Text copied!
Bibles in Swahili (individual language)

Matendo 16:11-32 in Swahili (individual language)

Help us?

Matendo 16:11-32 in Biblia Takatifu

11 Kutoka Troa, tulisafiri kwa meli moja kwa moja mpaka Samothrake, na kesho yake tukatia nanga Neapoli.
12 Kutoka huko, tulikwenda mpaka Filipi, mji wa wilaya ya kwanza ya Makedonia, na ambao pia ni koloni la Waroma. Tulikaa katika mji huo siku kadhaa.
13 Siku ya Sabato tulitoka nje ya mji, tukaenda kando ya mto ambapo tulidhani ya kuwa ni mahali pa kusali. Tuliketi, tukaongea na wanawake waliokusanyika mahali hapo.
14 Miongoni mwa wale waliotusikiliza alikuwa mwanamke mmoja mcha Mungu aitwaye Ludia mwenyeji wa Thuatira, ambaye alikuwa mfanyabiashara ya nguo za kitani za rangi ya zambarau. Bwana aliufungua moyo wake hata akayapokea yale maneno Paulo aliyokuwa anasema.
15 Baada ya huyo mama pamoja na jamaa yake kubatizwa, alitualika akisema, “Kama kweli mmeona kwamba mimi namwamini Bwana, karibuni nyumbani kwangu mkakae.” Akatuhimiza twende.
16 Siku moja, tulipokuwa tunakwenda mahali pa kusali, msichana mmoja aliyekuwa na pepo mwenye uwezo wa kuagua alikutana nasi. Msichana huyo alikuwa anawapatia matajiri wake fedha nyingi kwa uaguzi wake.
17 Basi, huyo msichana alimfuata Paulo na sisi, akipiga kelele na kusema, “Hawa watu ni watumishi wa Mungu Mkuu. Wanawatangazieni njia ya wokovu.”
18 Akawa anafanya hivyo kwa siku nyingi hata siku moja Paulo alikasirika, akamgeukia na kumwambia huyo pepo, “Nakuamuru kwa jina la Yesu Kristo, mtoke huyu!” Mara huyo pepo akamtoka.
19 Matajiri wa yule msichana walipoona kwamba tumaini lao la kupata mali limekwisha, waliwakamata Paulo na Sila, wakawaburuta mpaka hadharani, mbele ya wakuu.
20 Wakawashtaki kwa mahakimu wakisema, “Watu hawa ni Wayahudi na wanafanya fujo katika mji wetu.
21 Wanafundisha desturi ambazo sisi raia wa Roma haturuhusiwi kuzikubali wala kuzifuata.”
22 Kundi la watu likajiunga nao, likawashambulia. Wale mahakimu wakawatatulia Paulo na Sila mavazi yao, wakaamuru wapigwe viboko.
23 Baada ya kupigwa sana wakatiwa ndani, na askari wa gereza akaamriwa kuwaweka chini ya ulinzi mkali.
24 Kutokana na maagizo hayo, huyo askari aliwaweka katika chumba cha ndani kabisa cha gereza na kuifunga miguu yao kwenye nguzo.
25 Karibu na usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakisali na kuimba nyimbo za kumsifu Mungu, huku wafungwa wengine wakiwa wanasikiliza.
26 Ghafla, kulitokea mtetemeko mkuu wa ardhi ambao uliitikisa misingi ya gereza. Mara, milango yote ikafunguka na minyororo iliyowafunga hao wafungwa ikaachana.
27 Askari wa gereza alipoamka na kuiona milango ya gereza imefunguliwa, alidhani kwamba wafungwa wote walikuwa wametoroka na hivyo akauchomoa upanga wake, akataka kujiua.
28 Lakini Paulo akaita kwa sauti kubwa: “Usijidhuru mwenyewe kwa maana sisi sote tuko hapa.”
29 Baada ya kumwita mtu alete taa, huyo askari wa gereza alikimbilia ndani, akajitupa mbele ya miguu ya Paulo na Sila huku akitetemeka kwa hofu.
30 Halafu aliwaongoza nje, akawauliza, “Waheshimiwa, nifanye nini nipate kuokoka?”
31 Wao wakamjibu, “Mwamini Bwana Yesu nawe utaokolewa pamoja na jamaa yako yote.”
32 Basi, wakamhubiria neno la Bwana yeye pamoja na jamaa yake.
Matendo 16 in Biblia Takatifu

