Text copied!
CopyCompare
Biblia ya Kiswahili - Yoshua

Yoshua 24

Help us?
Click on verse(s) to share them!
1Kisha Yoshua aliyakusanya pamoja makabila yote ya Israeli huko Shekemu na aliwaita wazee wa Israeli, viongozi, waamuzi na maafisa wao, nao wakajihudhurisha mbele za Mungu.
2Yoshua akawaambia watu wote, “Hiki ndicho Yahweh, Mungu wa Israeli anachokisema, 'Mababu zenu kwa miaka mingi iliyopita waliishi ng'ambo ya mto Frati - Tera, baba wa Ibrahimu na baba wa Nahori - nao waliabudu miungu mingine.
3Lakini nilimchukua baba yenu kutoka ng'ambo ya Frati na nikamwongoza mpaka katika nchi ya Kanaani, na nilimpa watoto wengi kupitia kwa Isaka mwanaye.
4Na Isaka nikampa Yakobo na Esau. Nilimpa Esau nchi ya milima ya Seiri ili aimiliki, lakini Yakobo na watoto wake walishuka kwenda Misri.
5Nilimtuma Musa na Haruni, na niliwapiga Wamisri kwa mapigo. Baada ya hapo, niliwatoa ninyi.
6Niliwatoa baba zenu nje ya nchi ya Misri, nanyi mkafika hata katika bahari. Wamisri waliwafuata kwa magari na wapanda farasi hata katika bahari ya matete.
7Na baba zenu walipomwita Yahweh, aliweka giza kati yenu na Wamisri. Aliileta bahari ije juu yao na kuwafunika. Mliona yale niliyoyakifanya huko Misri. Kisha mliishi jangwaani kwa muda mrefu.
8Niliwaleta katika nchi wa Waamori, ambao waliishi katika upande mwingine mwa Yordani. Walipigana nanyi, nami niliwatia katika mkono wenu. Mliimiliki nchi yao, nami niliwaangamiza mbele yenu.
9Kisha Balaki mwana wa Zipori, mfalme wa Moabu, aliinuka na kuishambulia Israeli. Alimwita na kumtuma Baalamu mwana wa Beori, ili kuwalaani ninyi.
10Lakini sikumsikiliza Balaamu. Kwa hakika, aliwabarikia ninyi. Basi, niliwaokoa na mkono wake.
11Mlivuka Yordani na mkafika Yeriko. Viongozi wa Yeriko waliinuka wapigane nanyi, pamoja na Waamori, Waperizi, Wakanaani, Wahiti, Wagirgashi, Wahivi na Wayebusi. Niliwapa ninyi ushindi dhidi yao na niliwaweka chini ya mamlaka yenu.
12Nilituma manyingu mbele yenu, ambayo yaliwafukuzia mbali na wafalme wawili wa Waamori watoke mbele yenu. Haikutokea kwa sababu ya upanga wenu wala kwa upinde wenu.
13Niliwapeni ninyi nchi ambayo hamkuifanyia kazi na miji ambayo hamkuijenga, na sasa mnaishi ndani yake. Mnakula matunda ya mizabibu na na mashamba ya mizeituni ambayo hamkuyapanda'.
14Basi sasa mcheni Yahweh na kumwabudu yeye kwa uadilifu na uaminifu wote; jitengeni na miungu ambayo baba zenu waliiabudu ng'ambo ya Frati na katika Misri, na mkamwabudu Yahweh.
15Na kama inaonekana kuwa ni vibaya machoni penu kumwabudu Yahweh, chagueni ninyi katika siku hii ya leo ni nani mtakayemtumikia, kama ni miungu ambayo baba zenu waliiabudu ng'ambo ya Frati, au miungu ya Waamori, ambao ninyi mnakaa ndani ya nchi yao. Lakini kwangu mimi na nyumba yangu, tutumwabudu Yahweh.”
16Watu walijibu na kusema, “Hatutaweza kumwacha Yahweh na kuitumikia miungu mingine,
17kwa kuwa ni Yahweh Mungu wetu ambaye alitutoa sisi na baba zetu kutoka katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa, na ambaye alifanya hizo ishara kubwa mbele yetu, na ambaye alituhifadhi sisi katika njia zote ambazo sisi tuliziendea, na miongoni mwa mataifa yote ambayo tulipita kati kati yake,
18Na Yahweh aliwaondoa mbele yetu watu wote, na Waamori walioishi katika nchi hii. Hivyo, tutamwabudu Yahweh pia, kwa kuwa ni Mungu wetu”

19Lakini Yoshua akawaambia watu, “Hamwezi kumtumikia Yahweh, kwa kuwa ni Mungu mtakatifu; ni Mungu mwenye wivu; hatawasamehe makosa na dhambi zenu.
20Kama mtamwacha Yahweh na kuabudu miungu ya kigeni, basi atageuka na kuwaharibu. Atawaangamizeni baada ya kuwa amewatendea mema.”
21Lakini watu walimwambia Yoshua, “Hapana, tutamwabudu Yahweh.”
22Kisha Yoshua akawaambia watu, “Ninyi ni mashahidi dhidi yenu wenyewe kuwa mmemchagua Yahweh ninyi wenyewe, ili mmwabudu yeye.” Watu walijibu, “Sisi ni mashahidi.”
23“Sasa wekeni mbali miungu ya kigeni iliyoko kwenu, na geuzeni moyo wenu umwelekee Yahweh, Mungu wa Israeli.”
24Watu wakamwambia Yoshua, “Tutamwabudu Yahweh Mungu wetu. Tutaisikiliza sauti yake.
25Yoshua alifanya agano na watu siku hiyo. Aliziweka maagizo na sheria huko Shekemu.
26Yoshua aliyaandika maneno haya katika kitabu cha sheria za Mungu. Alichukua jiwe kubwa na kulisimamisha hapo chini ya mti wa mwaloni uliokuwa karibu na mahali pa takatifu pa Yahweh.
27Yoshua akawaambia watu, “Tazama, jiwe hili litakuwa ushuhuda dhidi yenu. Limeyasikia maneno yote ambayo Yahweh alitwambia. Hivyo, litakuwa ni shahidi dhidi yenu, hamtakiwi kumkana Mungu wenu.”
28Basi Yoshua aliwaacha watu waende zao, kila mmoja alienda kwenye urithi wake.
29Baada ya mambo haya, Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa Yahweh, alikufa akiwa na miaka 110.
30Walimzika katika mpaka wa urithi wake mwenyewe huko Timnathi Sera, ambayo iko kwenye nchi ya milima ya Efraimu, upande wa Mlima Gaashi.
31Israeli ilimwabudu Yahweh siku zote za maisha ya Yoshua, na siku zote za wazee ambao walidumu pamoja na Yoshua, wale ambao waliona kila kitu ambacho Yahweh alikuwa ameifanyia Israeli.
32Mifupa ya Yusufu ambayo watu wa Israeli waliileta kutoka Misri, waliizika huko shekemu, katika sehemu ya nchi ambayo Yakobo alikuwa ameinunua kutoka kwa wana wa Hamori, baba wa Shekemu. Aliinunua kwa vipande mia moja vya fedha, na ulikuwa urithi kwa wazawa wa Yusufu.
33Eliazeri mwana wa Haruni alikufa pia. Walimzika huko Gibea, katika mji wa ambao alikuwa amepewa Finehasi mwanaye, na ulikuwa katika nchi ya milima ya Efraimu.