33Kwa hivyo atautawala ukoo wa Yakobo milele, na ufalme wake hautakuwa na mwisho.”
34Maria akamjibu, “Yatawezekanaje hayo, hali mimi ni bikira?”
35Malaika akamjibu, “Roho Mtakatifu atakushukia, na uwezo wake Mungu Mkuu utakujia kama kivuli; kwa sababu hiyo, mtoto atakayezaliwa ataitwa Mtakatifu, Mwana wa Mungu.
36Ujue pia kwamba hata Elisabeti, jamaa yako, naye amepata mimba ingawa ni mzee, na sasa ni mwezi wa sita kwake yeye ambaye watu walimfahamu kuwa tasa.
37Kwa maana hakuna jambo lisilowezekana kwa Mungu.”
38Maria akasema, “Mimi ni mtumishi wa Bwana, nitendewe kama ulivyosema.” Kisha yule malaika akaenda zake.
39Siku kadhaa baadaye, Maria alifunga safari akaenda kwa haraka hadi mji mmoja ulioko katika milima ya Yuda.
40Huko, aliingia katika nyumba ya Zakariya, akamsalimu Elisabeti.
41Mara tu Elisabeti aliposikia sauti ya Maria, mtoto mchanga tumboni mwake Elisabeti akaruka. Naye Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifiu,
42akasema kwa sauti kubwa, “Umebarikiwa kuliko wanawake wote, naye utakayemzaa amebarikiwa.
43Mimi ni nani hata mama wa Bwana wangu afike kwangu?
44Nakwambia, mara tu niliposikia sauti yako, mtoto mchanga tumboni mwangu aliruka kwa furaha.
45Heri yako wewe uliyesadiki kwamba yatatimia yale Bwana aliyokwambia.”
46Naye Maria akasema,
47“Moyo wangu wamtukuza Bwana, roho yangu inafurahi kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.
48Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma mtumishi wake mnyenyekevu. Hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.
49Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu, jina lake ni takatifu.
50Huruma yake kwa watu wanaomcha hudumu kizazi hata kizazi.
51Amefanya mambo makuu kwa mkono wake: amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;
52amewashusha wenye nguvu kutoka vitu vyao vya enzi, akawakweza wanyenyekevu.
53Wenye njaa amewashibisha mema, matajiri amewaacha waende mikono mitupu.
54Amemsaidia Israeli mtumishi wake, akikumbuka huruma yake.
55Kama alivyowaahidia wazee wetu Abrahamu na wazawa wake hata milele.”
56Maria alikaa na Elisabeti kwa muda upatao miezi mitatu, halafu akarudi nyumbani kwake.
57Wakati wa kujifungua kwake Elisabeti ulifika, akajifungua mtoto wa kiume.
58Jirani na watu wa jamaa yake walipopata habari kwamba Bwana amemwonea huruma kubwa, walifurahi pamoja naye.
59Halafu siku ya nane walifika kumtahiri mtoto, wakataka kumpa jina la baba yake, Zakariya.
60Lakini mama yake akasema, “La, sivyo, bali ataitwa Yohane.”
61Wakamwambia, “Mbona hakuna yeyote katika ukoo wake mwenye jina hilo?”
62Basi, wakamwashiria baba yake wapate kujua alitaka mtoto wake apewe jina gani.
63Naye akaomba kibao cha kuandikia, akaandika hivi: “Yohane ndilo jina lake.” Wote wakastaajabu.
64Papo hapo midomo na ulimi wake Zakariya vikafunguliwa, akawa anaongea akimsifu Mungu.
65Hofu ikawaingia jirani wote, na habari hizo zikaenea kila mahali katika milima ya Yudea.
66Wote waliosikia mambo hayo waliyatafakari mioyoni mwao wakisema: “Mtoto huyu atakuwa mtu wa namna gani?” Maana, hakika nguvu ya Bwana ilikuwa pamoja naye.