1Na Mwanakondoo alipouvunja mhuri wa saba, kukawa kimya mbinguni kwa muda wa nusu saa.
2Kisha nikawaona wale malaika saba wanaosimama mbele ya Mungu wamepewa tarumbeta saba.
3Malaika mwingine akafika, akiwa anachukua chetezo cha dhahabu, akasimama mbele ya madhabahu ya kufukizia ubani. Naye akapewa ubani mwingi autoe sadaka pamoja na sala za watu wote wa Mungu, juu ya madhabahu ya dhahabu iliyo mbele ya kiti cha enzi.
4Moshi wa ubani ukapanda juu, pamoja na sala za watu wa Mungu, kutoka mikononi mwake huyo malaika aliyekuwa mbele ya Mungu.
5Kisha malaika akakichukua hicho chetezo, akakijaza moto wa madhabahuni akakitupa duniani. Kukawa na ngurumo, sauti, umeme na tetemeko la ardhi.
6Kisha wale malaika saba wenye tarumbeta saba wakajiweka tayari kupiga mbiu ya mgambo.
7Malaika wa kwanza akapiga tarumbeta yake. Mchanganyiko wa mvua ya mawe na moto, pamoja na damu, ukamwagwa juu ya nchi. Theluthi moja ya nchi ikaungua, theluthi moja ya miti ikaungua, na majani yote mabichi yakaungua.
8Malaika wa pili akapiga tarumbeta yake. Na kitu kama mlima mkubwa unaowaka moto ukatupwa baharini. Theluthi moja ya bahari ikawa damu,
9theluthi moja ya viumbe vya baharini vikafa na theluthi moja ya meli zikaharibiwa.
10Kisha malaika wa tatu akapiga tarumbeta yake. Na nyota kubwa ikiwaka kama bonge la moto, ikaanguka kutoka mbinguni, na kutua juu ya theluthi moja ya mito na chemchemi za maji.
11(Nyota hiyo inaitwa “Uchungu.”) Basi, theluthi moja ya maji yakawa machungu; watu wengi wakafa kutokana na maji hayo, kwa sababu yaligeuka kuwa machungu.
12Kisha malaika wa nne akapiga tarumbeta yake. Ndipo theluthi moja ya jua, ya mwezi na ya nyota ikapata pigo; hata mwangaza ukapoteza theluthi moja ya mng'ao wake. Theluthi moja ya mchana ikakosa mwanga, hali kadhalika na theluthi moja ya usiku.
13Kisha nikatazama, nikasikia tai akiruka juu kabisa angani anasema kwa sauti kubwa, “Ole, ole, ole kwa wanaoishi duniani wakati malaika watatu waliobaki watakapopiga tarumbeta zao!”