Text copied!
CopyCompare
Biblia ya Kiswahili - Kutoka

Kutoka 31

Help us?
Click on verse(s) to share them!
1Yahweh akasema na Musa,
2“Angalia, nimemwita kwa jina lake Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila ya Yuda
3Nami nimemjaza Bezaleli na roho ya Mungu, katika hekima, na maarifa, na ujuzi, na mambo ya kazi ya kila aina,
4ili abuni kazi za ustadi, kuwa fundi wa dhahabu, na wa fedha, na wa shaba,
5na kukata vito kwa kutiwa mahali, na kuchora miti, na kufanya kazi ya ustadi iwayo yote.
6Tena, nimemchagua, awe pamoja naye Oholiabu, mwana wa Ahisamaki, wa kabila ya Dani. Nami nimetia hekima katika mioyo ya wote wenye moyo wa hekima, ili wapate kufanya vyote nilivyokuagiza. Hii ni,
7hema ya kukutania na sanduku la ushuhuda, na kiti cha rehema kilicho juu yake, na vyombo vyote vya Hema;
8na meza, na vyombo vyake, na kinara cha taa safi pamoja na vyombo vyake vyote,
9na madhabahu ya kufukizia uvumba; na madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa na vyombo vyake vyote, na birika na tako lake.
10Pia mavazi yenye kufumwa kwa uzuri, na mavazi matakatifu ya Haruni kuhani, na mavazi ya wanawe, ili kutumika katika kazi ya ukuhani.
11Pia mafuta ya kutiwa, na uvumba wa manukato mazuri, kwa ajili ya mahali patakatifu; sawasawa na yote niliyokuagiza ndivyo watakavyofanya wao.
12akasema na Musa,
13“Waambie wana wa Israeli, 'Hakika mtazishika Sabato zangu, kwa kuwa ni ishara kati ya mimi na ninyi katika vizazi vyenu vyote; ili mpate kujua ya kuwa mimi ndimi BWANA niwatakasaye ninyi.
14Basi mtaishika hiyo Sabato; kwa kuwa ni takatifu kwenu; kila mtu atakayeitia unajisi hakika yake atauawa; kwa kuwa kila mtu afanyaye kazi katika siku hiyo, nafsi hiyo itakatiliwa mbali na watu wake.
15Kazi itafanywa siku sita; lakini siku ya saba ni Sabato ya kustarehe kabisa, takatifu kwa BWANA; kila mtu atakayefanya kazi yo yote katika siku ya Sabato, hakika yake atauawa.
16Kwa ajili ya hayo wana wa Israeli wataishika Sabato. Kuiangalia sana hiyo Sabato katika vizazi vyao vyote, ni agano la milele.
17Ni ishara kati ya mimi na wana wa Israeli milele; kwani kwa siku sita Yahweh alifanya mbingu na nchi, akastarehe kwa siku ya saba na kupumzika.
18Hapo Mungu alipokuwa amekwisha zungumza na Musa katika mlima wa Sinai, akampa hizo mbao mbili za ushuhuda, mbao mbili za mawe, zilizoandikwa kwa mkono wake.