11Kutoka Troa, tulisafiri kwa meli moja kwa moja mpaka Samothrake, na kesho yake tukatia nanga Neapoli.
12Kutoka huko, tulikwenda mpaka Filipi, mji wa wilaya ya kwanza ya Makedonia, na ambao pia ni koloni la Waroma. Tulikaa katika mji huo siku kadhaa.
13Siku ya Sabato tulitoka nje ya mji, tukaenda kando ya mto ambapo tulidhani ya kuwa ni mahali pa kusali. Tuliketi, tukaongea na wanawake waliokusanyika mahali hapo.
14Miongoni mwa wale waliotusikiliza alikuwa mwanamke mmoja mcha Mungu aitwaye Ludia mwenyeji wa Thuatira, ambaye alikuwa mfanyabiashara ya nguo za kitani za rangi ya zambarau. Bwana aliufungua moyo wake hata akayapokea yale maneno Paulo aliyokuwa anasema.
15Baada ya huyo mama pamoja na jamaa yake kubatizwa, alitualika akisema, “Kama kweli mmeona kwamba mimi namwamini Bwana, karibuni nyumbani kwangu mkakae.” Akatuhimiza twende.
16Siku moja, tulipokuwa tunakwenda mahali pa kusali, msichana mmoja aliyekuwa na pepo mwenye uwezo wa kuagua alikutana nasi. Msichana huyo alikuwa anawapatia matajiri wake fedha nyingi kwa uaguzi wake.
17Basi, huyo msichana alimfuata Paulo na sisi, akipiga kelele na kusema, “Hawa watu ni watumishi wa Mungu Mkuu. Wanawatangazieni njia ya wokovu.”
18Akawa anafanya hivyo kwa siku nyingi hata siku moja Paulo alikasirika, akamgeukia na kumwambia huyo pepo, “Nakuamuru kwa jina la Yesu Kristo, mtoke huyu!” Mara huyo pepo akamtoka.
19Matajiri wa yule msichana walipoona kwamba tumaini lao la kupata mali limekwisha, waliwakamata Paulo na Sila, wakawaburuta mpaka hadharani, mbele ya wakuu.
20Wakawashtaki kwa mahakimu wakisema, “Watu hawa ni Wayahudi na wanafanya fujo katika mji wetu.
21Wanafundisha desturi ambazo sisi raia wa Roma haturuhusiwi kuzikubali wala kuzifuata.”
22Kundi la watu likajiunga nao, likawashambulia. Wale mahakimu wakawatatulia Paulo na Sila mavazi yao, wakaamuru wapigwe viboko.
23Baada ya kupigwa sana wakatiwa ndani, na askari wa gereza akaamriwa kuwaweka chini ya ulinzi mkali.
24Kutokana na maagizo hayo, huyo askari aliwaweka katika chumba cha ndani kabisa cha gereza na kuifunga miguu yao kwenye nguzo.
25Karibu na usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakisali na kuimba nyimbo za kumsifu Mungu, huku wafungwa wengine wakiwa wanasikiliza.
26Ghafla, kulitokea mtetemeko mkuu wa ardhi ambao uliitikisa misingi ya gereza. Mara, milango yote ikafunguka na minyororo iliyowafunga hao wafungwa ikaachana.
27Askari wa gereza alipoamka na kuiona milango ya gereza imefunguliwa, alidhani kwamba wafungwa wote walikuwa wametoroka na hivyo akauchomoa upanga wake, akataka kujiua.
28Lakini Paulo akaita kwa sauti kubwa: “Usijidhuru mwenyewe kwa maana sisi sote tuko hapa.”
29Baada ya kumwita mtu alete taa, huyo askari wa gereza alikimbilia ndani, akajitupa mbele ya miguu ya Paulo na Sila huku akitetemeka kwa hofu.
30Halafu aliwaongoza nje, akawauliza, “Waheshimiwa, nifanye nini nipate kuokoka?”
31Wao wakamjibu, “Mwamini Bwana Yesu nawe utaokolewa pamoja na jamaa yako yote.”
32Basi, wakamhubiria neno la Bwana yeye pamoja na jamaa yake.