19Lakini Yoshua akawaambia watu, “Hamwezi kumtumikia Yahweh, kwa kuwa ni Mungu mtakatifu; ni Mungu mwenye wivu; hatawasamehe makosa na dhambi zenu.
20Kama mtamwacha Yahweh na kuabudu miungu ya kigeni, basi atageuka na kuwaharibu. Atawaangamizeni baada ya kuwa amewatendea mema.”
21Lakini watu walimwambia Yoshua, “Hapana, tutamwabudu Yahweh.”
22Kisha Yoshua akawaambia watu, “Ninyi ni mashahidi dhidi yenu wenyewe kuwa mmemchagua Yahweh ninyi wenyewe, ili mmwabudu yeye.” Watu walijibu, “Sisi ni mashahidi.”
23“Sasa wekeni mbali miungu ya kigeni iliyoko kwenu, na geuzeni moyo wenu umwelekee Yahweh, Mungu wa Israeli.”
24Watu wakamwambia Yoshua, “Tutamwabudu Yahweh Mungu wetu. Tutaisikiliza sauti yake.
25Yoshua alifanya agano na watu siku hiyo. Aliziweka maagizo na sheria huko Shekemu.
26Yoshua aliyaandika maneno haya katika kitabu cha sheria za Mungu. Alichukua jiwe kubwa na kulisimamisha hapo chini ya mti wa mwaloni uliokuwa karibu na mahali pa takatifu pa Yahweh.
27Yoshua akawaambia watu, “Tazama, jiwe hili litakuwa ushuhuda dhidi yenu. Limeyasikia maneno yote ambayo Yahweh alitwambia. Hivyo, litakuwa ni shahidi dhidi yenu, hamtakiwi kumkana Mungu wenu.”
28Basi Yoshua aliwaacha watu waende zao, kila mmoja alienda kwenye urithi wake.
29Baada ya mambo haya, Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa Yahweh, alikufa akiwa na miaka 110.
30Walimzika katika mpaka wa urithi wake mwenyewe huko Timnathi Sera, ambayo iko kwenye nchi ya milima ya Efraimu, upande wa Mlima Gaashi.
31Israeli ilimwabudu Yahweh siku zote za maisha ya Yoshua, na siku zote za wazee ambao walidumu pamoja na Yoshua, wale ambao waliona kila kitu ambacho Yahweh alikuwa ameifanyia Israeli.
32Mifupa ya Yusufu ambayo watu wa Israeli waliileta kutoka Misri, waliizika huko shekemu, katika sehemu ya nchi ambayo Yakobo alikuwa ameinunua kutoka kwa wana wa Hamori, baba wa Shekemu. Aliinunua kwa vipande mia moja vya fedha, na ulikuwa urithi kwa wazawa wa Yusufu.