1Ikawa wakati watu walipoanza kuongezeka juu ya uso wa nchi na wana wa kike wakazaliwa kwao,
2wana wa Mungu walipoona kuwa mabinti wa wanadamu ni wenye kuvutia. waliwachukua kuwa wake zao, kila waliye mchagua.
3Yahwe akaema, “roho yangu haitasalia kwa mwanadamu milele, kwa kuwa wao ni nyama. Wataishi miaka 120.”
4Majitu makubwa yalikuwa juu ya uso wa nchi nyakati hizo, na hata baada ya hapo. Hii ilitokea wakati wana wa Mungu walipowaoa binti za wanadamu, na kupata watoto pamoja nao. Hawa walikuwa watu hodari zamani, watu wenye sifa.
5Yahwe akaona kwamba uovu wa watu umezidi katika nchi, na kwamba mawazo ya mioyo yao daima inaelekea tu katika uovu.
6Yahwe akajuta kuwa amemuumba mwanadamu juu ya nchi, na ikamuhuzunisha moyo wake.
7Kwa hiyo Yahwe akasema, “Nitamfutilia mbali mwanadamu ambaye nimemuumba katika uso wa nchi; mwanadamu na wanyama wakubwa, na vitambaavyo na ndege wa angani, kwa kuwa nimehuzunika kuwa nimeviumba.”
8Lakini Nuhu akapata neema ya upendeleo machoni pa Yahwe.
9Kulikuwa na matukio kumuhusu Nuhu. Nuhu alikuwa mtu mwenye haki, na asiye na lawama miongoni mwa watu wa kipindi chake. Nuhu alitembea na Mungu.
10Nuhu akafanyika baba wa wana watatu wa kiume: Shem, Ham na Yafeti.
11Nchi iliharibika mbele za Mungu, na ikajaa ghasia.
12Mungu akaiona nchi; tazama, ilikuwa imeharibika, kwa kuwa wote wenye mwili walikuwa wameharibu njia zao juu ya nchi.
13Mungu akamwambia Nuhu, “Nimeona kuwa sasa niwakati wa mwisho kwa wote wenye mwili, kwa kuwa inchi imejaa ghasia kutokana na wao. Hakika, nitawaharibu wao pamoja na nchi.
14Tengeneza safina ya mti wa mvinje kwa ajili yako. Tengeneza vyumba katika safina, na vifunike kwa lami ndani na nje.
15Hivi ndivyo utakavyofanya: urefu wa safina dhiraa miatatu, upana wake dhiraa hamsini, kwenda juu kwake dhiraa thelathini.
16Tengeneza paa la safina, na ulimalize kwa kipimo cha dhiraa kutoka juu ubavuni. Weka mlango katika ubavu wa safina na utengeneze dari ya chini, ya pili na ya tatu.
17Sikiliza, nimekaribia kuleta gharika ya maji juu ya nchi, kuharibu wenye mwili wote wakaao ndani ya nchi wenye pumzi ya uhai chini ya mbingu. Kila kitu kilichopo juu ya nchi kitakufa.
18Lakini nitalifanya thabiti agano langu na wewe. Utaingia ndani ya safina, wewe, na wana wako wa kiume, na mke wako, pamoja na wake za wanao.
19Kwa kila kiumbe hai chenye mwili, viwili vya kila aina utavileta ndani ya safina, ili visalie hai pamoja nawe, vya kike na vya kiume.
20Katika ndege kwa jinsi yake, na wanyama wakubwa kwa jinsi yake, kila kitambaacho ardhini kwa jinsi yake, viwili viwili vya kila aina vitakuja kwako ili viwe salama.
21Kusanya kila aina ya chakula kinacholiwa kwa ajili yako na ukitunze, ili kwamba viwe chakula chako na chao.”
22Kwa hiyo Nuhu akafanya hivi. kulingana na yote ambayo Mungu alimuagiza, ndivyo alifanya.