataka kuwa watumwa tena?
10Mnashika kwa uangalifu siku maalumu, miandamo ya miezi, majira, na miaka. Ninaogopa kwa ajili yenu.
11Ninaogopa kwamba kwa namna fulani nimejitaabisha bure.
12Ninawasihi, ndugu, muwe kama nilivyo, kwa kuwa pia nimekuwa kama mlivyo. Hamkunikosea.
13Bali mnajua kwamba ilikuwa ni kwa sababu ya ugonjwa wa mwili kwamba nilihubiri injili kwenu kwa mara ya kwanza.
14Ingawa hali yangu ya mwili iliwaweka katika jaribu, hamkunidharau au kunikataa. Badala yake mlinipokea kama malaika wa Mungu, kana kwamba nilikuwa Kristo Yesu mwenyewe.
15Kwa hiyo, iko wapi sasa furaha yenu? kwa kuwa ninashuhudia kwenu kwamba, ikiwezekana, mungelin'goa macho yenu na kunipa mimi.
16Hivyo sasa, je nimekuwa adui yenu kwa sababu ninawaambia ukweli?
17Wanawatafuta kwa shauku, bali si kwa mema. Wanataka kuwatenganisha ninyi na mimi ili muwafuate.
18Ni vyema daima kuwa na shauku kwa sababu zilizo njema, na si tu wakati ninapokuwa pamoja nanyi.

19Wanangu wadogo, ninaumwa uchungu kwa ajili yenu tena mpaka Kristo aumbike ndani yenu.
20Ningependa kuwepo pale pamoja nanyi sasa na kugeuza sauti yangu, kwa sababu ninamashaka juu yenu.
21Niambieni, ninyi ambao mnatamani kuwa chini ya sheria, hamsikii sheria isemavyo?
22Kwa kuwa imeandikwa kwamba Abrahamu alikuwa na wana wa kiume wawili, mmoja kwa yule mwanamke mtumwa na mwingine kwa mwanamke huru.
23Hata hivyo, yule wa mtumwa alizaliwa kwa mwili tu, bali yule wa mwanamke huru alizaliwa kwa ahadi.
24Mambo haya yanaweza kuelezwa kwa kutumia mfano, kwa kuwa wanawake hawa wanafanana na maagano mawili. Mojawapo kutoka katika mlima Sinai. Huzaa watoto ambao ni watumwa. huyu ni Hajiri.
25Sasa Hajiri ni mlima Sinai ulioko Arabuni. Hufananishwa na Yerusalem ya sasa, kwa kuwa ni mtumwa pamoja na watoto wake.
26Bali Yerusalemu ambayo iko juu ni huru, na hii ndiyo mama yetu.
27Kwa kuwa imeandikwa, “Furahi, wewe mwanamke uliye tasa, wewe usiye zaa. Paza sauti na upige kelele kwa furaha, wewe ambaye huna uzoefu wa kuzaa. kwa maana wengi ni watoto wa aliye tasa, zaidi ya wale wa yule ambaye ana mume.”
28Sasa ndugu, kama Isaka, ninyi ni watoto wa ahadi.
29Kwa wakati ule ambao mtu ambaye alizaliwa kwa mujibu wa mwili alimtesa yule aliyezaliwa kwa mujibu wa Roho. Kwa sasa ni vilevile.
30Maandiko husemaje? “Muondoe mwanamke mtumwa pamoja na mwanawe wa kiume. Kwa kuwa mtoto wa mwanamke mtumwa hatarithi pamoja na mtoto wa mwanamke huru.”
31Kwa hiyo, ndugu, sisi si watoto wa mwanamke mtumwa, bali ni wa mwanamke huru.