1Sasa ilitokea baada ya kufa kwa Musa, mtumishi wa Yahweh, Yahweh alimwambia Yoshua, mwana wa Nuni, msaidizi mkuu wa Musa, kusema,
2“Musa, mtumishi wangu amekufa. Sasa basi inuka, vuka mto huu wa Yordani, wewe na watu hawa wote, kuingia katika nchi ambayo ninawapa - watu waisraeli.
3Nimewapa ninyi kila sehemu ambapo nyayo za miguu yenu itakanyaga. Nimewapa ninyi, kama nilivyomwahidi Musa.
4kuanzia jangwani na Lebanoni, hadi mto mkubwa wa Frati, nchi yote ya Wahiti, na hata Bahari kuu, ambako jua huzama, itakuwa nchi yenu.
5Hakuna mtu awaye yote atakayeweza kusimama kinyume chako siku zote za maisha yako. Nitakuwa pamoja nawe kama nilivyokuwa na Musa. Sitakupungukia wala kukuacha.
6Uwe hodari na jasiri. Wewe utawafanya watu hawa wairithi nchi ambayo niliwaahidi baba zao kuwa ningewapa.
7Uwe hodari na jasiri sana. uwe makini kutii sheria zote ambazo Musa mtumishi wangu alikuagiza. Usikengeuke upande wa kulia au wa kushoto, ili uweze kufanikiwa kila mahali utakapoenda.
8Siku zote uuongee juu ya kitabu hiki cha sheria. Utakitafakari mchana na usiku ili kwamba uweze kutii yote yaliyoandikwa humo. Kisha utastawi na kufanikiwa.
9Je si mimi niliyekuagiza? Uwe hadori na jasiri! Usiogope. Usivunjike moyo. Yahweh Mungu wako yuko pamoja nawe kila uendeko.
10Kisha Yoshua akawaagiza viongozi wa watu,
11“Nendeni katika kambi na waagizeni watu, 'andaeni chakula kwa ajili yenu. Baada ya siku tatu mtavuka mto huu wa Yordani na kuingia ndani na kuimiliki nchi ambayo Yahweh Mungu wenu awapeni ninyi ili kuimiliki.””
12Yoshua akawaambia Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase,
13“Kumbukeni maneno ambayo Musa, mtumishi wa Yahweh, aliwaaagiza aliposema, 'Yahweh Mungu wenu awapeni ninyi pumziko, naye awapeni ninyi nchi hii.'
14Wake zenu, na watoto wenu na mifugo yenu itakaa katika nchi ambayo Musa aliwapa ninyi ng'ambo ya Yordani. Lakini watu wenu wa vita wataenda pamoja na ndugu zao na kuwasaidia.
15Mpaka hapo Yahweh atakapowapa ndugu zenu pumziko kama alivyowapa ninyi. Na wao pia watamiliki nchi ambayo Yahweh Mungu wenu awapeni ninyi. Kisha mtarudi katika nchi yenu na kuimiliki, nchi ambayo Musa mtumishi wa Yahweh aliwapa ninyi ng'ambo ya Yordani, mahali pa mapambazuko ya jua.”
16Nao wakamjibu Yoshua, na kusema, “Mambo yote uliyotuagiza tutayafanya, na kila mahali utakapotutuma tutaenda.
17Tutakutii kama tulivyomtii Musa. Yahweh Mungu wako na awe pamoja nawe tu kama aliyokuwa pamoja na Musa.
18Yeyote anayeasi maagizo yako na kutotii maneno yako atauawa. Uwe hodari na jasiri tu.