Text copied!
CopyCompare
Biblia Takatifu - Luka - Luka 5

Luka 5:10-28

Help us?
Click on verse(s) to share them!
10Hali kadhalika Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo, waliokuwa wavuvi wenzake Simoni. Yesu akamwambia Simoni, “Usiogope; tangu sasa utakuwa ukivua watu.”
11Basi, baada ya kuzileta zile mashua ukingoni mwa ziwa, wakaacha yote, wakamfuata.
12Ikawa, Yesu alipokuwa katika mmojawapo wa miji ya huko, mtu mmoja mwenye ukoma mwili mzima akamwona. Basi, mtu huyo akaanguka kifudifudi akamwomba Yesu: “Mheshimiwa, ukitaka, waweza kunitakasa.”
13Yesu akaunyosha mkono wake, akamgusa na kusema, “Nataka, takasika!” Mara ule ukoma ukamwacha.
14Yesu akamwamuru: “Usimwambie mtu yeyote; bali nenda ukajionyeshe kwa kuhani, ukatoe sadaka kwa ajili ya kutakasika kwako kama inavyotakiwa na Sheria ya Mose, iwe uthibitisho kwao kwamba umepona.”
15Lakini habari za Yesu zilizidi kuenea kila mahali. Watu makundi mengi wakakusanyika ili kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao.
16Lakini yeye alikwenda zake mahali pasipo na watu, akawa anasali huko.
17Siku moja Yesu alikuwa akifundisha. Mafarisayo na walimu wa Sheria kutoka katika kila kijiji cha Galilaya, Yudea na Yerusalemu, walikuwa wameketi hapo. Nguvu ya Bwana ilikuwa pamoja naye kwa ajili ya kuponyea wagonjwa.
18Mara watu wakaja wamemchukua mtu mmoja aliyepooza maungo, amelala kitandani; wakajaribu kumwingiza ndani wamweke mbele ya Yesu.
19Lakini kwa sababu ya wingi wa watu, hawakuweza kuingia ndani. Basi, wakapanda juu ya dari, wakaondoa vigae, wakamshusha huyo aliyepooza pamoja na kitanda chake, wakamweka mbele ya Yesu.
20Yesu alipoona jinsi walivyokuwa na imani kubwa, akamwambia huyo mtu, “Rafiki, umesamehewa dhambi zako.”
21Walimu wa Sheria na Mafarisayo wakaanza kujiuliza: “Nani huyu anayemkufuru Mungu kwa maneno yake? Hakuna mtu awezaye kusamehe dhambi ila Mungu peke yake!”
22Yesu alitambua mawazo yao, akawauliza, “Mnawaza nini mioyoni mwenu?
23Ni lipi lililo rahisi zaidi: kusema, Umesamehewa dhambi, au kusema, Simama utembee?
24Basi, nataka mjue kwamba Mwana wa Mtu anao uwezo wa kusamehe dhambi duniani.” Hapo akamwambia huyo mtu aliyepooza, “Simama, chukua kitanda chako uende zako nyumbani.”
25Mara, huyo mtu aliyepooza akasimama mbele yao wote, akachukua kitanda chake akaenda zake nyumbani huku akimtukuza Mungu.
26Wote wakashangaa na kushikwa na hofu; wakamtukuza Mungu wakisema: “Tumeona maajabu leo.”
27Baada ya hayo, Yesu akatoka nje, akamwona mtoza ushuru mmoja aitwaye Lawi, ameketi ofisini. Yesu akamwambia, “Nifuate!”
28Lawi akaacha yote, akamfuata.

Read Luka 5Luka 5
Compare Luka 5:10-28Luka 5:10-28