1Kisha Mungu akambariki Nuhu na wanawe, na kuwaambia, “Zaeni, mkaongezeke, na muijaze nchi.
2Hofu na utisho wenu vitakuwa juu ya kila mnyama aliye hai juu ya nchi, juu ya kila ndege wa angani, juu ya kila kitu kiendacho chini juu ya ardhi, na juu ya samaki wote wa baharini. Vimetolewa katika mikono yenu.
3Kila kitu kiendacho kilicho hai kitakuwa chakula kwa ajili yenu. Kama nilivyo wapa mimea, sasa nawapa kila kitu.
4Lakini msile nyama pamoja na uhai wake - yaani damu yake - ndani yake.
5Lakini kwa ajili ya damu yenu, uhai uliomo katika damu yenu nitataka malipo. Kutoka katika mkono wa kila mnyama nitaitaka. Kutoka katika mkono wa kila mtu, yaani, kutoka katika mkono wa yule ambaye amemuua ndugu yake, nitataka fidia kwa ajili ya uhai wa mtu huyo.
6Yeyote amwagaye damu ya mtu, kwa njia ya mtu damu yake itamwagwa, kwa sababu ilikuwa ni katika mfano wa Mungu kwamba Mungu alimuumba mtu.
7Na hivyo nanyi zaeni na kuongezeka, sambaeni katika inchi yote na muongezeke juu yake.”
8Kisha Mungu akazungumza na Nuhu na wanae pamoja naye, akisema,
9“Kwa ajili yangu, sikiliza! Ninakwenda kulithibitisha agano langu pamoja nawe na uzao wenu baada yenu,
10na kwa kila kiumbe hai kilicho pamoja nawe, pamoja na ndege, mnyama wa kufugwa, na kila kiumbe cha nchi pamoja nawe, kuanzia kwa wote waliotoka kwenye safina, mpaka kwa kila kiumbe hai juu ya nchi.
11Kwa sababu hii ninalithibitisha agano langu pamoja nanyi, kwamba hapatatokea kuangamizwa kwa mwenye mwili kwa njia ya maji ya gharika. Tena hapatatokea gharika ya kuangamiza nchi.”
12Mungu akasema, “na hii ndiyo ishara ya agano ambalo ninafanya kati yangu na ninyi pamoja na kila kiumbe hai kilicho pamoja nanyi, kwa vizazi vyote vya baadaye:
13Nimeweka upinde wangu wa mvua katika wingu, na itakuwa ndiyo ishara ya agano kati yangu na nchi.
14Hata itakuwa nitakapoleta wingu juu ya nchi na upinde wa mvua ukaonekana katika wingu,
15ndipo nitakumbuka agano langu, ambalo ni kati yangu na ninyi na kila kiumbe hai cha wote mwenye mwili. Maji hayatafanyika tena gharika kuharibu wote wenye mwili.
16Upinde wa mvua utakuwa katika mawingu na nitauona, ili kukumbuka agano la milele kati ya Mungu na kila kiumbe hai cha wote wenye mwili ambacho kiko juu ya nchi.”
17Kisha Mungu akamwambia Nuhu, “Hii ni ishara ya agano ambalo nimelithibitisha kati yangu na wenye mwili wote ambao wako juu ya nchi.”
18Wana wa Nuhu ambao walitoka katika safina walikuwa ni Shemu, Hamu, na Yafethi. Na Hamu akamzaa kanaani.
19Watatu hawa walikuwa ndio wana wa Nuhu, na kutokea kwa hawa nchi yote ikajaa watu.
20Nuhu akaanza kuwa mkulima, na akapanda mizabibu.
21Akanywa sehemu ya divai na akalewa. Akawa amelala hemeani uchi.
22Kisha Hamu, baba yake na Kanaani, akaona uchi wa baba yake na akawaambia ndugu zake wawili waliokuwa nje.
23Kwa hiyo Shemu na Yafethi wakachukua kanzu wakaitanda juu ya mabega yao, na wakatembea kinyumenyume na wakaufunika uchi wa baba yao. Nyuso zao zikiwa zimegeuka nyuma upande mwingine, kwa hiyo hawakuona uchi wa baba yao.
24Nuhu alipozinduka kutoka katika ulevi wake, alijua ni jambo gani mtoto wake mdogo amemfanyia.
25Hivyo akasema, “Alaaniwe Kanaani. Na awe mtumishi kwa watumishi wa ndugu zake.”
26Akasema pia, Yahwe, Mungu wa Shemu, abarikiwe, Kanaani na awe mtumwa wake.
27Mungu na apanuwe mipaka ya Yafethi, na afanye makazi yake katika hema za Shemu. Kanaani na awe mtumwa wake.”
28Baada ya gharika, Nuhu aliishi miaka miatatu na hamsini.
29Siku zote za Nuhu zilikuwa ni miaka mia tisa na hamsini, na kisha alikufa.