1Bora mtu masikini ambaye huenenda katika uadilifu wake kuliko mwenye ukaidi katika maneno yake na ni mpumbavu.
2Tena, si vizuri kuwa na hamu bila maarifa na mwenye kukimbia haraka sana hukosea njia.
3Upuuzi wa mtu unaharibu maisha yake na moyo wake hughadhabika dhidi ya Yehova.
4Utajiri huongeza marafiki wengi, bali mtu masikini hutengwa na rafiki zake.
5Shahidi wa uongo hatakosa adhabu na mwenye kupumua uongo hataokoka.
6Wengi wataomba fadhila kutoka kwa mtu mkarimu na kila mtu ni rafiki wa yule anayetoa zawadi.
7Mtu masikini huchukiwa na ndugu zake wote; je marafiki wengi kiasi gani hujitenga kutoka kwake! Anawaita, lakini wameondoka.
8Anayepata hekima huyapenda maisha yake mwenyewe; yeye atunzaye ufahamu atapata kilicho chema.
9Shahidi wa uongo hatakosa kuadhibiwa, bali mwenye kupumua uongo ataangamia.
10Haifai kwa mpumbavu kuishi kwa anasa- wala kwa mtumwa kutawala juu ya wafalme.
11Busara humfanya mtu achelewe kukasirika na utukufu wake ni kusamehe kosa.
12Ghadhabu ya mfalme ni kama muungurumo wa simba kijana, bali fadhila yake ni kama umande kwenye majani.
13Mwana mpumbavu ni uharibifu kwa baba yake na mke mgomvi ni maji yanayochuruzika daima.
14Nyumba na utajiri ni urithi kutoka kwa wazazi, bali mke mwenye busara hutoka kwa Yehova.
15Uvivu unamtupa mtu kwenye usingizi mzito, bali asiyetamani kufanya kazi atakwenda njaa.
16Yeye anayetii amri huyaongoza maisha yake, bali mtu asiyefikiri juu ya njia zake atakufa.
17Mwenye ukarimu kwa masikini humkopesha Yehova na atalipwa kwa kile alichofanya.
18Mrudi mwanao wakati kuna matumaini na usiwe na shauku ya kumweka katika mauti.
19Mtu mwenye hasira kali lazima alipe adhabu; kama ukimwokoa, utafanya hivyo mara mbili.
20Sikiliza ushauri na ukubali maelekezo, ili uweze kuwa na hekima mwishoni mwa maisha yako.
21Moyoni mwa mtu kuna mipango mingi, bali kusudi la Yehova ndilo litakalo simama.
22Shauku ya mtu ni uaminifu na mtu masikini ni bora kuliko muongo.
23Kumheshimu Yehova huwaelekeza watu kwenye uzima; mwenye nayo atashibishwa na hatadhurika kwa madhara.
24Mtu goigoi huuzika mkono wake ndani ya dishi; hataurudisha juu ya kinywa chake.
25Kama utampiga mwenye mzaha, wajinga watakuwa na hekima; mwelekeze mwenye ufahamu, naye atapata maarifa.
26Anayempora baba yake na kumfukuza mama yake ni mwana anayeleta aibu na shutuma.
27Mwanangu, kama utaacha kusikiliza maelekezo, utapotea kutoka kwenye maneno ya maarifa.
28Shahidi mpotofu huidhihaki haki na kinywa cha waovu humeza uovu.