Text copied!
CopyCompare
Biblia ya Kiswahili - 2 Timotheo

2 Timotheo 3

Help us?
Click on verse(s) to share them!
1Lakini fahamu hili: katika siku za mwisho kutakuwa na nyakati ngumu.
2kwa sababu watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye majivuno, wenye dhihaka, wasiotii wazazi wao, wasiokuwa na shukurani na waovu.
3Wasio na upendo wa asili, wasiotaka kuishi kwa amani na yeyote, wachonganishi, wasingiziaji, wasioweza kujizuia, wenye vurugu, wasiopenda mema.
4Watakuwa wasaliti, wakaidi, wenye kujipenda wenyewe na wapenda anasa kuliko kumpenda Mungu.
5Kwa nje watakuwa na sura ya ucha Mungu, lakini wataikana nguvu yake. Jiepushe na watu hao.
6Kwa kuwa baadhi yao ni wanaume wanaoingia kwenye familia za watu na kushawishi wanawake wajinga. Hawa ni wanawake waliojawa dhambi na wenye kuongozwa na tamaa za kila aina.
7Wanawake hawa hujifunza siku zote, lakini kamwe hawawezi kuufikia ufahamu wa ile kweli.
8Kama vile ambavyo Yane na Yambre walisimama kinyume na Musa. Kwa njia hii walimu hawa wa uongo husimama kinyume na kweli. Ni watu walioharibiwa katika fikira zao, wasiokubalika kuhusiana na imani.
9Lakini hawataendelea mbali. Kwa kuwa upumbavu wao utawekwa wazi kwa watu wote, kama ulivyokuwa wa wale watu.
10Lakini wewe umeyafuata mafundisho yangu, mwenendo wangu, makusudi yangu, imani yangu, uvumilivu wangu, upendo wangu na ustahimilivu wangu,
11mateso, maumivu na yaliyonipata kule Antiokia, Ikonio na Listra. Niliyavumilia mateso. Bwana aliniokoa katika yote hayo.
12Wote wanaotaka kuishi katika maisha ya kumcha Mungu katika Kristo Yesu watateswa.
13Watu waovu na wadanganyifu watazidi kuwa waovu zaidi. Watawapotosha wengine. Wao wenyewe wamepotoshwa.
14Lakini wewe, dumu katika mambo uliyojifunza na kuyaamini kwa uthabiti. Kwa kuwa unajua umejifunza kwa nani.
15Unatambua ya kuwa tangu utotoni mwako uliyajua maandiko matakatifu. Haya yanaweza kukuhekimisha kwa ajili ya wokovu kwa njia ya imani katika kristo Yesu.
16Kila andiko limetiwa pumzi na Mungu. Linafaa kwa mafundisho yenye faida, kwa kushawishi, kwa kurekebisha makosa, na kwa kufundishia katika haki.
17Hii ni kwamba mtu wa Mungu awe kamili, akiwa amepewa nyenzo zote kwa ajili ya kutenda kila kazi njema.