19 Lakini Yoshua akawaambia watu, “Hamwezi kumtumikia Yahweh, kwa kuwa ni Mungu mtakatifu; ni Mungu mwenye wivu; hatawasamehe makosa na dhambi zenu.
20 Kama mtamwacha Yahweh na kuabudu miungu ya kigeni, basi atageuka na kuwaharibu. Atawaangamizeni baada ya kuwa amewatendea mema.”
21 Lakini watu walimwambia Yoshua, “Hapana, tutamwabudu Yahweh.”
22 Kisha Yoshua akawaambia watu, “Ninyi ni mashahidi dhidi yenu wenyewe kuwa mmemchagua Yahweh ninyi wenyewe, ili mmwabudu yeye.” Watu walijibu, “Sisi ni mashahidi.”
23 “Sasa wekeni mbali miungu ya kigeni iliyoko kwenu, na geuzeni moyo wenu umwelekee Yahweh, Mungu wa Israeli.”
24 Watu wakamwambia Yoshua, “Tutamwabudu Yahweh Mungu wetu. Tutaisikiliza sauti yake.
25 Yoshua alifanya agano na watu siku hiyo. Aliziweka maagizo na sheria huko Shekemu.
26 Yoshua aliyaandika maneno haya katika kitabu cha sheria za Mungu. Alichukua jiwe kubwa na kulisimamisha hapo chini ya mti wa mwaloni uliokuwa karibu na mahali pa takatifu pa Yahweh.
27 Yoshua akawaambia watu, “Tazama, jiwe hili litakuwa ushuhuda dhidi yenu. Limeyasikia maneno yote ambayo Yahweh alitwambia. Hivyo, litakuwa ni shahidi dhidi yenu, hamtakiwi kumkana Mungu wenu.”
28 Basi Yoshua aliwaacha watu waende zao, kila mmoja alienda kwenye urithi wake.
29 Baada ya mambo haya, Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa Yahweh, alikufa akiwa na miaka 110.
30 Walimzika katika mpaka wa urithi wake mwenyewe huko Timnathi Sera, ambayo iko kwenye nchi ya milima ya Efraimu, upande wa Mlima Gaashi.
31 Israeli ilimwabudu Yahweh siku zote za maisha ya Yoshua, na siku zote za wazee ambao walidumu pamoja na Yoshua, wale ambao waliona kila kitu ambacho Yahweh alikuwa ameifanyia Israeli.
32 Mifupa ya Yusufu ambayo watu wa Israeli waliileta kutoka Misri, waliizika huko shekemu, katika sehemu ya nchi ambayo Yakobo alikuwa ameinunua kutoka kwa wana wa Hamori, baba wa Shekemu. Aliinunua kwa vipande mia moja vya fedha, na ulikuwa urithi kwa wazawa wa Yusufu.