27Kisha kuanzia kutoka kwa Musa na manabii wote, Yesu akawatafsiria mambo yanayomuhusu yeye katika maandiko yote.
28Walipokaribia kile kijiji, huko walikokuwa wakienda, Yesu akafanya kana kwamba anaendelea mbele.
29Lakini walimlazimisha, wakisema, “Kaa pamoja nasi, maana inaelekea jioni na siku ni kama imeisha.” Hivyo Yesu akaingia kwenda kukaa nao.
30Ilitokea kwamba, wakati amekaa nao kula, alichukua mkate, akaubariki, na kuuvunja, akawapa.
31Kisha macho yao yakafunguliwa, wakamjua, na akatoweka ghafla mbele ya macho yao.
32Wakasemezana wao kwa wao, “Hivi mioyo yetu haikuwaka ndani yetu, wakati alipoongea nasi njiani, wakati alipotufungulia maandiko?”
33Wakanyanyuka saa hiyo hiyo, na kurudi Yerusalemu. Wakawakuta wale kumi na mmoja wamekusanyika pamoja, na wale waliokuwa pamoja nao,
34wakisema, “Bwana amefufuka kwelikweli, na amemtokea Simoni.”
35Hivyo wakawaambia mambo yaliyotokea njiani, na namna Yesu alivyodhihirishwa kwao katika kuumega mkate.
36Wakati wakiongea mambo hayo, Yesu mwenyewe alisimama katikati yao, na akawaambia, “Amani iwe kwenu.”
37Lakini waliogopa na kujawa na hofu, na wakafikiri kwamba waliona roho.
38Yesu akawaambia, Kwanini mnafadhaika? Kwanini maswali yanainuka mioyoni mwenu?
39Angalieni mikono yangu na miguu yangu, kwamba ni mimi mwenyewe. Niguseni na muone. Kwa maana roho haina nyama na mifupa, kama mnionavyo mimi kuwa navyo.”
40Alipokwisha kusema hivi, akawaonyesha mikono yake na miguu yake.
41Walipokuwa bado na furaha iliyochanganyikana na kutokuamini, na kustaajabu, Yesu akawaambia, “Je mna kitu chochote cha kula?”