Text copied!
CopyCompare
Biblia Takatifu - Luka - Luka 24

Luka 24:27-51

Help us?
Click on verse(s) to share them!
27Akawafafanulia mambo yote yaliyomhusu yeye katika Maandiko Matakatifu kuanzia Mose hadi manabii wote.
28Walipokikaribia kile kijiji walikokuwa wanakwenda, Yesu akafanya kana kwamba anaendelea na safari;
29lakini wao wakamsihi wakisema, “Kaa pamoja nasi, maana kunakuchwa, na usiku unakaribia.” Basi, akaingia kijijini, akakaa pamoja nao.
30Alipoketi kula chakula pamoja nao, akachukua mkate, akaubariki, akaumega, akawapa.
31Mara macho yao yakafumbuliwa, wakamtambua; lakini yeye akatoweka kati yao.
32Basi, wakaambiana, “Je, mioyo yetu haikuwa inawaka ndani yetu wakati alipokuwa anatufafanulia Maandiko Matakatifu kule njiani?”
33Wakaondoka saa ileile, wakarudi Yerusalemu: wakawakuta wale mitume kumi na mmoja na wale wengine waliokuwa pamoja nao, wamekusanyika
34wakisema, “Hakika Bwana amefufuka, amemtokea Simoni.”
35Basi, hao wafuasi wawili wakawajulisha yale yaliyowapata njiani, na jinsi walivyomtambua katika kumega mkate.
36Wanafunzi wote wawili walipokuwa wakiwaambia hayo, Yesu mwenyewe akasimama kati yao, akawaambia “Amani kwenu.”
37Wakashtuka na kushikwa na hofu wakidhani wameona mzimu.
38Lakini yeye akawaambia, “Kwa nini mnafadhaika? Mbona mnakuwa na mashaka mioyoni mwenu?
39Angalieni mikono na miguu yangu, ya kwamba ni mimi mwenyewe. Nipapaseni mkanione, maana mzimu hauna mwili na mifupa kama mnionavyo.”
40Baada ya kusema hayo, akawaonyesha mikono na miguu.
41Wakiwa bado katika hali ya kutosadiki kwa sababu ya furaha yao, na wakiwa wanastaajabu, akawauliza, “Mnacho chakula chochote hapa?”
42Wakampa kipande cha samaki wa kuokwa.
43Akakichukua, akala, wote wakimwona.
44Halafu akawaambia, “Hii ndiyo maana ya maneno niliyowaambia nilipokuwa pamoja nanyi: kwamba ilikuwa lazima kukamilisha yote yaliyoandikwa juu yangu katika Sheria ya Mose na katika vitabu vya manabii na katika kitabu cha Zaburi.”
45Kisha, akaziangazia akili zao ili wapate kuelewa Maandiko Matakatifu.
46Akawaambia, “Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na siku ya tatu atafufuka kutoka wafu,
47na kwamba ni lazima, kwa jina lake, mataifa yote kuanzia na Yerusalemu yahubiriwe juu ya kutubu na kusamehewa dhambi.
48Ninyi ni mashahidi wa mambo hayo.
49Nami mwenyewe nitawapelekeeni yule ambaye Baba aliahidi kumtuma, lakini ngojeni huku mjini mpaka mtakapopewa ile nguvu itokayo juu.”
50Kisha akawaongoza nje ya mji hadi Bethania, akainua mikono yake juu, akawabariki.
51Alipokuwa anawabariki, akawaacha; akachukuliwa mbinguni.

Read Luka 24Luka 24
Compare Luka 24:27-51Luka 24:27-51