Text copied!
CopyCompare
Biblia ya Kiswahili - Mwanzo

Mwanzo 30

Help us?
Click on verse(s) to share them!
1Raheli alipoona kwamba hamzalii Yakobo watoto, Raheli akamwonea wivu dada yake. Akamwambia Yakobo, “Nipe watoto, sivyo nitakufa.”
2Hasira ya Yakobo ikawaka juu ya Raheli. Akasema, “Mimi ni badala ya Mungu, aliyekuzuilia usipate watoto?
3Akasema, “Tazama, kuna mjakazi wangu Bilha. Lala naye, hivyo aweze kuzaa watoto magotini pangu, nami nitapata watoto kwake.
4Hivyo akampa Bilha mjakazi kama mke wake, na Yakobo akalala naye.
5Bilha akashika mimba na kumzalia Yakobo mwana.
6Kisha Raheli akasema, “Mungu ameamua kwa faida yangu. Ameyasikiliza maombi yangu na kunipa mwana.” Kwa sababu hiyo akamwita jina lake Dani
7Bilha, mjakazi wa Raheli, akashika mimba tena na kumzalia Yakobo mwana wa pili.
8Raheli akasema, “Kwa mashindano yenye nguvu nimeshindana na dada yangu na kushinda.” Akamwita jina lake Naftali.
9Lea alipoona kwamba ameacha kuzaa, akamchukua Zilpa, mjakazi wake, na kumpa Yakobo kama mke wake.
10Zilpa, mjakazi wa Lea, akamzalia Yakobo mwana.
11Lea akasema, “Hii ni bahati njema!” Hivyo akamwita jina lake Gadi.
12Kisha Zilpa, mjakazi wa Lea, akamzalia Yakobo mwana wa pili.
13Lea akasema, “Nina furaha! Kwa maana mabinti wataniita furaha.” Hivyo akamwita jina lake Asheri.
14Siku za mavuno ya ngano Rubeni akaenda shambani na kuona tunguja. Akazileta kwa mama yake. Kisha Raheli akamwambia Lea, “Nipe baadhi ya tunguja za mwanao.”
15Lea akamwambia, “Je ni jambo dogo kwako, kumchukua mme wangu? Je na sasa unataka kuchukua tunguja za mwanangu pia? Raheli akasema, “Kisha atalala nawe leo usiku, kwa kubadilishana na tunguja za mwanao.
16Jioni Yakobo akaja kutoka uwandani. Lea akaenda kumlaki na kusema, “Leo usiku utalala nami, kwani nimekuajiri kwa tunguja za mwanangu.” Hivyo Yakobo akalala na Lea usiku huo.
17Mungu akamsikia Lea, na akashika mimba na kumzalia Yakobo mwana wa tano.
18Lea akasema, “Mungu amenipa ujira wangu, kwa sababu nilimpa mme wangu mjakazi wangu.” Akamwita jina lake Isakari.

19Lea akashika mimba tena na kuzaa mwana wa tano kwa Yakobo.
20Lea akasema, “Mungu amenipa zawadi njema. Sasa mme wangu ataniheshimu, kwa sababu nimemzalia wana sita.” Akamwita jina lake Zabuloni.
21Baadaye akazaa binti na kumwita jina lake Dina.
22Mungu akamkumbuka Raheli na kumsikiliza. Akampa kushika mimba.
23Akashika mimba na kuzaa mwana. Akasema, “Mungu ameiondoa aibu yangu.”
24Akamwita jina lake Yusufu, akisema, Yahwe ameniongeza mwana mwingine.”
25Baada ya Raheli kumzaa Yusufu, Yakobo akamwambia Labani, “Niache niande, ili kwamba niende nyumbani kwetu na katika nchi yangu.
26Nipe wake zangu na watoto wangu niliokutumikia kwa ajili yao, na uniache niondoke, kwani unafahamu nilivyokutumikia.
27Labani akamwambia, “Ikiwa nimepata kibali machoni pako, subiri, kwa sababu nimejifunza kwa kutumia uaguzi kwamba Yahwe amenibariki kwa ajili yako.”
28Kisha akasema, “Taja ujira wako, nami nitalipa.”
29Yakobo akamwambia, “Unajua nilivyokutumikia, na jinsi ambavyo mifugo wako wamekuwa nami.
30Kwani walikuwa wachache kabla sijaja, na wameongezeka kwa wingi. Popote nilipokutumikia Mungu amekubariki. Je ni lini mimi nitaandaa kwa ajili ya nyumba yangu pia?”
31Hivyo Labani akasema, “Je nikulipe nini? Yakobo akasema, 'Usinipe chochote. Ikiwa utafanya jambo hili kwa ajili yangu, nitawalisha tena kondoo wako na kuwatunza.
32Niache nipite kati ya kundi lako lote leo, kwa kuondoa kila kondoo mwenye milia na mabaka, na kila kondoo mweusi kati yao, na kati ya wenye mabaka na milia katika mbuzi. Hawa watakuwa ujira wangu.
33Uadilifu wangu utashuhudia kwa ajili yangu hapo baadaye, utakapokuja kuangalia ujira wangu. Kila ambaye hana milia na hana madoa miongoni mwa mbuzi, na mweusi kati ya kondoo, ikiwa wataonekana kwangu, watahesabiwa kuwa wameibwa.”
34Labani akasema, “Nakubali. Na iwe kama yalivyo maneno yako.”
35Siku hiyo Labani akaondoa mabeberu yaliyokuwa na milia na madoa, na majike ya mbuzi yaliyokuwa na milia na madoa, kila aliyekuwa mweupe, na weusi wote katika mbuzi, akawakabidhi katika mikono ya wanaye.
36Pia Labani akaweka safari ya siku tatu kati yake na Yakobo. Hivyo Yakobo akabaki kuchunga wale kondoo wa Labani waliosalia.

37Yakobo akachukua matawi mabichi yaliyokatwa ya mipopla, mlozi na mwaramoni mbichi akatoa maganda ili michilizi myeupe ionekane, na akaifanya sehemu nyeupe ya ndani ya mti iliyokuwa ndani ya fito ionekane.
38Kisha akaziweka fito alizokuwa amezibambua mbele ya makundi ya kondoo, mbele ya mabirika yakunyweshea walipokuja kunywa maji. Wakashika mimba walipokuja kunywa maji.
39Wanyama wakapandana mbele ya fito; nao wakazaa watoto wenye milia, mabaka na wenye madoa.
40Yakobo akawatenga hawa wanakondoo, lakini akawafanya waliosalia kuelekea wanyama wenye milia na kondoo weusi wote katika kundi la Labani. Kisha akayatenga makundi yake mwenyewe pekee na hakuwaweka pamoja na wale wa Labani.
41Pindi kondoo wenye nguvu katika kundi walipopandana, Yakobo alilaza fito katika mabirika ya maji mbele ya macho ya kundi, ili kwamba washike mimba kati ya fito.
42Lakini wakati waliodhaifu walipokuja, hakuweka fito mbele yao. Hivyo wanyama dhaifu wakawa wa Labani, na wenye nguvu wakawa wa Yakobo.
43Mtu huyo akastawi sana. Akawa na kundi kubwa la kondoo, wajakazi na wajoli, ngamia na punda.