Text copied!
CopyCompare
Biblia ya Kiswahili - Mwanzo

Mwanzo 26

Help us?
Click on verse(s) to share them!
1Basi njaa ikatokea katika nchi, mbali na njaa ya kwanza iliyotokea siku za Ibrahimu. Isaka akaenda kwa Abimeleki, mfalme wa Wafilisiti huko Gerari.
2Basi Yahwe akamtokea na kumwambia, “Usishuke kwenda Misri; kaa katika nchi niliyokuambia.
3Kaa katika nchi hii hii niliyokuambia, nami nitakuwa pamoja nawe na kukubariki; kwani kwako wewe na uzao wako, nitawapa nchi hii yote, nami nitatimiza kiapo nilichomwapia Ibrahimu baba yako.
4Nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, nami nitawapa uzao wako nchi hizi zote. Kupitia uzao wako mataifa yote ya dunia yatabarikiwa.
5Nitalifanya hili kwa sababu Ibrahimu aliitii sauti yangu na kutunza maelekezo yangu, amri zangu na sheria zangu.”
6Hivyo Isaka akakaa Gerari.
7Watu wa eneo hilo walipomwuliza juu ya mke wake, alisema, “Yeye ni dada yangu.” Aliogopa kusema, “Yeye ni mke wangu,” kwa kuwa alidhani, “Watu wa nchi hii wataniua ili wamchukue Rebeka, kwa kuwa ni mzuri wa uso.”
8Baada ya Isaka kuwa amekaa pale kwa muda mrefu, Ikatukia kwamba Abimeleki mfalme wa Wafilisiti alichungulia katika dirisha. Tazama, akamwona Isaka akimpapasa Rebeka, mke wake.
9Abimeleki akamwita Isaka kwake na kusema, “Tazama, kwa hakika yeye ni mke wako. Kwa nini ulisema, 'Yeye ni dada yangu?” Isaka akamwambia, “Kwa sababu nilidhani mtu mmoja aweza kuniua ili amchukue.”
10Abimeleki akamwambia, “Ni jambo gani hili ulilotufanyia? Mmojawapo wa watu angeweza bila shaka kulala na mke wako, nawe ungeweza kuleta hatia juu yetu.”
11Hivyo Abimeleki akawaonya watu wote na kusema, “Mtu yeyote atakayemgusa mtu huyu au mke wake atauwawa.”
12Isaka akapanda mazao katika nchi hiyo na kuvuna mwaka huo vipimo mia, kwa kuwa Yahwe alimbariki.
13Mtu huyo akawa tajiri, naye akaongezeka zaidi hata akawa mkuu sana.
14Alikuwa na kondoo na ngombe na familia kubwa. Wafilisiti wakamwonea wivu.
15Basi visima vyote watumishi wa baba yake walikuwawamevichimba katika siku za Ibrahimu baba yake, Wafilisiti wakavikatalia kwa kwa kuvijaza kifusi.
16Abimeleki akamwambia Isaka, “Ondoka kati yetu, kwa kuwa wewe una nguvu kuliko sisi.”
17Hivyo Isaka akaondoka pale na kukaa katika bonde la Gerari, na kuishi pale.
18Kwa mara nyingine tena Isaka akachimba visima vya maji, vilivyokuwa vimechimbwa siku za Ibrahimu baba yake. Wafilisiti walikuwa wamevizuia baada ya kufa kwake Ibrahimu. Isaka akaviita visima kwa majina aliyokuwa ameviita baba yake.

19Watumishi wa Isaka walipochimba katika bonde, wakaona kisima cha maji yaliyokuwakuwa yakibubujika.
20Wachungaji wa Gerari wakagombana na wachungaji wa Isaka, na kusema, “Haya ni maji yetu.” Hivyo Isaka akakiita kisima hicho “Eseki,” kwa sababu waligombana naye.
21Wakachimba kisima kingine, wakakigombania hicho nacho, hivyo akakiita “Sitina.”
22Akatoka hapo na akachimba kisima kingine, lakini hicho hawakukigombania. Hivyo akakiita Rehobothi, na akasema, “Sasa Yahwe ametufanyia nafasi, na tutafanikiwa katika nchi.”
23Kisha Isaka akaenda Beersheba.
24Yahwe akamtokea usiku huohuo na akasema, “Mimi ni Mungu wa Ibrahimu baba yako. Usiogope, kwa maana mimi nipo pamoja nawe na nitakubariki na kuvidisha vizazi vyako, kwa ajili ya mtumishi wangu Ibrahimu.”
25Isaka akajenga madhabahu pale na akaliita jina la Yahwe. Akapiga hema yake pale, na watumishi wake wakachimba kisima.
26Kisha Abimeleki akamwendea kutoka Gerari, pamoja na Ahuzathi, rafiki yake, na Fikoli, jemedari wa jeshi.
27Isaka akawambia, “Kwa nini mmekuja kwangu, kwani mlinichukia na kunifukuza kwenu.
28Nao wakasema, “Tumeona yakini kwamba Yahwe amekuwa nawe. Hivyo tukaamua kwamba kuwe na kiapo kati yetu, ndiyo, kati yetu nawe. Hivyo na tufanye agano nawe,
29kwamba hautatudhuru, kama ambavyo sisi hatukukudhuru, na kama sisi tulivyokutendea vema wewe na tumekuacha uondoke kwa amani. Kwa kweli, Yahwe amekubariki.”
30Hivyo Isaka akawaandalia sherehe, na wakala na kunywa.
31Wakaamuka mapema asubuhi na wakaapiana kiapo. Kisha Isaka akawaruhusu kuondoka, nao wakamwacha katika amani.
32Siku hiyohiyo watumishi wake wakaja na kumwambia juu ya kisima walichokuwa wamekichimba. Wakasema, “Tumeona maji.”
33Akakiita kile kisima Shiba, hivyo jina la mji ule ni Beersheba hata leo.
34Esau alipokuwa na umri wa miaka arobaini, akajitwalia mke, Yudithi binti Beeri Mhiti, na Basemathi binti Eloni Mhiti.
35Wakamhuzunisha Isaka na Rebeka.