1Kisha Yakobo akaendelea na safari yake na akafika katika nchi ya watu wa mashariki.
2Hata alipotazama, akaona kisima kondeni, na, tazama, makundi matatu ya kondoo yalikuwa yamelala kando yake. Kwani kutoka katika hicho wangeyanywesha makundi, na jiwe juu ya mdomo wa kisima lilikuwa kubwa.
3Wakati makundi yote yangekusanyika pale, wachungaji wangevingirisha jiwe kutoka katika mdomo wa kisima na kuwanywesha kondoo, na kisha kurudisha jiwe juu ya mdomo wa kisima, mahali pake.
4Yakobo akawambia, “Ndugu zangu, ninyi mnatokea wapi?” nao wakasema, “Tunatoka Harani.”
5Akawambia, “Mnamfahamu Labani mwana wa Nahori?” Wakasema, “Tunamfahamu.”
6Akawambia, “Je hajambo?” Wakasema, “Hajambo, na, tazama pale, Raheli binti yake anakuja na kondoo.”
7Yakobo akasema, “Tazama, ni mchana. Siyo wakati wa kukusanya kondoo pamoja. Mnapaswa kuwanywesha kondoo na kisha mkaenda na kuwaacha wachunge.”
8Wakamwambia, “Hatuwezi kuwanywesha mpaka makundi yote yakusanyike pamoja. Ndipo wanaume watakapovingirisha jiwe kutoka mlangoni mwa kisima, na ndipo tutakapowanywesha kondoo.”
9Wakati bado Yakobo anaongea nao, Raheli akaja pamoja na kondoo wa babaye, kwani alikuwa akiwachunga.
10Yakobo alipomwona Raheli, binti wa Labani, kaka wa mamaye, na kondoo wa Labani, kaka wa mama yake, Yakobo akaja juu, akalivingirisha jiwe kutoka mlangoni mwa kisima, na akawanywesha kondoo wa Labani, kaka wa mama yake.
11Yakobo akambusu Raheli na akalia kwa sauti.
12Yakobo akamwambia Raheli kwamba alikuwa ni ndugu wa baba yake, na kwamba alikuwa mwana wa Rebeka. Kisha yeye akakimbia kumwambia baba yake.
13Labani aliposikia habari kuhusu Yakobo mwana wa dada yake, akaenda kukutana naye, akamkumbatia, akambusu, na kumleta nyumbani kwake. Yakobo akamwambia Labani mambo haya yote.
14Labani akamwambia, “Kwa hakika wewe ni mfupa wangu na nyama yangu.” Kisha Yakobo akakaa naye kama mwezi mmoja.
15Kisha Labani akamwambia Yakobo, “Je unitumikie bure kwa kuwa wewe ni ndugu yangu? Niambie, ujira wako utakuwaje?
16Basi Labani alikuwa na binti wawili. Jina la mkubwa lilikuwa ni Lea, na jina la mdogo lilikuwa Raheli.
17Macho ya Lea yalikuwa dhaifu, lakini Raheli alikuwa mzuri wa umbo na mwonekano.
18Yakobo alimpenda Raheli, hivyo akasema, “Nitakutumikia miaka saba kwa ajili ya Raheli, binti yako mdogo.”
19Labani akasema, Itakuwa vema kukupa wewe, kuliko kumpa mtu mwingine. Kaa nami.”
20Hivyo Yakobo akamtumikia kwa miaka saba kwa ajili ya Raheli; nayo ilionekana kwake kama siku chache tu, kwa ajili ya upendo aliokuwa nao kwake.
21Kisha Yakobo akamwambia Labani, “Nipe mke wangu, kwani siku zangu zimetimia - ili kwamba nimwoe!
22Hivyo Labani akawaalika watu wa mahali hapo na kuandaa sherehe.
23Wakati wa jioni, Labani akamchukua Lea binti yake mkubwa na kumleta kwa Yakobo, aliyelala naye.
24Labani akampa mtumishi wake wakike Zilpa kuwa mjakazi wa Lea.
25Ilipofika asubuhi, tazama, kumbe ni Lea! Yakobo akamwambia Labani, “Ni nini hiki ulichonifanyia? Je sikukutumikia kwa ajili ya Raheli? Kwa nini basi umenihadaa?
26Labani akamwambia, “Siyo utamaduni wetu kumtoa bindi mdogo kabla ya mzaliwa wa kwanza.
27Timiza juma la bibi arusi, na tutakupa yule mwingine pia kwa mbadala wa kunitumikia miaka mingine saba.”
28Yakobo akafanya hivyo, na akatimiza juma la Lea. Kisha Labani akampa Raheli binti yake kuwa mke wake.
29Lakini pia Labani akampa Raheli binti yake Bilha, kuwa mjakazi wake.
30Hivyo Yakobo akalala na Raheli, pia, lakini akampenda Raheli zaidi ya Lea. Hivyo Yakobo akamtumikia Labani kwa miaka saba mingine.
31Yahwe akaona kwamba Lea hakupendwa, hivyo akalifungua tumbo lake, lakini Raheli hakuwa na mtoto.
32Lea akashika mimba na kuzaa mwana, naye akamwita Rubeni. Kwani alisema, “Kwa sababu Yahwe ameliangalia teso langu; bila shaka mme wangu sasa atanipenda.”
33Kisha akashika mimba tena na kuzaa mwana. Akasema, “Kwa sababu Yahwe amesikia kwamba sipendwi, kwa hiyo amenipa mwana mwingine,” na akamwita Simoni.
34Kisha akashika mimba tena na kuzaa mwana. Akasema, “Wakati huu mme wangu ataungana nami, kwa kuwa nimemzalia wana watatu.” Kwa hiyo akaitwa Lawi.
35Akashika mimba tena na kuzaa mwana. Akasema, “Wakati huu nitamsifu Yahwe.” Kwa hiyo akamwita jina lake Yuda; kisha akaacha kuzaa watoto.