1Yusufu akamwamru msimamizi wa nyumba yake, akisema, “Jaza magunia ya watu hawa kwa chakula, kiasi wawezacho kubeba, na uweke pesa ya kila mtu katika mdomo wa gunia lake.
2Uweke kikombe changu, cha fedha, katika mdomo wa gunia la mdogo, na pesa yake ya chakula pia.” Msimamizi akafanya kama Yusufu alivyosema.
3Kukapambazuka asubuhi, na wale watu wakaruhusiwa kuondoka, wao na punda zao.
4Walipokuwa wametoka mjini lakini hawajafika mbali, Yusufu akamwambia msimamizi wa nyumba yake, “Inuka, uwafuatie wale watu, na utakapowapata, wambie, 'Kwa nini mmelipa uovu badala ya mema?
5Je hiki siyo kikombe ambacho bwana wangu hukinywea, na kikombe akitumiacho kwa uaguzi? Mmefanya vibaya, kwa jambo hili mlilolifanya.”
6Msimamizi wa nyumba akawapata na kuwambia maneno haya.
7Wakasema, “Kwa nini bwana wetu anasema maneno kama haya? Na iwe mbali na watumishi wako kwamba wanaweza kufanya jambo hili.
8Tazama, pesa tulizozikuta katika midomo ya magunia yetu, tulizileta kwako kutoka katika nchi ya Kanaani. Ni kwa jinsi gani basi tunaweza kuiba katika nyumba ya bwana wako fedha au dhahabu?
9Yeyote kitakayeonekana kwake miongoni mwa watumishi wako, atakufa, nasi sote tutakuwa watumwa wa bwana wangu.”
10Msimamizi akasema, “Basi na iwe kwa kadili ya maneno yenu. Yeye ambaye kikombe kitaonekana kwake atakuwa mtumwa wangu, nanyi wengine mtakuwa bila hatia.”
11Kisha kila mtu akaharakisha na kulishusha gunia lake chini. na kila mtu akalifungua gunia lake.
12Msimamizi akatafuta. akaanza na mkubwa wa wote na kumaliza kwa mdogo wa wote, na kikombe kikaonekana katika gunia la Benjamini.
13Wakararua mavazi yao. Kila mtu akapakia juu ya punda wake nao wakarudi mjini.
14Yuda na ndugu zake wakaja katika nyumba ya Yusufu. Bado alikuwepo pale, nao wakainama mbele zake hata chini.
15Yusufu akawambia, “Je ni nini hili mlilolifanya? Je hamjui kwamba mtu kama mimi anafanya uaguzi.
16Yuda akasema, “Je tunaweza kumwambia nini bwana wangu? Tuseme nini? au ni jinsi gani twaweza kujithibitisha wenyewe? Mungu ameona uovu wa watumishi wako. Tazama, sisi ni watumwa wa bwana wangu, wote sisi na yule ambaye kikombe kimeonekana mkononi mwake.”
17Yusufu akasema, “Na iwe mbali nami kwamba naweza kufanya hivyo. Mtu ambaye kikombe kimeonekana mkononi mwake, huyu ndiye atakuwa mtumwa wangu, lakini ninyi wengine, nendeni kwa amani kwa baba yenu.”
18Ndipo Yuda alipomkaribia na kusema, “Bwana wangu, tafadhari mwache mtumishi wako aseme neno katika masikio ya bwana wangu, na usiziache hasira zako kuwaka dhidi ya mtumishi wako, kwani wewe ni kama Farao.
19Bwana wangu aliwauliza watumishi wake, kusema, Je mnaye baba au ndugu?'
20Nasi tukamwambia bwana wangu, 'Tunaye baba, ni mzee, na mwana wa uzee wake, ni mdogo. Na ndugu yake alishakufa, na yeye peke yake ndiye amebaki kwa mama yake, na baba yake anampenda.'
21Nawe ukawambia matumishi wako, 'Mleteni ili nimwone.'
22Nasi tukamwambia bwana wangu, 'Kijana hawezi kumwacha babaye. Kwani akimwacha babaye baba yake angekufa.'
23Na ukawambia watumishi wako, 'Mdogo wenu asipokuja pamoja nanyi, hamtauona uso wangu tena.'
24Na ikawa tulipokwenda kwa mtumishi wako baba yangu, tulimwambia maneno ya bwana wangu.
25Na baba yetu akasema, Nendeni tena, mkatununulie chakula.'
26Nasi tukasema, “Hatuwezi kushuka. Ikiwa mdogo wetu atakuwa nasi, ndipo tutakaposhuka, kwani hatuwezi kuuona uso wa mtu yule mdogo wetu asipokuwa pamoja nasi.'
27Mtumishi wako baba yetu akatwambia, 'Mnajua kwamba mke wangu alinizalia wana wawili.
28Na mmoja akatoka kwangu nami nikasema, “Bila shaka ameraruliwa vipande, na tangu hapo sijamwona.”
29Nanyi mkimchukua huyu naye kutoka kwangu mabaya yanaweza kumpata, mtashusha mvi zangu kwa kaburini kwa huzuni.
30Kwa hiyo, basi, nitapokuja kwa mtumishi wako baba yangu, na kijana hayupo nasi, kwa kuwa uhai wake umefungamanishwa katika uhai wa kijana,
31itakuwa, atakapoona kwamba kijana hayupo nasi atakufa. Na watumishi wako watazishusha mvi za mtumishi wako baba yetu kaburini kwa masikitiko.
32Kwani mtumishi wako alikuwa mdhamini wa kijana kwa baba yangu na alisema, 'Ikiwa sitamleta kwako, ndipo nitakapokuwa mwenye hatia kwa baba yangu daima.”
33Kwa hiyo sasa, tafadhari mwache mtumishi wake akae kama mtumwa kwa bwana wangu badala ya kijana, na umwache kijana aende na ndugu zake.
34Kwa maana nitakwenda jinsi gani kwa baba yangu ikiwa kijana hayupo nami? Ninaogopa kuona mabaya yatakayompata baba yangu.”