Matendo ya Mitume 16:11-32 in Biblia ya Kiswahili

11 Hivyo tukaondoka kutoka Troa, tukaenda moja kwa moja Samothrake, na siku iliyofuata tukafika mji wa Neapoli.
12 Kutoka hapo tukaenda Filipi ambao ni moja ya mji wa Makedonia, mji muhimu katika wilaya na utawala wa Kirumi na tukakaa siku kadhaa.
13 Siku ya Sabato, tulikwenda nje ya lango kwa njia ya mto, sehemu ambayo tulidhania kutakuwa na mahali pa kufanyia maombi. Tulikaa chini na kuongea na akinamama waliokuja pamoja.
14 Mwanamke mmoja aitwaye Lidia, muuzaji wa zambarau, kutoka katika mji wa Tiatira, mwenye kumwabudu Mungu, alitusikiliza. Bwana alimfungua moyo wake na kuweka maanani maneno yaliyosemwa na Paulo.
15 Baada ya kubatizwa, yeye na nyumba yake yote, alitusihi akisema “kama mmeniona kuwa mimi ni mwaminifu katika Bwana, basi nawasihi muingie na kukaa kwangu”. Akatusihi sana.
16 Ikawa kwamba, tulipokuwa tunaenda mahali pa kuomba, msichana mmoja aliyekuwa na pepo la utambuzi akakutana nasi. Alimletea bwana wake faida nyingi kwa kubashiri.
17 Mwanamke huyu alimfuata Paulo pamoja na sisi, akipiga kelele na kusema “Hawa wanaume ni watumishi wa Mungu aliye Mkuu, wanaowatangazia ninyi habari ya wokovu”.
18 Alifanya hivyo kwa siku nyingi, lakini Paulo akiwa amekasirishwa na tendo hilo, aligeuka nyuma na kumwambia pepo, “Nakuamuru kwa Jina la Yesu umtoke ndani yake.” Naye akatoka na kumwacha mara moja.
19 Mabwana zake walipoona ya kuwa tumaini la faida yao limeondoka, waliwakamata Paulo na Sila na kuwaburuza sokoni mbele ya wenye mamlaka.
20 Walipowafikisha kwa mahakimu, walisema, “Hawa wanaume ni Wayahudi na wanasababisha ghasia kubwa katika mji wetu.
21 Wanafundisha mambo ambayo siyo sheria sisi kuyapokea wala kuyafuata kama Warumi.”
22 Umati ukawainukia kinyume Paulo na Sila, mahakimu wakararua nguo zao na kuwavua na kuamuru wachapwe viboko
23 Baada ya kuwachapa viboko vingi, waliwatupa gerezani na kumuamuru askari wa gereza kuwalinda vyema.
24 Baada ya kupokea amri hiyo, askari wa gereza aliwatupa katika chumba cha ndani ya gereza na kuwafunga miguu yao kwenye sehemu alipowahifadhi.
25 Wakati wa usiku wa manane, Paulo na Sila wakawa wakiomba na kuimba nyimbo za kumsifu Mungu, huku wafungwa wengine wakiwasikiliza,
26 Ghafla kukatokea tetemeko kuu na misingi ya gereza ikatikiswa, milango ya gereza ikafunguka, na minyororo ya wafungwa wote ikalegezwa.
27 Mlinzi wa Gereza aliamka kutoka usingizini na akaona milango yote ya gereza imefunguliwa; hivyo akachukua upanga wake maana alitaka kujiua kwa sababu alifikiri wafungwa wote walikwishatoroka,
28 Lakini, Paulo akapiga kelele kwa sauti kuu, akisema “usijidhuru kwa sababu wote tuko mahali hapa”.
29 Mlinzi wa gereza aliomba taa ziletwe na akaingia ndani ya gereza kwa haraka, akitetemeka na kuogopa, akawaangukia Paulo na Sila,
30 na kuwatoa nje ya gereza na kusema, “Waheshimiwa, nifanye nini ili nipate kuokoka?”
31 Nao wakamwambia, “Mwamini Bwana Yesu nawe utaokoka pamoja na nyumba yako.”
32 Walinena neno la Bwana kwake, pamoja na watu wote wa nyumbani kwake,
Matendo ya Mitume 16 in Biblia ya Kiswahili