1Kisha Sarai mke wa Abram, alikuwa hajamzalia mtoto, lakini alikuwa na mtumishi wa kike, Mmisri ambaye jina lake aliitwa Hajiri.
2Kwa hiyo Sarai akamwambia Abram, “Tazama, Yahwe hajanifanya mimi kuwa na watoto. Nenda na ulale na mtumishi wangu. Ili kwamba niweze kupata watoto kupitia yeye.” Abram akasikiliza sauti ya Sarai.
3Ilikuwa baada ya Abram kuishi miaka kumi katika nchi ya Kanaani ndipo Sarai, mke wa Abram, alimtoa Hajiri yule mmisri mtumishi wake kwa mume wake awe kama mke wake.
4Kwa hiyo akawa na mahusiano na Hajiri, na akabeba mimba. Na alipoona kuwa amebeba mimba, akamdharau bibi yake.
5Kisha Sarai akamwambia Abram, “Jambo hili baya kwangu ni kwa sababu yako. Nilimtoa mtumishi wangu wa kike katika kumbatio lako. Na alipoona kuwa amebeba mimba, nilidharaulika machoni pake. Na sasa acha Yahwe aamuwe kati yangu na wewe.”
6Lakini Abram akamwambia Sarai, “Tazama, hapa, mtumishi wako yuko katika uwezo wako, fanya unachofikiri ni kizuri sana kwake.” Kwa hiyo Sarai akakabiliana naye kwa ukatili, na akatoroka.
7Malaika wa Yahwe akamkuta karibu na chemichemi ya maji katika jangwa, chemichemi iliyo katika njia kuelekea Shuri.
8Akasema, Hajiri, mtumishi wa Sarai, umetoka wapi na unakwenda wapi?” Na akasema, ninamtoroka bibi yangu Sarai.”
9Malaika wa Yahwe akamwambia, “Rudi kwa bibi yako, na unyenyekee chini ya mamlaka yake.”
10Kisha Malaika wa Yahwe akamwambia, “Nitazidisha uzao wako maradufu, kiasi kwamba watakuwa wengi wasioweza kuhesabika.”
11Malaika wa Yahwe pia akamwambia, “Tazama, wewe unamimba, na utazaa mtoto kiume, na utamwita jina lake Ishmaeli, kwasabab Yahwe amesikia mateso yako.
12Atakuwa punda mwitu wa mtu. Atakuwa adui dhidi ya kila mtu, na kila mtu atakuwa adui yake, na ataishi kando na ndugu zake wote.”
13Kisha akamwita jina hili Yahwe aliye zungumza naye, “Wewe ni Mungu unionaye mimi,” kwa kuwa alisema, “je ninaendelea kweli kuona, hata baada ya kuwa ameniona?”
14Kwa hiyo kisima kiliitwa Beerlahairori; Tazama, kiko kati ya Kadeshi na Beredi.
15Hajiri akamzalia Abram mwana wa kiume, na Abram akamwita mwanawe, ambaye Hajiri amemzaa jina, Ishmaeli.
16Abram alikuwa na umri wa miaka themanini na sita wakati Hajiri alipomzaa Ishmaeli kwa Abram.