1Basi kulikuwa na Farisayo ambaye jina lake Nikodemo, mmoja wa wajumbe wa baraza la Wayahudi.
2Mtu huyu alimwendea Bwana Yesu usiku na akamwambia, “Rabi, tunajua ya kuwa u mwalimu kutoka kwa Mungu, kwa maana hakuna mtu awezaye kutenda ishara hizi zote Mungu asipokuwa pamoja naye.”
3Yesu akamjibu, “Amini, amini, mtu hawezi kuingia katika ufalme wa Mungu asipozaliwa mara ya pili.”
4Nikodemo akasema,” Mtu anawezaje kuzaliwa akiwa mzee? Hawezi kuingia tumboni mwa mama yake mara ya pili na kuzaliwa, je anaweza?”
5Yesu akajibu, “Amini, amini mtu sipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuingia katika ufalme wa Mungu.
6Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili, na kilichozaliwa kwa Roho ni roho.
7Usishangae kwa sababu nilikuwambia, 'ni lazima kuzaliwa mara ya pili.'
8Upepo huvuma popote upendapo na sauti yake mwaisikia, lakini hamjui utokako wala uendako. Ndivyo ilivyo hali ya kila aliyezaliwa na roho.
9Nikodemo akajibu, kwa kusema, “Mambo haya yawezekanaje?”
10Yesu akamjibu, “Wewe u mwalimu wa Israeli, hata hauyajui mambo haya?
11Amini, amini, nakuambia, kile tunachokifahamu twakishuhudia kwa kile tulichokiona. Lakini hampokei ushuhuda wetu.
12Kama nimewambia mambo ya hapa duniani na hamuamini, mtawezaje kuamini kama nikiwambia mambo ya mbinguni?
13Maana hakuna aliyepanda juu kutoka mbinguni isipokuwa yeye aliyeshuka, Mwana wa Adamu.
14Kama vile Musa alivyomwinua nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu lazima ainuliwe,
15ili kwamba wote watakaomwamini wapate uzima wa milele.
16Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, kwamba akamtoa mwanae wa pekee, ili kwamba mtu yeyote amwaminiye asiangamie bali awe na uzima wa milele.
17Kwa sababu Mungu hakumtuma mwanae duniani ili auhukumu ulimwengu, bali kwamba ulimwengu uokolewe katika yeye.
18Amwaminiye Yeye hatahukumiwa. Yeye asiyemwamini tayari ameshahukumiwa kwa sababu hajaliamini jina la Mwana pekee wa Mungu.
19Hii ndiyo sababu ya hukumu, ya kwamba nuru imekuja ulimwenguni, lakini wanadamu wakapenda giza zaidi ya nuru kwa sababu matendo yao yalikuwa maovu.
20kila mtu atendaye mabaya huichukia nuru wala haji nuruni ili matendo yake yasije yakawekwa wazi.
21Lakini, yeye atendaye kweli huja kwenye nuru ili matendo yake yaonekane kwamba yametendwa kwa utiifu wa Mungu.
22Baada ya haya, Yesu pamoja na wanafunzi walienda katika nchi ya Yudea. Huko alitumia muda pamoja nao na alikuwa akibatiza.
23Sasa Yohana pia alikuwa akibatiza huko Ainea karibu na Salim maana kulikuwa na maji mengi pale. Watu walikuwa wakija kwake na kubatizwa,
24kwa kuwa Yohana alikuwa hajatupwa gerezani.
25Kisha palitokea mabishano kati ya wanafunzi wa Yohana na Myahudi kuhusu sikukuuu za utakaso.
26Wakaenda kwa Yohana wakamwambia, “Rabi, yeye uliyekuwa naye ng'ambo ya Mto Yorodani, yeye uliyeshuhudia habari zake, tazama, anabatiza na wote wanaenda wanamfuata.”
27Yohana akajibu mtu hawezi kupokea kitu chochote isipokuwa kama amepewa kutoka mbinguni.
28Ninyi wenyewe mwashuhudia kuwa nalisema kuwa, 'mimi sio Kristo', badala yake nilisema, 'nimetumwa mbele yake.'
29Yeye aliye na bibi arusi ni bwana harusi. Sasa rafiki wa bwana arusi, asimamaye na kusikiliza hufurahia sana kwa sababu ya sauti ya bwana arusi. Hii sasa ni furaha yangu iliyotimilika.
30Anapaswa kuzidi, nami napaswa kupungua.
31Yeye atokaye juu, yu juu ya yote. Yeye aliye wa ulimwengu anatoka ulimwenguni na huongea mambo ya ki ulimwengu. Yeye atokaye mbinguni yuko juu ya yote.
32Yeye hushuhudia yale aliyoyaona na kuyasikia, lakini hakuna apokeaye ushuhuda wake.
33Yeye aliye pokea ushuhuda wake amehakikisha kuwa Mungu ni mkweli.
34Kwa sababu yeye aliyetumwa na Mungu huongea maneno ya Mungu. Kwa kuwa hampi Roho kwa kipimo.
35Baba humpenda Mwana na amempa vitu vyote mikononi mwake.
36Yeye amwaminiye Mwana anao uzima wa milele, lakini kwa yeye asiye mtii Mwana hatauona uzima, bali ghadhabu ya Mungu hushikamana juu yake.